KATIKA karne hii ya sayansi, teknolojia na ubunifu, bado kuna maeneo nchini ambako imani za kishirikina zimeendelea kuwa miongoni mwa vikwazo vikubwa vya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Tukio lililobainika hivi karibuni katika Wilaya ya Wanging’ombe, mkoani Njombe, ni kielelezo cha wazi kuwa ujinga na hofu ya kuhusishwa na uchawi bado vimekita mizizi katika baadhi ya jamii zetu.
Imeelezwa kuwa wakazi wengi wa maeneo hayo wanashindwa kujenga nyumba bora, kuanzisha biashara au hata kuwasomesha watoto wao katika shule nzuri kwa hofu ya “kurogwa” au “kuuliwa kwa wivu wa mafanikio”.
Hali hii si tu ya kusikitisha, bali pia ni aibu kwa taifa linalojitahidi kupiga hatua za kimaendeleo kwa kasi.
Tunapaswa kujiuliza, ni kwa nini katika ulimwengu unaoelekea kutua kwenye sayari ya Mars, bado baadhi ya Watanzania wanahusisha mafanikio ya jirani yao na uchawi?
Ni kwa nini jamii inayoishi katika nchi yenye amani, uhuru wa kuabudu na elimu ya bure, bado inaishi kwa woga wa nguvu zisizoonekana?
Kwa hakika, imani hizi potofu zimegeuka kuwa mzigo mzito wa kisaikolojia unaozuia wananchi kufikiri kwa uhalisia.
Watu wanashindwa kufanya kazi kwa bidii au kutafuta mafanikio kwa hofu ya kuonekana “wamepewa na mizimu.” Wengine wanalazimika kuficha mafanikio yao, kuishi maisha ya kawaida, au hata kuhamia maeneo mengine kwa woga wa kuhusishwa na uchawi.
Tunaona kuwa ni wajibu wa viongozi wa dini, serikali na taasisi za elimu kushirikiana kwa karibu katika kampeni ya kitaifa ya kupinga imani za kishirikina.
Kama alivyosema mmoja wa waumini wa Kanisa la KKKT katika harambee ya ujenzi wa kanisa Kijiji cha Ihadzutwa, “Watu wanaogopa kuanzisha shughuli za maendeleo kwa hofu ya kurogwa.” Kauli hii inaakisi ukweli mchungu unaokabili jamii nyingi vijijini.
Nipashe tunawapongeza viongozi wa dini kama Makarisi Kabelege na Oraph Mhema, waliohimiza jamii kuongozwa na neno la Mungu na kuachana na fikra za kishetani zinazowagawa watu.
Ni ukweli usiopingika kwamba dini, zikiwa zikitumika ipasavyo, ni silaha madhubuti ya kubomoa ngome za giza na hofu.
Nipashe tunasisitiza kuwa mapambano haya hayawezi kuachiwa viongozi wa dini pekee. Serikali inapaswa kuongeza juhudi za elimu kwa umma, hasa kupitia vyombo vya habari na mitaala ya shule za msingi na sekondari.
Elimu kuhusu sayansi, tiba na uzalishaji lazima itolewe kwa lugha rahisi inayoweza kueleweka na kila mwananchi, ili kupunguza utegemezi wa imani zisizo na msingi.
Vyombo vya usalama navyo havipaswi kukaa kimya. Matukio ya mauaji ya wazee au watu wanaodaiwa ni wachawi bado yanaripotiwa mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini.
Ni wajibu wa Jeshi la Polisi na mahakama kuhakikisha wanaohusishwa na vitendo vya kishirikina wanachukuliwa hatua kali ili kuwa fundisho kwa wengine.
Ni ukweli ulio wazi kwamba imani za kishirikina si tatizo la Njombe pekee. Zimeenea katika sehemu mbalimbali za Tanzania, zikichangia kwa kiwango kikubwa kurudisha nyuma juhudi za maendeleo, kuharibu umoja wa kijamii na kueneza hofu isiyo na msingi.
Tunapendekeza kuwa serikali za mitaa ziwe mstari wa mbele katika kuhimiza mijadala ya kijamii kuhusu maendeleo na maarifa, badala ya kuacha nafasi kwa waganga wa kienyeji na manabii wa uongo kushika hatamu.
Jamii ikielimishwa vizuri, itatambua kwamba mafanikio ni matokeo ya juhudi, nidhamu, maarifa na mipango bora. Si matokeo ya uchawi.
Kwa upande mwingine, ni lazima tutambue kwamba kuendelea kuamini katika ushirikina ni sawa na kujifunga minyororo ya umasikini kwa mikono yetu wenyewe.
Taifa haliwezi kusonga mbele ikiwa sehemu ya wananchi wake bado inashindwa kutofautisha kati ya maendeleo ya kweli na imani za kishirikina.
Tanzania inahitaji watu wanaothubutu na wanaoamini katika kazi, elimu na ubunifu. Tukiendelea kushikilia imani hizi potofu, hatutafika kokote.
Kwa hiyo, ni wakati sasa wa kila mmoja wetu kusimama na kusema hapana kwa imani za kishirikina. Tujikomboe kifikra, tuelekeze nguvu zetu kwenye elimu, kazi na ujasiriamali.
Hapo ndipo tutaweza kujenga taifa lenye maendeleo ya kweli. Taifa lisilojawa na hofu, bali matumaini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED