Yanga isikate tamaa, bado ina nafasi

Nipashe
Published at 02:31 PM Oct 20 2025
Uwanja wa Bingu Mutharika
Picha: Mtandao
Uwanja wa Bingu Mutharika

WIKI hii tumeshuhudia michezo mbalimbali ya kimataifa kwa ngazi ya Klabu ambapo hapa nchini timu zetu kubwa za Yanga na Simba nazo zilikuwa uwanjani.

Yanga ilikuwa ya kwanza kucheza Jumamosi kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Stirikers ya Malawi, uliopigwa Uwanja wa Bingu Mutharika, Malawi na ikapoteza kwa bao 1-0.

Kipigo hicho kikawalazimu Yanga kumtimua kocha wake mkuu, Romain Folz.

Watani zao, Simba wenyewe walicheza jana Jumapili dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini.

Wao Simba walipata matokeo mazuri kwa ushindi wa mabao 3-0 ugenini na hivyo kujiweka kwenye nafasi nzuri katika mchezo wa marudiano.

Simba sasa itakuwa na kazi ndogo kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa Ijumaa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Ni Yanga ambayo haikupata matokeo mazuri kwenye uwanja wake wa ugenini baada ya kipigo hicho.

Matokeo hayo yameibua hisia tofauti miongoni mwa mashabiki wa Yanga ambao wanaona timu yao haifanyi vizuri na imeanza vibaya kwenye michuano hiyo.

Wengi wao wanaona timu haijacheza vizuri na wapo wanaoona kuondoka kocha wao hakuwa na uwezo.

Maumivu hayo yamekuja pia baada ya Yanga kutoka sare mchezo mmoja wa Ligi kuu Tanzania Bara na sasa mashabiki wameanza kuikatia tamaa timu yao.

Lakini kiuhalisia na kwa maana halisi ya mpira wa miguu, ni mapema sana kwa mashabiki na wapenzi wa Yanga kuanza kuikatia tamaa timu hiyo.

Kupoteza alama tatu kwenye mchezo wa kwanza bado sio kigezo cha timu hiyo kufanya vibaya kwenye hatua hiyo kwa sababu bado ina mchezo wa nyumbani.

Kikubwa kwa sasa Yanga wanapaswa kutuliza akili na kujipanga upya kuelekea kwenye mchezo wao wa pili ambao watacheza nyumbani.

Wachezaji na benchi la ufundi wanapaswa kufahamu michezo inayofuata ndio muhimu zaidi kwao.

Matokeo ya mchezo uliopita yaishie kule Malawi na sasa ni kipindi cha kufanya maandalizi na kujipanga vizuri kabla ya mchezo unaofuata ambao utachezwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Matokeo mazuri watakayoyapata kwenye mchezo huo yatainua molari kwa wachezaji na kuanza kurudisha imani ya mashabiki wao katika kuikimbialia hatua ya makundi.

Mashabiki hawapaswi kukata tamaa na kuingiwa unyonge baada ya mchezo huo mmoja, bado kuna michezo mingine mbele ambayo kama Yanga watachanga karata zao vizuri wananafasi kubwa.

Nipashe tunaamini Yanga bado ipo kwenye nafasi ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa marudiano.

Kikubwa ni kujipanga na kujiandaa kikamirifu kuelekea kwenye mchezo wao wa Jumamosi ijayo, kwani hakuna kisichowezekana kwenye mpira, Yanga inaweza kupata ushindi ugenini na kushangaza wengi.

Hasa ikizingatiwa na ukweli kwamba, wachezaji wake muhimu walikuwa majeruhi, tunaamini kwamba, katika mchezo wa marudiano wanaweza kuwa fiti kucheza.

Hivyo tunawatakia kila la heri na tunaamini kwamba, watajipanga vizuri zaidi kwa ajili ya mchezo huo na hatimaye kufuzu hatua ya makundi.