Walezi wenzangu, tuamke kipindi hiki ‘madogo’ wanamaliza mitihani

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 03:36 PM Oct 23 2025
Wanafunzi
Picha: Mtandao
Wanafunzi

SASA ni kipindi ambacho wanafunzi wamemaliza elimu ya msingi na wapo majumbani wakisubiri kujiunga na elimu zaidi kwa awamu ijayo.

Kama ilivyo utashi wa umri wao, wamechangamka kupita kiasi, kila kona wanakopatikana, maana ratiba ya asubuhi shule na jioni mikononi mwa wazazi imekuwa ikiwadhibiti.

Wazazi nao katika saikolijia hiyo kujua namna vijana wao walivyohaha na ratiba ya masomo, sasa wanaachiwa kupumua wakijsikia kama wanadamu katika nafasi yao, kabla ya kujiunga na awamu ya pilika za pili.

Ni kipindi mtu anakuta baadhi ya wazazi huwasafirisha watoto kwa ndugu na jamaa na wazazi wengine wanawaingiza watoto hao katika vituo vinavyotoa elimu ya kiingereza na misingi mingine ya kujiunga na elimu ya sekondari.

Kila mzazi na mipango au uamuzi wake kulingana na mitazamo yao ya ulezi nyumbani kuhusu mtoto huyo. 

Ndipo kunashuhudiwa uamuzi wa wazazi fulani, wanaowapeleka  watoto hao kwa ajili ya maandalizi ya elimu ya awali ya sekondari.

Na kwa wale ambao shule walizosoma zimewafundisha ujuzi wa ujasiriamali, likizo hiyo inakuwa sehemu ya kujiongezea kipato, pia wakati huo huo ni mafunzo kwa vitendo.

Kielelezo chake kimojawapo ni pale, mtu akiwa katika maeneo yenye msongamano wa watu, anakuta watoto wadogo nao wanatembea, mikononi wana karanga au pili wazazouza na hata ukiwauliza, unajibiwa biashara za wazazi wao.

Kuna kundi linajichanganya, kuwapo watoto katika sehemu zenye hatari, nao kunadi hivyo wanavyoviuza, iwe karanga au sigara.

Ni mustkabali huo hunianzishia  maswali, kulikoni mzazi anashindwaje kubuni biashara ya kuendesha binafsi, hata anabaki kumsogezea mtoto huyo wake amfamyie kazi hiyo? Ni kitendawil kwa jamii yote!

Huo muda ambao mtoto anauza bidhaa zako, ilitakiwa awe anacheza na wenzake na sio wewe mzazi kukaa nyumbani.

Kwao watoto wana haki kama watoto wenzao wengine, kokote waliko. Na tukitafakari vipindi hivi vya kumaliza shule, wazazi mnatakiwa kuwaendeleza watoto kitaaluma.

Hiyo inajumuisha walau kwa wale wasiojua lugha kama Kiingereza, wajue na wale ambao wanaingia kidato cha kwanza waingie kujisomea ili wakiingia shuleni kwa ajili ya kujiunga na kidato cha kwanza wawe wanajua walau lugha.

Lakini, baadhi ya maeneo yenye mikusanyiko, unaona watoto wadogo wanatembaza vitu na ukiwauliza majibu yao ni mepesi tu wanakwambia biashara ya mama wengine watakwambia biashara ya bibi.

Kuna kundi lingine la wahitimu wa kidato cha nne na wale ambao wanamaliza mitihani ya kidato cha pili.

Makundi hayo, pia wazazi muwawezeshe watoto hao na sio kuwaacha na kujiingiza katika makundi yasiyofaa.

Kwa wale wa kidato cha nne ambao wanamaliza, kama walijifunza ujasiliamali ni mahali pake kwa hatua fulani 

Wanaweza kujiajiri wenyewe huku wakiwa wanasubiri matokeo yao ya mtihani waliofanya.

Kuna eneo jingine la ‘mchawi’ mitandao, ambayo iko katika kupigiwa kelele za kupitiliza.

Inaweza kuwa simu na televisheni au kompyuta za wazazi. Kote ikivamiwa ovyo, ni kufunguliwa mlango madhara ya kitabia kwa kundi hilo, na anaweza kunogewa na baadhi ya yasiyofaa (hasa kwa umri wake) ikawa sumu nzito kuiengua kutoka hisia hizo tajwa.

Sasa niseme hilio liwe ama kwa jirani, hata ndani ya familia na hata ukaribu wa mtaani kwako. Ni nadharia njema ya sote kuungana kukabili hali ya namna hiyo, tutakuwa tunakaribisha magumu yatayotushinda na waathirika ni zaidi ya ndani ya familia.