Tuendelee kuenzi 'Mtu ni Afya' aliyoienzi Baba Taifa

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 02:49 PM Oct 16 2025
 Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
Picha: Mtandao
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

MWEZI huu wa Oktoba, ni wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwani ndio ambao alifariki dunia ambako kumbukumbu ya miaka 26 ya kifo chake ilifanyika juzi.

Baba wa Taifa alifariki dunia Oktoba 14 mwaka 1999 wakati akipatiwa matibabu katika hospitali moja jijini London na kuliacha taifa aliloliongoza kwa miaka 23 katika majonzi makubwa.

Ni miaka 26 imepita tangu afariki dunia, lakini hotuba zake ambazo amewahi kuzitoa, ambazo huwa zinarushwa kwenye runinga au redioni pamoja na misemo na maandiko yake bado vinaendelea kuishi. 

Ingawa kumbukumbu ya kifo chake ilifanyika Jumanne wiki hii, ni vyema kukumbushana kuwa kiongozi huyo alifanya mengi patika nchi hii kwa ajili ya Watanzania wote matajiri na maskini.

Kwa leo ninataka kuelezea sekta ya afya ambayo kimsingi ni ya muhimu, kwa sababu bila kuwa na afya bora, si rahisi kufanya kazi na si rahisi kuleta maendeleo binafsi na hata taifa kwa ujumla. 

Ukweli ni kwamba, serikali yake ilikuwa makini kwenye masuala ya afya hadi ikaamua kupaa na kaulimbiu mbalimbali ikiwamo ya 'Mtu ni Afya' na kuhamasisha wananchi kujikinga na adu maradhi. 

'Mtu ni Afya', ni kaulimbiu iliyolenga kutoa ujumbe maalum kwa jamii, kwamba bila ya kuwa na afya bora na mazingira bora, binadamu anaweza kuathirika na maradhi yote hatari.

Ninaamini kwamba wale ambao wakati huo walikuwa wameshajitambua watakuwa wanakumbuka jinsi kaulimbiu ya ‘Mtu ni Afya’ ilivyokuwa ikisikika redioni na kutangazwa pia magazetini.

Vilevile, hata wasanii na wananamuziki wa bendi za muziki wa dansi na sabna nyinginezo, pia vikundi mbalimbali walitungia nyimbo kaulimbiu hiyo ili kusaidiana na serikali, katika kuhamasisha umuhimu wa kila Mtanzania kuwa na afya bora. 

Wale waliokuwapo wakati huo na sasa bado wapo, watakubalina nami kwamba Mwalimu Nyerere alihimiza umuhimu wa afya bora inayotokana na lishe bora, kwani wakati huo kulikuwa pia na nyimbo za kuhamasisha lishe hiyo na hata kujenga nzuri lakini pia pa kulala pawe bora. 

Tunapoadhimisha miaka 26 ya kifo chake, ni vyema tukumbushane machache aliofanya kwenye afya wakati wa uongozi wake, hasa kwa kuzingatia kwamba alikuwa anamchukia adui maradhi. 

Mara tu baada ya Tanganyika kupata uhuru, Mwalimu Nyerere alitangaza vita dhidi ya maadui watatu ambao ujinga, umasikini na maradhi, ambao alipambana nao kwa nguvu zake zote. 

Mojawapo ya njia alizotumia kupambana na adui maradhi, ni kuwapa elimu Watanzania ili waweze kutambua mbinu mbalimbali za kujikinga au kutibu maradhi kwa kwenda hospitali kupata huduma za afya. 

Habari njema ni kwamba, hata baada ya yeye kung'atuka, awamu zilizofuata, zinaendeleza yale ambayo alianzisha ikiwamo mkakati unaoendelea sasa wa kujenga zahati kila kijiji, vituo vya afya kila kata.

Mkakati huo unakwenda sambamba na ujenzi wa hospitali za wilaya, hospitali za mikoa na za rufani, ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kutimiza kaulimbiu kwa ajili ya 'Mtu ni Afya'.

Hayo hayaishii hapo tu bali bali pia kuna matangazo mbalimbali yanayohusu afya au kujikinga na maradhi yakiwamo ya mlipuko kama kipundupindu, kuhara na mengine, huwa yanaandikwa kwenye magazeti. 

Matangazo hayo pia huwa yanasikika redioni, katika runinga na mitandao ya kijamii, kufikisha ujumbe kwa Watanzania ili wawe tayari linapotokea tatizo, wajue jinsi ya kuchukua tahadhari.