TAKWIMU kuhusu udumavu wa watoto na lishe duni katika baadhi ya mikoa inayozalisha vyakula hasa ya nyanda za juu kusini kutokana na ukosefu wa lishe bora zimekuwa zikishtusha na kutisha licha ya jitihada zinazochukuliwa na serikali kukabiliana na tatizo hilo.
Takwimu hizo zinanifanya nijiulize maswali mengi na kukosa majibu inakuwaje mikoa hiyo ambayo imebarikiwa kuwa na uzalishaji mkubwa wa mazao ya nafaka, matunda na mboga na kuwa tegemeo la kulisha sehemu kubwa ya Tanzania na hata nchi jirani inakabiliwa na tatizo hilo.
Maeneo hayo yanazalisha vyakula hivyo na matunda ambavyo yanaboresha lishe kwa watoto kuanzia wanapokuwa tumboni wakati wa ujauzito wa mama na hata watu wazima.
Kinachoelezwa na wataalamu mbalimbali wa lishe, wakiwamo viongozi wa serikali na mashirika ya ndani na nje yanapambana na tatizo hilo ni kuwa tatizo hilo linasababishwa na baadhi kujenga mazoea ya kutozingatia mpangilio wa nyakula vya aina mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha lishe bora na afya za watoto hadi watu wazima.
Katika Ukanda wa Nyanda za Juu kusini, mikoa ambayo inatajwa kukithiri kwa tatizo hilo ni Mbeya na Njombe ambayo ni miongoni mwa inayoongoza kitaifa kwa uzalishaji wa mazao ya biashara na vyakula.
Inaendelezwa kuwa katika mkoa wa Mbeya, jamii inaendeleza kula mlo wa aina moja wa wali mara tatu kwa siku kwa maana yake asubuhi, mchana na usiku ambao hauna virutubisho vya kujenga afya bora kwa watoto.
Takwimu zinaonesha kuwa licha ya mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini, tatizo la udumavu liko juu ya wastani wa kitaifa kutokana na mtindo mbovu wa baadhi ya wakazi wa kula walau ubwabwa mara tatu.
Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera anatoa takwimu hizo wakati wa uzinduzi wa Mradi wa ‘Lishe ya Mwanao’ kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo la udumavu.
Homera anasema pamoja na mkoa kufanikiwa kupunguza tatizo hilo kutoka asilimia 33.8 mwaka 2018 mpaka asilimia 31.5 mwaka 2020, bado upo juu ya wastani wa kitaifa.
Anasema bado kuna shida kwa wakazi hao kula ubwabwa asubuhi, mchana na jioni.
Jamani Wanambeya ni wakati wa kubadilika katika ulaji wa vyakula badala ya kuendelea kupuuza ushauri wa wataalamu wa lishe na kufanikisha mkakati wa mkoa uliojiwekea kupunguza tatizo hilo hadi kufikia asilimia 24 mwaka 2030.
Mikakati hiyo ni kutoa elimu kwa wazazi na walezi kuhusu namna bora ya uandaaji wa chakula cha watoto.
Halmashauri zote za mkoa huo kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kupunguza tatizo hilo ili kufikia malengo ya kuwa na taifa lenye watu wenye uwezo wa kufanya kazi vizuri kwa kuwa watakuwa na afya bora.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), linastahili pongezi kwa kufadhili mradi huo kwa kushirikiana na Serikali ya Norway kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.3 katika mikoa ya Mbeya na Njombe.
Mradi huo unatekelezwa katika halmashauri za Mbarali, Mbeya na Rungwe ambazo ni miongoni mwa zenye tatizo hilo la udumavu kwa watoto kwa kukosa lishe bora.
Ikumbukwe kuwa udumavu unaathiri ukuaji wa mwili na akili kwa watoto na kusababisha madhara ya muda mrefu ikiwamo tija ndogo kwenye uzalishaji wanapokuwa watu wazima.
Ikumbukwe na wazazi, walezi na wananchi wengine kuwa mikoa hiyo inalitia aibu taifa kwa kuwa dhamana ya kuhakikisha linakuwa na watu wenye afya bora, akili, ubunifu na uchapa kazi iko mikononi mwao, lakini wao wanachukulia kampeni dhidi ya vita hivyo vya udumavu ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED