MADEREVA 759 wa bodaboda wamefariki dunia kutokana na ajali kati ya mwaka 2022 na 2024, huku wananchi wa kawaida 283 nao wakiwa wamefariki dunia kutokana na ajali za bodaboda katika kipindi hicho.
Hayo yamo katika taarifa ya hivi karibuni ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Fatuma Hassan Toufiq.
Kwa hali kama hiyo, ni wazi kuna umuhimu kwa watu kuwa salama kwa kufuata sheria za usalama barabarani ili kujiepusha na ajali ambazo wakati mwingine si za lazima ingawa ajali haina kinga.
Udereva wa bodaboda ni ajira ambao imesaidia kuwaingiza kipato vijana mbalimbali nchi, lakini tatizo limekuwa ni kutozingatia suala la usalama ambalo ni kufuata sheria za usalama barabarani.
Ili kuboresha au kustawisha biashara hiyo ya kusafirisha abiria, waendesha pikipiki hao watakiwa kufuata sheria ya usalama barabarani kwa usalama wao, abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Ninaamini kwamba kama watafuata sheria na taratibu za usalama barabarani, itakuwa ni njia salama ya usafirishaji wa abiria, tofauti na sasa ambapo wamekuwa wakisababisha ajali.
Ikumbukwe ongezeko la bodaboda lina uhusiano wa kiuchumi, kutokana na kwamba zinaagizwa kutoka nje na kulipiwa kodi, lakini madereva wenyewe wanapaswa kusoma na kulipia leseni zao za udereva.
Hivyo, kazi ya kuendesha bodaboda, ni biashara pia ni ajira kama zilivyo ajira nyingine halali zinazowaingizia watu vipato vya kuendeshea maisha yao ya kila siku. Hivyo madereva wanapaswa kulinda ajira hizo.
Lakini bahati mbaya, baadhi ya vijana ambao wameingia katika ajira hiyo ni kama wamekuwa wazito kuelewa umuhimu wa ajira hiyo na kuiheshimu ili iweze kuwanufaisha na familia zao.
Ninaeleza hivyo, kwa sababu kila uchao wamekuwa wakiibuka na mitindo ambayo ni hatari kwa maisha yao, aidha kwa kuelewa au kutoelewa madhara ya kile wanachokifanya wawapo barabarani.
Wakati wakiendelea kupoteza maisha kwa ajali, wapo waliokuja na mtindo wanaouona wa kawaida, lakini unaweza kuwasababishia madhara makubwa iwapo wataendelea nao au wasipodhibitiwa.
Kwa mafuno wakiwa ni kama wamiliki wa barabara ambapo huendesh vyombo hivyo vya moto kwa fujo bila tahadhari huku wakifanya vituko vya kuachia usukani, wanapokuwa katika msafara wa kusindikiza mwenzao aliyefariki dunia kwa ajali.
Katika mazingira hayo, wengine hubebana hata wanne kwenye bodaboda moja, wengine wakiendesha huku wamesimama. Yaani hufanya kila aina ya vituko barabarani, ambavyo ni hatari kwa usalama wao.
Vilevile, kuna kero ambayo madereva hao wanachangia ya kutawala pande zote za barabara kwa muda na kusababisha watu wengine washindwe kuitumia kana kwamba ni mali yao.
Kwa Dar es Salaam imekuwa, hilo limekuwa kama jambo la kawaida kusikia honi nyingi zikipigwa pale wanapokuwa wakisindikiza msafara wa msiba wa mwenzao huku wametanda barabara yote.
Madereva wa bodaboda wanapaswa kushtuliwa na takwimu za vifo vyao ili wachukue hatua sahihi za kutii sheria bila shuruti ili wawe salama wawapo barabarani badala ya kujiendea tu kama ilivyo sasa.
Lakini pia ni vyema watambue kuwa wanajiweka katika mazingira ya kuhatarisha maisha yao kwa kutotii sheria za usalama barabara ambazo kimsingi ndizo zinazoweza kuwafanya wawe salama.
Tanzania bila ajali za bodaboda zisizo za lazima inawezekana iwapo madereva watakubali kutii sheria bila shuruti, lakini wasipofanya hivyo, wataendelea kusababisha ajali zaidi na kupoteza uhai.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED