Fainali CAF, umakini Simba unapaswa kuwa nje, ndani

Nipashe
Published at 11:39 AM May 12 2025
Fainali CAF, umakini Simba unapaswa kuwa nje, ndani
Picha: Mtandao
Fainali CAF, umakini Simba unapaswa kuwa nje, ndani

KIKOSI cha Simba kinatarajiwa kuondoka wakati wowote kuanzia kesho kuelekea nchini Morocco kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane.

Ni mechi iliyobeba matumaini si ya wanachama na mashabiki wa Simba tu, bali nchi kwa ujumla, kwani ushindi kwao ni sifa kwa Taifa zima la Tanzania ambalo kwa mara ya kwanza litakuwa linashuhudia timu ya nchi hii ikichukua moja kati ya makombe makubwa barani Afrika, yanayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika, CAF.

Kingine ambacho kimewapa matumaini makubwa wanachama na mashabiki wa Simba ni sapoti kubwa ya serikali, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo mbali na kutoa pesa kwa kila bao, lakini kwa mechi iliyopita na hii ametoa ndege, malazi, na huduma zingine muhimu zinazohitajika ili mradi tu kuhakikisha timu hiyo ya nchini kwake haipati matatizo na usumbufu usio wa lazima, ikiwamo kubadilisha ndege, wakati mwingine kwenda hadi Ulaya nchini Uturuki, halafu timu inarudi tena Afrika na kuifanya safari kuwa ndefu na kuleta uchovu kwa wachezaji.

Imani nyingine kwa mashabiki wa Simba ni serikali kuahidi kuwa mechi ya marudiano itachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao kwao ni zaidi ya uwanja kutokana na matokeo mazuri ambayo imekuwa ikiyapata uwanjani hapo kwenye michuano ya kimataifa.

Ndiyo maana Simba walikuwa na wasiwasi sana kwenye mchezo uliopita wa kwanza wa nusu fainali uliopigwa, New Amaan Complex, Zanzibar, na ushindi kiduchu wa bao 1-0, ulionekana kutokana na wachezaji wenyewe, wanachama na mashabiki kuathirika kisaikolojia.

Pamoja na imani kubwa hii, lakini tunatoa tahadhari kwa viongozi, wanachama, mashabiki na wachezaji wa Simba kuwa mechi dhidi ya RS Berkane haitokuwa rahisi kama wanavyodhani. Itakuwa ni zaidi ya mechi. Itakuwa ni vita ya ndani na nje ya uwanja. Hivyo, viongozi wa Simba wanatakiwa washinde kwanza vita ya nje ambayo inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko ya ndani. Pia kwa kuangalia tu unaweza kuona kama mechi ya ugenini itakayochezwa, Jumamosi wiki hii,  itakuwa ngumu kuliko ya nyumbani. 

Ukweli ni kwamba mechi ya ugenini kwa Simba itakuwa ngumu ndani ya uwanja tu, lakini si nje, ila ya marudiano, Mei 25, mwaka huu itakuwa ngumu zaidi nje ya uwanja, uongozi, wanachama na mashabiki wanapaswa kujiandaa na kuongeza umakini.

Tunasema hivyo kwa sababu siasa za mpira wa Tanzania zinaeleweka. Sidhani kama baadhi ya timu zitataka Simba itwae kombe hilo. Kutwaa kombe kunaweza kusababisha baadhi ya timu kuonekana kama hakuna ilichofanya msimu huu, hivyo kutaka kuingia katika vita ya kuzuia hilo lisitokee kwa Simba.

Tumesikia kuwa baadhi ya viongozi wa RS Berkane wapo nchini wakiifuatilia Simba kwenye michezo yake. Nadhani si michezo tu, hata na mambo mengine ikisaka mbinu na siri mbalimbali ambazo inaweza kuzitumia itakapokuja.

Tuliona Al Masry walipokuja nchini, hawakuingia kwenye mlango mkuu ambao hutumiwa na timu zote, badala yake wakaingia kwenye mlango mdogo, ambao kwa mastaajabu makubwa uliachwa wazi, sijui kwa amri ya nani na nani aliwataka wapite huko. Hii inaonesha kuwa baadhi ya timu ngeni zinapata siri hapa hapa nchi nini zifanye na hii ni kengele ya hatari kwa Simba.

Kwa maana hiyo tunadhani wakati Simba inakwenda kupambana na RS Berkane ugenini, ikumbuke pia kuwa makini na mchezo wa fainali ya marudiano ambao ndio utatoa matokeo ya nani atalibeba kombe hilo.

Viongozi wa Simba wanatakiwa kuwa waangalifu zaidi kuelekea kwenye mchezo huo wa Mei 25 bila kujali aina ya matokeo itakayopata ugenini.

Matokeo yatakayoonekana kuinufaisha Simba ugenini, ndiyo yatakayoifanya mechi ya marudiano kuwa ngumu zaidi kwani vita itakuwa kubwa nje ya uwanja.