Ikiwa zimebaki siku mbili kutamatika mwaka 2025, matukio ya utekaji ni mojawapo ya mambo yaliyoutikisa mwaka huu, huku matarajio ya wengi yakiwa ni kuona matukio hayo yakikomeshwa ili wananchi waishi kwa amani na furaha.
Katika mwaka 2025 wapo watu kadhaa maarufu waliotekwa wengine kupotea kabisa huku wengine wakipatikana wakiwa wameuawa. Matukio ya kutekwa kwa watu kama Humphrey Polepole, Mdude Nyagali, Mzee Ali Kibao ni mojawapo ya matukio yaliyotikisa mwaka huu na kuacha maswali mengi kwa wananchi, ndugu, jamaa na marafiki wa watu hao.
Mpaka sasa hakuna taarifa kuhusu wahusika wa matukio hayo kukamatwa hivyo kuacha sintofahamu katika jamii kuhusu uwezekano wa kuendelea kujirudia kwa matukio hayo. Bahati mbaya hata ndugu wa watu hao walipozunguka katika vituo mbalimbali vya polisi kuwatafuta ndugu zao hawakufanikiwa kuwapata.
Kutokana na mabadiliko yaliyoahidiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene katika utendaji wa jeshi la polisi nchini ni matumaini ya wananchi kwamba matukio ya utekaji yaliyojitokeza mwaka 2025 hayatajirudia 2026.
Katika mojawapo ya matukio yaliyotikisa ni kutekwa kwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendelo (CHADEMA) Mdude Nyagali na watu wasiojulikana usiku wa Mei 2 mwaka huu akiwa nyumbani kwake mkoani Mbeya.
Kwa mujibu wa mkewe, Sije Mbugi aliyesimulia tukio hilo na kunukuliwa na vyombo vya habari, anasema wakiwa nyumbani kwao Mtaa wa Iwambi, Jijini Mbeya walisikia sauti za watu wakijaribu kufungua geti, yeye akiwa wa kwanza kusikia alimuamsha na mumewe baada ya muda mfupi walifanikiwa kuvunja geti kisha mlango wa chumba walicholala na kuingia ndani.
Yeye na mumewe anaeleza walijitahidi kupambana lakini walizidiwa nguvu na watu hao ambao walifanikiwa kumchukua Mdude na kuondoka nae kusikojulikana na hadi leo haijulikani alipo. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya wakati huo Juma Homera alitoa dau la Sh milioni 5 kwa atakayewezesha kupatikana Mdude lakini hadi sasa hakuna aliyefanikiwa kumuona au kutoa taarifa za mahali alipo.
Hali ikiwa hivyo kwa Mdude Nyagali, aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole yeye inadaiwa alivamiwa na watu wasiojulikana usiku wa Oktoba 6 mwaka huu. Picha zilizosambaa mitandaoni zilionesha nyumba yake ikiwa imevunjwa milango huku michirizi ya damu ikionekana sakafuni kuonesha huenda palikuwapo na mapambano ya kujitetea dhidi ya watekaji na hivyo huenda alijeruhiwa na watu hao wakati wa mapambano baina yao.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro aliahidi kulifuatilia suala hilo ili kubaini waliohusika na tukio hilo lakini hadi mwaka unakaribia kuisha hakuna yeyote aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED