KATIKA majiji mengi nchini kilio kikubwa ni kuzagaa kwa taka ambazo zinadaiwa kutozolewa kwa muda mrefu na kuharibu mazingira hali inayosababisha miji hiyo kuonekana michafu.
Ki ukweli suala la taka za plastiki limepatiwa ufumbuzi baada ya kupigwa marufuku kwa mifuko ya aina hiyo na vilevile, urejeleshaji wa chupa za plastiki umesaidia kwa kiasi kikubwa chupa kutosambaa ovyo.
Hata hivyo, bado kuna tatizo la taka ngumu, ambazo zinaweza kurejeleshwa na kuwa fursa ya kuwainua watu kiuchumi.
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limewataka Watanzania kuanza kubadili mtazamo na kuziona taka kama fursa ya kuzirejeleza na kupata bidhaa mbalimbali na kujikomboa kiuchumi.
Kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Kuondoa Taka, iliweka msisitizo kuwa taka si uchafu bali ni malighafi yenye thamani endapo itasimamiwa na kutumika vyema.
Siku hiyo ilianzishwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Desemba 2022 ili kukuza mifumo endelevu ya matumizi na uzalishaji na kuongeza uelewa kuhusu udhibiti wa taka.
Pia, ilianzishwa kwa lengo la kuhimiza mazoea ya kuwajibika ya kupunguza taka ulimwenguni na kwa Tanzania NEMC iliahidi kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa ukusanyaji taka.
Kama ilivyo kwa chupa za plastiki ambazo kwa sasa zinatoa ajira kwa watu wengi kwa kuziokota na kuzipeleka kwenye viwanda vinavyotengeneza bidhaa za plastiki na kufanya maeneo mengi kuwa safi, chupa za vioo pia zimeanza kuwakomboa vijana wengi.
Kaulimbiu ya siku hiyo kimataifa ni kuwezesha taka sifuri kwenye sekta ya nguo na mitindo na kwa kuzingatia dhana ya punguza, tumia tena na rejeleza, Tanzania itajenga jamii inayojali mazingira na kuchochea uchumi mzunguko kwa maendeleo endelevu ya taifa letu.
Katika kuadhimisha siku hiyo, NEMC inahimiza na kuhakikisha kuwa dhana ya punguza, tumia tena na rejeleza katika sekta zote za uzalishaji inatekelezwa kwa vitendo.
NEMC inazingatia matakwa ya sheria ya usimamizi wa mazingira katika sekta hiyo yanatekelezwa ipasavyo ili kuwa na mazingira safi, afya bora kwa jamii na matumizi endelevu ya rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
NEMC kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam iliadhimisha siku hiyo muhimu katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Wananchi walipata fursa nzuri ya kushiriki katika maadhimisho hayo ili kupata taarifa, elimu na kutambua fursa zilizopo katika uwekezaji wa eneo taka za aina zote.
Wadau zaidi 100 kutoka taasisi za serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na makundi maalum walioshiriki maonesho hayo walionesha shughuli zao za kila siku ambazo zimelenga kutoa huduma za kukusanya/uzoaji wa taka, pamoja na kurejeleza.
Wadau hao walionesha wanavyotumia taka kama rasilimali katika kutengeneza bidhaa nyingine, kutoa ajira, kuongeza kipato, kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuweka mazingira safi.
Kupitia taka, wananchi wanaweza kupata fursa nyingi za kujipatia kipato. Mfano halisi ni taka ngumu kama chupa za mvinyo ambazo watu wamebuni na kuzigeuza kuwa mapambo ya ndani na pia kutumika kama vyombo vya nyumbani.
Taka zikitenganishwa kwa kuzingatia aina na makundi zitarahisisha uteketezaji na urejelezaji wa dhana ya punguza, tumia tena na rejeleza mazingira yetu, uhai wetu, tuyatunze yatutunze.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED