TFF iwe makini na waamuzi Championship

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 03:48 PM Oct 13 2025
Omari Mdoe
Picha: Mtandao
Omari Mdoe

HIVI karibuni Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), katika kikao chake cha Oktoba 2, mwaka huu, kilitoa maamuzi kadhaa baada ya kupitia matukio ya mbalimbali ya ligi ya kufanya maamuzi.

Mbali na kutoa adhabu kwa klabu, wachezaji, viongozi  na mambo mengine yanayofanana hayo, ilitoa adhabu pia kwa waamuzi kwa kushindwa kusimamia vyema sheria na kanuni za mpira wa miguu.

Mwamuzi Omari Mdoe kutoka Tanga, alifungiwa kwa kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa michezo mitano kwa kosa la kushindwa kuchukua hatua kutokana na vitendo vya ukiukwaji wa sheria za mpira.

Pamoja na matukio mengine, alishindwa kutafsiri sheria katika dakika ya 46, ambapo mchezaji wa Mbeya City, Mateo Antony, aliposhika mpira ndani ya eneo la hatari, lakini hakuchukua hatua yoyote.

Pia, mwamuzi huyo alishindwa kuchukua hatua baada ya mchezaji, Ibrahim Hamad 'Bacca', kumchezea rafu mbaya, Ibrahim Ame wa Mbeya City.

Naye, mwamuzi wa kati, Jackson Samuel wa Arusha, pia ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano kwa kushindwa kutafsiri vyema sheria na kuchukua hatua wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya JKT Tanzania na Azam FC.

Binafsi nilivutiwa na vitu viwili hapo. Kwanza kamati kuwawajibisha wale wote waliofanya makosa. Pili nilichofurahi zaidi ni uharaka wa kufanya maamuzi. Huko nyuma adhabu zilitoka hata baada ya randi tano, lakini safari hii, raundi tatu tu, kamati imetoa adhabu, pia zikiwa kubwa zaidi kuliko za msimu uliopita kwa mujibu wa kanuni.

Huku ni kwenye Ligi Kuu, sasa kinachotakiwa ni kamati kumulika Ligi ya Champioship ambayo nayo imenza wiki iliyopita.

Ni ligi inayopandisha timu daraja kwenda Ligi Kuu. Mashabiki wa soka wanahitaji timu inayokwenda huko iwe ni ile iliyopambana kihalali iki ikatoe ushindani na si kupanda kwa upendeleo na mizengwe.

Timu zinazopanda kwa upendeleo, rushwa na mizengwe hushindwa kufanya chochote zinapofika Ligi Kuu, badala yake zinashuka daraja na kurudi zilikotoka. Kwa sababu hazileti ushindani huko.

Wakati tunaipongeza kamati, tunaiomba pia imulike Ligi cha Champioship, ambayo inadaiwa kuwa ina mambo mengi yasiyo ya kiuadilifu kutokana na mechi nyingi kutoonyeshwa laivu.

Huko baadhi ya waamuzi huchezesha wanavyotaka kwa sababu hawaangaliwi kwenye televisheni, pia si mashabiki wengi wanaoifutilia.

Hata wachembuzi wengi macho yao hawapo huko, badala yake wao huzitazama timu mbili tu za Simba na Yanga kwenye Ligi Kuu.

Sababu hii huwafanya wamuzi huko wafanye wanavyotaka. Klabu nazo zinafanya zinavyotaka kuhakikisha timu zao zinapanda Ligi Kuu hata kama hazina uwezo.

Ni wajibu wa Kamati kuwa makini sana kwenye Ligi ya Champioship kuliko hata Ligi Kuu, kwani huko hata baadhi ya viongozi, mashabiki huweza kufanya chochote cha ajabu, kwa sababu tu huwa hawaonekani.