Tunywe maziwa kujiepusha na magonjwa nyemelezi

Nipashe
Published at 10:17 AM Jun 03 2025
Tunywe maziwa kujiepusha na magonjwa nyemelezi
Picha: Mtandao
Tunywe maziwa kujiepusha na magonjwa nyemelezi

TANZANIA ni miongoni mwa nchi kumi Afrika zinazoongoza kwa uzalishaji maziwa, ikiongozwa na Ethiopia.

Nchi zingine kwenye orodha hiyo ni Sudan, Kenya, Misri, Afrika Kusini, Zimbabwe, Nigeria, Uganda, Madagascar na Tanzania ikishika namba kumi.

Idara ya Takwimu ya Taifa (NBS), imetoa data ya mifugo ikionesha kwamba Tanzania inakadiriwa kuwa na ng’ombe milioni 33.9, huku Ethiopia ikiongoza kwa kuwa na idadi ya milioni 60.39.

Hata hivyo, unywaji maziwa kwa Tanzania bado uko chini kulinganishwa na viwango vya kimataifa, ambavyo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) inapendekeza lita 200 kwa mwaka.

Kutozingatia unywaji wa maziwa kumesababisha watoto kutokua vizuri na kupata udumavu na vile vile kutofanya vizuri kwenye masomo.

Takwimu za WHO zinaonesha kuwa zaidi ya watu bilioni sita duniani hutumia maziwa na bidhaa zake. Hata hivyo, wengi wa watu hao wanaishi katika nchi zinazoendelea.

Sekta ya maziwa husindika maziwa mabichi kuwa safu ya bidhaa ikiwa ni pamoja na siagi, jibini, krimu, mtindi, samli, maziwa yaliyokaushwa na askrimu.

Maziwa yanaweza kutumiwa kwa njia mbali mbali, lakini hayatiliwi maanani pengine kwa watu kutojua umuhimu wake katika mwili wa binadamu.

Kwa utafiti wa macho tu, unaweza kugundua kuwa mikoa ambayo inaoongoza kwa ufugaji na bidhaa za wanyama hao kutumika ipasavyo, watu wake huwa na siha nzuri na hata mwonekano wao wa ngozi huwa nyororo na zenye kuvutia.

Kwa kabila la Maasai ambao husifika kwa kutumia bidhaa zitokanazo na ng’ombe, kuanzia nyama mpaka maziwa, mwonekano wa ngozi zao huwa ni wa kuvutia na hawanyemelewi na magonjwa.

Faida ya kunywa maziwa huimarisha mifupa, kuimarisha mifupa dhidi ya magonjwa kama vile udhaifu wa mifupa (osteoroporis). Maradhi haya huzuiliwa kwa kalsiamu ipatikanayo kwenye maziwa na ambayo hufunzwa kutokana na uwapo wa vitamin D.

Kwa hapa nchini jambo la ajabu unaloweza kugundua, licha ya baadhi ya mikoa kuwa na mifugo mingi, lakini hawatumii bidhaa zake kwa faida ya miili yao.

Baadhi ya mikoa hiyo ndio yenye watoto wenye udumavu kwa kukosa lishe bora na watoto wake hawafanyi vizuri kwenye masomo darasani.

Unywaji maziwa ni lazima utiliwe mkazo ili kujenga jamii yenye afya bora na kuepuka maradhi yanayosababishwa na ukosefu wa virutubisho vinavyochangiwa na bidhaa hiyo.

Ndio maana hata wataalamu wa afya wanashauri watoto wanapozaliwa wanyonyeshwe maziwa ya mama mpaka watakapofika miaka miwili ili kumjengea mtoto kinga thabiti dhidi ya maradhi.

Umuhimu wa maziwa unaonekana kuanzia ya binadamu mpaka kwenye wanyama. Na kwa umuhimu huo, hata mtoto anapokuwa hapati maziwa ya kutosha toka kwa mama, inashauriwa apewe maziwa ya ng’ombe.

Uzalishaji wa bidhaa ya maziwa kwa mujibu wa takwimu za sasa, umeongezeka kutoka lita bilioni 3.9 kwa mwaka 2023/24 hadi lita bilioni nne mwaka huu, sawa na ongezeko la asilimia moja, huku vituo vya kukusanyia maziwa viongezeka kutoka 258 hadi 269.

Jitihada kubwa zinafanyika kwenye kuongeza maeneo ya malisho, usindikaji na usambazaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Licha ya jitihada hizo cha muhimu ni kuendelea kueneza elimu ya watu kupendelea kunywa maziwa ili waweze kujiongezea virutubisho vya kuilinda miili yao dhidi ya magonjwa.