AWAMU ya tatu ya programu ya ufadhili wa masomo ngazi ya shahada ya uzamili katika uhandisi wa nishati imezinduliwa huku ikitarajiwa kutoa ufadhili kwa wanawake 10 wa Kitanzania.
Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam, mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Abasi Kitogo amesema watakaoruhusiwa kutuma maombi ni wenye umri wa chini ya miaka 35, na wawe na ufahamu wa masuala ya nishati.
Amesema dirisha la maombi litafunguliwa kesho Julai 15 na litakuwa wazi kwa miezi miwili na kufungwa Septemba 15, mwaka huu, huku akitoa wito kwa wanawake wenye ndoto ya kuwa wahandisi wa nishati kuchangamkia fursa hiyo.
“Kama shirika tunalioni hili kama jukumu la muhimu hasa katika kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabianchi kwasababu matumizi sahihi ya nishati inasaidia sana kupunguza uzalishaji wa hewa chafu. Kama UNDP tutaangalia namna ya kuongeza wigo zaidi wa mafunzo katika programu hii,” alisema.
Amesema programu hiyo ni muhimu na inawasaidia kusukuma mbele ajenda ya matumizi bora ya nishati nchini.
Amesema kwa utamaduni wa Tanzania wahandisi wengi walikuwa ni wanaume lakini sasa programu hiyo imezalisha wahandisi wa kike, na kwamba hao ndio wenye uchungu wa matumizi bora ya nishati kwasababu inawagusa kwa asilimia kubwa, akisema watasaidia kujua umeme na ada ‘bills’ mbalimbali zinalipwaje.
“Hivi karibuni kulikuwa na mkutano mkubwa wa nishati ulifanyika Tanzania ulikutanisha maraisi karibu wote wa Afrika, walikuja nchini kwasababu tunaonekana kupiga hatua kwa matumizi ya nishati, sasa programu hii inatujengea uwezo katika kusukuma ajenda ya nishati na kuhakikisha inatekelezwe vizuri.
“Nishukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Umoja wa Ulaya (EU), na Ubalozi wa Ireland, kwakweli tumeanza kuona mabadiliko, sasa hivi hata ajira mpya serikalini unaona karibu namba inaelekea kulingana kati ya wahandisi wa umeme wanawake na wanaume,” amesema Nyamanga.
Aidha, ameeleza kuwa mwisho wa programu hiyo watakapopata wahakiki ubora au wanaufanisi wa masuala ya umeme, watawasaidia sana kupunguza matumizi ya nishati hiyo, akieleza kuwa wanazingatia upataji wa umeme lakini pia na kujua kwamba unatumikaje.
Sherida Magomele, miongoni mwa wanufaika wa programu hiyo awanu zilizopita alisema kabla hajaingia kwenye mafunzo hayo alikuwa akitamani kuwa mhandisi mkubwa katika masuala ya nishati, na kwamba kwa sasa amefurahi kuona matamanio yake yamefanikiwa.
“Ufadhili huu umekuwa na umuhimu mkubwa kwangu kwasababu umenifanikishia kutimiza ndoto na kuongeza vitu vingi ikiwemo ujuzi mkubwa ambao utatumika kuhamasisha matumizi sahihi ya nishati kwa ukubwa wake,” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED