MWENGE wa Uhuru juzi ulianza rasmi mbio zake kwa mwaka 2025 ambazo zitatamatika Oktoba 14 ambapo pia huadhimishwa kama Kumbukumbu ya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, maarufu kama Siku ya Kumbukumbu ya Nyerere.
Mwenge huo ambao kaulimbiu yake kwa mwaka huu ni ‘Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu’, ulizinduliwa rasmi katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani na mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango. Mbio za Mwenge huo zinatarajiwa kufanyika katika mikoa yote, ikiwamo ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Wakati wa uzinduzi wa mbio hizo, Dk. Mpango aliagiza wakimbiza Mwenge kufichua vitendo vya udhalimu na ubadhirifu wa mali za umma bila woga. Pia aliwaagiza viongozi wa mikoa na wilaya kutoa ushirikiano kwa wakimbiza Mwenge hao katika maeneo yote utakaopita kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za serikali, wafadhili na nguvu za wananchi.
Wakati wa mbio za Mwenge kila mwaka, katika mikoa na wilaya, kumekuwa na matukio mbalimbali ya ukaguzi na uzinduzi wa miradi Pamoja na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ile ambayo huanza kutekelezwa.
Katika miaka ya karibuni, kumekuwa na taarifa mbalimbali kupitia vyombo vya habari kuhusu madudu yanayobainishwa kwenye mbio hizo. Miongoni mwa madudu hayo ni baadhi ya miradi ya maendeleo kujengwa chini ya kiwango, upigaji wa fedha za miradi na kutokutekelezwa kwa wakati kama ilivyoainishwa katika mikataba.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya miradi imekuwa ikikataliwa kutokana na sabau zilizotajwa hasa kutekelezwa katika viwango duni au baadhi ya fedha zilizotolewa kupitia serikali au wafadhili kutojulikana ziliko. Kwa hatua hiyo, ni wazi kwamba Mwenge wa Uhuru umekuwa na faida kubwa katika kuibua mambo yaliyojificha na wahusika kuwajibishwa baada ya uchunguzi kuthibitisha kuwapo ubadhirifu.
Wakati wa mbio za Mwenge za mwaka 2023, kwa mfano, aliyekuwa Kiongozi wa Mbio hizo alikuwa akitoa taarifa mbalimbali baada ya kukuta madudu kwenye miradi. Aliwahi kukataa kufungua kituo cha afya katika wilaya ya Longido mkoani Arusha na mradi wa maji wilayani Mwanga, Kilimanjaro kwa sababu ilikuwa imejengwa kwa viwango duni.
Hiyo ni mifano michache tu lakini iko mingi katika sehemu mbalimbali kwenye mikoa yote ya Tanzania ambayo imekuwa ikiripotiwa kuwa katika viwango visivyoridhisha na kuwapo kwa shaka kuwa sehemu ya fedha za miradi hiyo zimekwenda katika mikono ya baadhi ya watumishi wasio waaminifu.
Ni dhahiri kwamba wananchi katika maeneo mbalimbali Tanzania, wanakabiliwa na kero mbalimbali kama vile ubovu wa Barabara ambazo zinakwamisha usafiri kwa wananchi, maji, huduma za afya na ukosefu wa masoko. Kutokana na hali hiyo, serikali imekuwa ikipeleka mabilioni ya fedha kwa ajili ya kutatua kero hizo za wananchi lakini baadhi ya watendaji wamekuwa wakifanya ubadhirifu na Mwenge umekuwa ukianika mambo hayo.
Wakati umefika sasa Mbio za Mwenge za mwaka 2025 zianike madudu yote yanayosababisha kero kwa wananchi. Kufichua madudu hayo hakutoshi bali jambo la muhimu ni wanaohusika na matatizo hayo yachukuliwe hatua kuwa zaidi ambazo zitasaabisha wengine kuwa macho na tahadhari na fedha za serikali ambazo sehemu kubwa ni za walipakodi.
Si kwamba serikali imekuwa haichukui hatua. La hasha! Bali imeshuhudiwa watu mbalimbali wakiwajibishwa kwa kusimamishwa kazi na kuondolewa baada ya kubainika kuhusika na wale wateule wa Rais, uteuzi wao umekuwa ukitenguliwa.
Hatua hizo pekee hazitoshi bali wanaobainika kuhusika na madudu hayo, wanapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili wachukuliwe hatua kubwa ikiwamo kufungwa iwapo itathibitika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED