Haki, weledi wahitajika Ligi Kuu Bara ikielekea ukingoni

Nipashe
Published at 11:42 AM Apr 21 2025
Ligi  Kuu Bara.
Picha: Mtandao
Ligi Kuu Bara.

LIGI Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea tena leo kwa mabingwa watetezi, Yanga ya Dar es Salaam kushuka ugenini kuwakabili Fountain Gate FC kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa ulioko Babati, mkoani Manyara.

Yanga itashuka katika mchezo huo ikitoka kwenye michuano ya Kombe la FA huku Fountain yenyewe ilikuwa ikisubiri kukutana na vinara hao, lakini ikiwa na mwenendo wa kusuasua.

Ligi hiyo tayari imeshaanza kuelekea ukingoni kwa sababu baadhi ya timu zimebakia michezo mitatu au minne ili kumaliza msimu isipokuwa Simba ambayo inakabiliwa na majukumu wa kimataifa, kwa sasa imetinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hatua hii ya hatua ya lala salama ni muhimu kwa kila timu kwa sababu kila upande unahitaji kufikia malengo yake.

Kuna timu ambazo ziko katika vita ya kuwania ubingwa, hapa unaweza kuwaona vigogo (Simba na Yanga), kutokana na Azam kujiweka kando baada ya kupoteza michezo yake miwili ya hivi karibuni.

Hata hivyo Azam, Singida Black Stars na Tabora United, wao wapo kwenye hesabu za kumaliza katika nafasi nne za juu ili kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

Hii inatokana na Tanzania kutoa wawakilishi wanne kwenye michuano inayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), timu mbili zikienda kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa na nyingine katika michuano ya Kombe la Shirikisho.

Mpaka sasa kuna makundi matatu, kundi la kwanza ni zile ambazo zinaendelea kupambana kuwania taji na zinaonyesha wazi zina kiu kubwa ya kutwaa ubingwa kwa kila siku kujiimarisha na kujipanga kuvuna pointi tatu kwa sababu inaamini bado taji liko wazi.

Kundi lingine ni zile timu ambazo zimeshajidhihirisha zinahitaji pointi muhimu ili kujiweka mahali salama katika msimamo lakini pia zikihitaji kumaliza kwenye nafasi nne za juu na kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na CAF ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

Lakini pia kuna kundi ambao lenyewe malengo yake sasa ni kuvuna pointi na kujinusuru na janga la kushuka daraja kwa sababu kwao itakuwa ni miujiza zikibeba taji hilo, kutokana na kutokuwa na matokeo chanya katika mechi za mzunguko wa kwanza.

Hawa ndio hucheza kwa kukamia na wakati mwingine mechi zao hupoteza mvuto.

Katika soka lolote hutokea hasa pale michezo iliyobaki ni mingi, huu ni wakati wa viongozi, makocha na wachezaji kuongeza utulivu na hatimaye kusaka ushindi na kudhihirisha matokeo ya mzunguko wa kwanza yalitokana na 'kuteleza'.

Pia wachezaji kuonyesha kandanda safi sio tu kutaisaidia kupata matokeo chanya timu yao, ubora huo utawaongezea thamani wachezaji na kujiweka 'sokoni' kuelekea maandalizi ya msimu mpya.

Wachezaji kuonyesha nidhamu ndani na nje ya uwanja itawasaidia kuwaongezea mashabiki kujitokeza kwa wingi viwanjani kwa sababu wataamini wanakwenda kushuhudia vipaji na si vurugu au faulo ambazo hazistahili kutokea kwa wanamichezo.

Tunawakumbusha waamuzi wetu kuongeza umakini kwa sababu filimbi yao itachangia kupata matokeo ya haki na ambayo kila mmoja ataridhika nayo, tofauti na hapo lawama na malalamiko juu yao yataongezeka.

Huu ndio ule wakati ambao wachezaji, viongozi na mashabiki hawataki kusikia neno 'makosa ya kibinadamu' kwa sababu wanaamini mara nyingi huwafaidisha vigogo na zile timu changa kuumia.