UANDISHI wa habari na mawasiliano kwa umma ni taaluma muhimu kwa maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi si kwa Tanzania na Afrika pekee bali kwa dunia nzima. Ni tasnia ambayo inategemewa na sekta zote kwa ajili ya kuuhabarisha umma kuhusu mambo yanayoendelea ama katika sekta au tasnia husika.
Kwa maneno mengine, hakuna taaluma isiyohitaji waandishi wa habari ili kutoa ujumbe kwa hadhira iliyokusudiwa. Hata wanasiasa wakiwamo viongozi wakuu wa serikali, wanapotaka kutoa taarifa kwa umma, ni vyombo vya habari kupitia waandishi wa habari, ndivyo vinavyotumika.
Kwa Tanzania, kila uchao kupitia mitandao ya kijamii, viongozi wa kisiasa wamekuwa wakiwaalika waandishi wa habari kuhudhuria mkutano kwa ajili ya kutoa ujumbe kwa umma. Kwa maana nyingine, bila vyombo vya habari kuuhabarisha umma, hakuna kitakachojulikana.
Hivi sasa Rais Samia Suluhu Hassan yuko katika ziara ya kikazi mkoani Tanga na ni vyombo vya habari ndivyo vinavyotumika kutoa taarifa kuhusu ziara hiyo na mambo anayoyafanya mkoani humo. Pia hivi sasa, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, anaumwa huku vyombo vya habari vikitoa taarifa za maendeleo ya afya yake siku kwa siku. Yote hiyo ni kuonesha umuhimu wa vyombo vya habari kwa masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Pamoja na umuhimu wa tasnia ya habari kwa maendeleo endelevu katika nyanja anuai, wanahabari wamekuwa wakionekana watu wa daraja la chini na wamekuwa wakitolewa lugha mbaya na hata kufanyiwa vitendo vya ajabu na baadhi ya wahusika.
Mwaka 2001 mjini Dodoma wakati Bunge likiendelea na Mkutano wa Bajeti, walifika watu kutoka Afrika Kusini waliokuwa na nia ya kuwekeza katika mradi wa chuma na makaa ya mawe Liganga na Mchuchuma, Ludewa mkoani Njombe. Wakati wa mazungumzo baina ya serikali na wawekezaji hao, waandishi walikaribishwa kuandika habari kuhusu mpango huo ambao serikali ikiongozwa na Wizara ya Viwanda na Biashara iliunadi kwa nguvu zote.
Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, ratiba ya chakula ilifuata lakini cha kushangaza, alitokea ofisa kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na kuwazuia wanahabari kushiriki tendo hilo. Ofisa huyo bila aibu alisema: “Waandishi hamruhusiwi kwenda kwenye chakula, Waziri anaweza kudondokewa na mchuzi halafu mkamwandika kwenye magazeti yenu!”
Kauli hiyo iliwafanya waandishi wa habari kuondoka eneo la tukio na kukubaliana kutokuripoti habari hiyo kwa kile walichodai kuwa wamedhalilishwa na ofisa huyo wa serikali.
Yako matukio mengi ambayo yameoneshwa na baadhi ya maofisa wa serikali na wanasiasa ambayo yanatweza utu wa wanahabari na taaluma kwa ujumla. Miongoni mwa matendo hayo ni wanahabari kutumiwa na maofisa na wanasiasa hao kuwaandisha lakini baadaye wanawatelekeza.
Hivi sasa, kwa mfano, mwandishi wa habari amefariki dunia mkoani Mbeye na wengine watatu kujeruhiwa wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Taarifa ya Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya inabainisha kwamba waliolazwa katika Hospitali ya Rufani ya Kanda Mbeya ni kama wametelekezwa kwa kuwa hakuna kiongozi anayewajali na hawapati matibabu ipasavyo kwa sababu hawana bima ya afya.
Mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu, hivyo wanahabari watatumika sana kwenye misafara ya kampeni ya wanasiasa kutoka vyama mbalimbali vya siasa sehemu nyingi nchini. Kama mambo ya kuwadharau wanahabari hayatakemewa na hatua kuchukuliwa, hadithi itakuwa ile ile.
Ni rai kwamba taaluma ya uandishi wa habari ina umuhimu sawa na zingine kwa maendeleo ya nchi, hivyo ni vyema ikaheshimiwa. Wanahabari wasionekane kama madekio, sabuni za kuwasafishia watu au ngazi ya kuwapandishia juu watu fulani na baada ya hapo wanadharauliwa na kuonekana si lolote si chochote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED