WIKI hii Jumamosi Aprili 26, ni kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ndio umetupa Tanzania. Tanganyika na Zanzibar ziliungana Aprili 26 mwaka 1964, zikiunganishwa na waasisi Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume.
Maisha ya miaka 61 ya Muungano imeshuhudia mafanikio mengi hasa kudumisha ulinzi na usalama wa Bara na Visiwani, kuwapo amani na maelewano, uvumilivu na ukomavu kisiasa, kukuza uchumi, kuimarisha demokrasia na usawa wa kijinsia.
Tanzania na Zanzibar zimekuwa mashuhuri kwenye utalii visiwani kukikaribia kuwa kitovu cha utalii barani Afrika. Kwa ujumla, Watanzania wanajivunia Muungano kwa mambo mengi.
Wanajivunia kuanzia kimikakati, kijiografia, kitamaduni, kibiashara, kisiasa na kiusalama ambavyo vimeendelea kuwaunganisha watu wa Zanzibar na Tanzania Bara kama taifa moja
Pamoja na hayo, Tanzania inajivunia kuwa na Rais mwanamke ambaye anatoka Zanzibar upande wa pili na Muungano.
Hilo linazidi kuidhihirisha ukweli kwamba Watanzania wote ni waamini wa Muungano bila kujali kwamba kiongozi anatoka upande upi au jinsi yake.
Ndani ya miaka 61 ya Muungano huo, viongozi wa serikali wamefanikiwa kupunguza kero 25 za zilizokuwa zikilalamikiwa hadi kubakia nne zinazoendelea kupunguzwa hatimaye ikabaki ziro.
Kero hizo nne ni mgawanyo wa mapato yatokanayo na hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na faida kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Zingine ni mapendekezo ya tume ya pamoja ya fedha, usajili wa vyombo vya moto na uingizaji wa sukari kutoka Zanzibar katika soko la Tanzania Bara.
Hizo zinaendelea kushughulikiwa na kufanyiwa kazi, tunawapongeza viongozi na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulika na Muungano kwa juhudi hizo.
Wapokee maua yao, kama wamefanikiwa kumaliza kero nyingi na kubaki chache, ni wazi zilizobaki itakuwa ni rahisi kuzimaliza ili kuendelea kulinda Muungano huo ambao unaweza kuwa wa mfano kwa kuduumu muda mrefu. Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk. Selemani Jafo.
Anasema kwamba katika kuimarisha na kulinda Muungano, pande zote mbili zimekuwa kwenye majadiliano ya kumaliza kero nne ambazo hazijapatiwa ufumbuzi. Kwa maelezo hayo ya Waziri Jafo, ni wazi kwamba serikali mbili zitaweza kufanya kila iwezekanavyo ili kumalizia kero zilizobaki, kwa manufaa ya pande mbili za Muungano. Kuzitatua kero hizo ni sawa na kumaliza manung'uniko yaliyokuwapo ambayo wananchi wanaona hayana manufaa kwao, hivyo tunapoadhimisha miaka 61 ya Muungano, zifanyike jitihada za kuhakikisha kero zote zinamalizwa. Miaka 61 si haba, kwani aliyezaliwa wakati huo kwa sasa ni mtu mzima mwenye wajukuu. Tukumbuke ipo haja ya kuendelea kuudumisha na kujivunia umoja na mashikamano uliopo ndani ya Muungano bila kuwapo kero. Wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar hawana budi kupongezwa kwa jinsi wanavyoendelea kuulinda kwa manufaa yao na vizazi vijavyo, licha ya kuwapo kero zinazowagusa.
Ikumbukwe kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni wa mfano duniani, kwani ni wa dola mbili huru zilizoungana na kuunda nchi moja yenye serikali mbili zinazofanya kazi zake kwa umakini. Muungano huo ulianzishwa ili kupanua maeneo ya kiuchumi, heshima kimataifa, amani, umoja kwenye masuala ya ulinzi na usalama katika mataifa haya mawili tunatamani uendelee zaidi kwa manufaa ya pande zote Ndani ya miaka 61 kukaa pamoja, lazima yanakuwapo haya na yale, lakini wananchi wameendelea kuvumiliana, serikali zikifanya jitihada za kumaliza kero ambazo wanalalamikia. Zipo nchi mbalimbali zilizowahi kuungana ikiwamo Ghana na Guinea ambazo ziliungana mwaka 1958 baadaye Mali nayo ilijiunga nazo, lakini muungano huo haukudumu ukasambaratika. Vilevile, kulikuwa na muungano wa nchi za Senegal na Gambia, ambao baadaye ulisambaratika mwaka 1989, lakini kwa Tanzania imekuwa tofauti, kwani ndani ya kero umeendelea kuwapo na kuimariki zaidi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED