ZIMEBAKI raundi tatu kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa baadhi ya timu, zingine zikisalia na michezo minne, chache zikiwa na michezo zaidi ya hiyo.
Vita iliyokuwapo hapo ni baadhi ya timu zinasaka ubingwa, zingine zikisaka kuwapo ndani ya nne bora ili zicheze mechi za kimataifa, zipo zinazojiongezea pointi ili zisiingie katika hatari ya kucheza mechi za mchujo.
Katika timu hizo 16 zinazocheza Ligi Kuu, kuna zilizo kwenye hali mbaya ambazo zinajipapatua ili zisishuke daraja na ambazo zinapambana ili kutoka kwenye mtego wa kucheza 'play off'.
Ukichana na Ligi Kuu, kuna Ligi ya Championship, ambayo timu zake zinasaka nafasi ya kupanda Ligi Kuu kwa ajili ya msimu ujao, mbili zilipanda moja kwa moja.
Timu zitakazoshika nafasi ya tatu na ya nne zitacheza mechi ya mchujo ili kupata timu moja ambayo itaisubiri timu itakayofungwa kwenye 'play off' ya Ligi Kuu ili kupata mshindi ambaye, atabaki Championship, atapanda, au atashuka daraja kwa kutegemea ni timu gani iliyoshinda, kutoka Ligi ya Championship.
Kwa maana hiyo sasa hivi timu nyingi zimeongeza umakini mkubwa tofauti na ilivyokuwa katika michezo ya mwanzo wa msimu.
Ni michezo ambayo viongozi, benchi la ufundi na wachezaji wanakuwa wamoja, wakiwa kwenye ushirikiano mkubwa ili kuwezesha malengo yao, kutwaa ubingwa, kubaki Ligi Kuu, au kuhakikisha hawashuki daraja.
Hii ndiyo michezo ambayo utaona timu na wachezaji wakitoa asilimia kubwa ya jasho na kujituma uwanjani kuliko wakati mwingine wowote.
Ni wakati ambao baadhi ya viongozi huwaahidi wachezaji pesa, motisha, vile vile hata viongozi wa serikali za mikoa tunashuhudia wakihusika kuongezea hamasa na morali kwa wachezaji.
Kwa hali kama hii sasa inahitaji uangalizi mkubwa kutoka kwa Bodi ya Ligi na waamuzi wanaochezesha ili kila timu ishinde kwa haki.
Macho ya waangalizi wa bodi yanatakiwa yawe makini kuangalia mambo mbalimbali ili kuepukana na upangaji wa matokeo, uonevu na rushwa kutoka kwa baadhi ya waamuzi.
Zipo timu ambazo kwa sasa zinacheza bila presha ya kushuka daraja au kuchukua ubingwa.
Kama zikicheza na timu ambazo zinahitaji pointi tatu ili kujipambanua kushuka daraja inabidi zimulikwe kwa makini kwani kuna uwezokano na kulegeza ili kuibeba timu hitaji.
Wapo baadhi ya waamuzi ambao kwa makusudi wanaamuzi kuzibeba timu wanazohitaji zishinde kwa manufaa yao.
Hali hii inaweza kusababisha kupatikana kwa bingwa asiyestahili, timu dhaifu zinazopanda daraja na kuja kutoa ushindani hafifu, kushusha daraja timu zisizostahili na kuzibakisha ambazo hazikustahili.
Huu ndiyo wakati sasa wa waamuzi kuonyesha uwezo wao na kulisaidia soka la Tanzania kuziweka timu zote sehemu zinazostahili kubwa kwa kuchezesha kwa haki.
Bodi ya Ligi nayo huu ndiyo wakati wa kuchunguza timu na wachezaji wanaouza mechi, viongozi wanaonunua au kuuza michezo na waamuzi ambao hawatendi haki kwenye maamuzi yao kwa ajili ya kuzipendelea timu ambazo wao wanataka zishinde kwa manufaa yao binafsi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED