Hongera kwa ubunifu wa kunusuru watoto

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 12:04 PM Apr 22 2025
Watoto.
Picha:Mtandao
Watoto.

TANZANIA imepiga hatua kubwa katika masuala ya elimu ikiwamo kuanzisha sekondari za kata kuwa na shule mbili za msingi katika kijiji, na sasa zinajengwa sekondari kila kijiji, ili kusogeza elimu karibu. Hatua hiyo pia imesaidia watoto wengi kwenda shule, hasa baada ya serikali kurejea mfumo wa elimu bure ili hata watoto wanaotoka katika familia duni waweze kupata elimu.

Lakini pamoja na jitihada hizo, kumekuwapo na changamoto mbalimbali ambazo kwa namna moja au nyingine, zinakwamisha maendeleo ya elimu kutokana na wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani. Miongoni mwa changamoto hizo ni ukosefu wa chakula shuleni. 

Lakini imekuwa ikielezwa na wataalamu wa afya kuwa chakula shuleni ni moja ya njia muhimu za kuboresha afya, kujifunza na ukuaji wa watoto. Inaelezwa kuwa watoto wanaopata lishe bora wakiwa shuleni wana uwezo wa kujifunza vizuri zaidi na kukua kwa afya njema, kwamba chakula shuleni husaidia kuboresha afya ya wanafunzi kwa kuwapatia virutubisho wanavyohitaji kwa ukuaji na maendeleo.

 Hata hivyo, pamoja na umuhimu huo, suala la chakula shuleni limekuwa ni changamoto kwa baadhi ya shuleni, kutokana na baadhi ya wazazi na walezi kutokuwa tayari kuchangia. Mazingira hayo yanaibuliwa katika mkutano wa siku tatu wa wadau wa elimu wa Musoma Vijijini mkoani Mara, wakati wakijadili mbinu mbalimbali za kuboresha elimu.

Mkutano huo ulifanyika hivi karibuni na kujadili kwa kina changamoto zinazokaili elimu katika eneo hili na kuibuka na kampeni iliyopewa jina la "Mkomboe Nyangeta na Athumani Kielimu". Ukosefu wa chakula shuleni ni miongoni mwa changamoto zilizoibuliwa na kuamuliwa kwamba sasa suala la chakula kwa wanafunzi shuleni litakuwa ni la lazima, huku watendaji wa vijiji wakitakiwa kuanza utekelezaji kwa kuwashirikisha wazazi na walezi. 

Inaelezwa kuwa katika mazingira hayo mengine mengi au uhaba wa walimu, vinatajwa kuwa chanzo cha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za Musoma Vijijini kufanya vibaya katika mitihani yao. Hivyo, wameamua kuja na kampeni ya Mkomboe Nyangeta na Athuman Kielimu kwa kuhamasisha wazazi na walezi kutambua umuhimu wa elimu na kuwa tayari kuchangia chakula na kufuatila maendeleo ya watoto wao shuleni ili kuhakikisha wanasoma.

 Binafsi ninaona kampeni hiyo ni nzuri na inaweza kuwa na mchango mkubwa wa maendeleo ya elimu iwapo wazazi na walezi wakijihusisha kikamilifu katika kuhudumia watoto wao wawapo shuleni. Ninajua wapo baadhi ya wazazi na walezi ambao wamekuwa wakihoji kwa nini watoe chakula kwa watoto wao wakati elimu ilishatangazwa kutolewa  bure, na kwamba ni jukumu la serikali kutoa chakula.

 Serikali imeanzisha huduma ya chakula shuleni kama njia ya kuboresha elimu na umakini wa wanafunzi wakiwa shuleni, ili kuongeza ufaulu wao. Hii inalenga kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata lishe bora wanapokuwa shuleni. Hata hivyo, ninadhani kuna uelewa mdogo miongoni mwa jamii kuhusu umuhimu wa utoaji wa chakula shuleni. 

Hivyo Musoma Vijijini wana kampeni hiyo, ni vyema wakumbuke kuwa kuna haja ya kuielimisha.  Wazazi, walezi na jamii kwa ujumla wakipata elimu kuhusu umuhimu wa chakula shuleni, ninaamini hata kampeni ya "Mkomboe Nyangeta na Athuman Kielimu" itakuwa na matokeo chanya. Yawezekana wapo wanaamini kuwa kuchangia chakula shuleni ni kupoteza fedha au ni matumizi mabaya ya fedha, bila kuelewa kuwa chakula hicho kinachangwa kwa ajili ya lishe ya watoto wao.