JANA taifa liliadhimisha kumbukumbu ya miaka 26 tangu kuondoka kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kiongozi ambaye si tu alijenga misingi ya taifa huru, bali pia alijenga dhamira ya maadili ya uongozi.
Pengine hakuna somo kubwa zaidi alilotupa Mwalimu kuliko lile la kupambana na rushwa, adui ambaye hadi leo bado analiandama taifa.
Katika misingi ya falsafa yake ya uongozi, Mwalimu Nyerere alisisitiza mara kwa mara kuwa rushwa ni ugonjwa unaoliua taifa taratibu.
Aliiona rushwa kama “adui wa nne” baada ya ujinga, maradhi na umaskini. Kauli yake kwamba “rushwa ni adui mkubwa zaidi kwa ustawi wa watu wakati wa amani kuliko hata vita" inabaki kuwa onyo lisilozeeka.
Wakati vita hubomoa majengo, rushwa hubomoa misingi ya haki na utu, mambo ambayo hayawezi kujengwa upya kwa zege wala chuma.
Katika hotuba zake nyingi, Mwalimu Nyerere alionya juu ya madhara ya rushwa katika mfumo wa utawala na siasa. Alisema: "Uongozi si biashara, ni utumishi. Mtu anayenunua kura ili achaguliwe hawezi kuwatumikia watu, atawatawala kwa kulipiza gharama za kura alizonunua."
Kauli hii inaakisi kile kinachoendelea leo katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, ambapo taarifa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) zimeonesha kuwapo vitendo vya rushwa hasa kwenye kura za maoni ndani ya vyama.
Ni ukweli mchungu kwamba, zaidi ya robo karne baada ya kifo cha Mwalimu, wosia wake haujatekelezwa kwa ukamilifu. Rushwa imevaa sura mpya; imeingia katika siasa, zabuni, ajira na hata huduma za jamii.
Wakati mwingine, imepambwa kwa jina la "fadhila", "chai" au "motisha". Hali hii inadhihirisha jinsi maadili ya uongozi na uzalendo vilivyoanza kuyumba, jambo ambalo Mwalimu aliwahi kuliona mapema na kulikemea kwa ukali.
Katika hotuba yake ya Machi 15, 1984 kwa majaji, Mwalimu Nyerere alitoa kauli nzito: "Huwezi kununua haki. Haki hainunuliwi. Rushwa yetu siku hizi haina aibu." Leo, maneno haya yanaonekana kama unabii.
Wapo wanaotumia nafasi zao kuamua hatima za watu kwa mizani ya bahasha badala ya mizani ya haki. Wapo wanaogeuza kura kuwa biashara na uongozi kuwa soko. Huu ni msalaba mzito kwa taifa lililojengwa kwa misingi ya uadilifu na heshima.
Mwalimu Nyerere hakusema tu. Alitenda. Alijenga mifumo ya kudhibiti rushwa, alihimiza viongozi kuishi kwa kipato halali na alisisitiza nidhamu ya maadili kwa viongozi wa umma.
Aliamini kuwa kiongozi wa kweli ni yule anayechaguliwa kwa sifa, si kwa hongo. Ndiyo maana alitoa onyo kwa wananchi: "Ukimwuzia mtu kura yako, umempa haki ya kukutawala kama mtumwa."
Hii leo, onyo hilo linapaswa kuwa mwongozo kwa Watanzania wote wanaoingia katika msimu wa uchaguzi. Huu si wakati wa kuuza kura; ni wakati wa kuamua hatima ya taifa.
Rushwa katika uchaguzi ni sawa na kujinyima haki ya kupata viongozi bora. Ni sawa na kupiga kura dhidi ya mustakabali wa watoto wetu.
Taasisi kama TAKUKURU zimeonesha nia ya kupambana na tatizo hili, kama alivyoeleza Mkurugenzi wake Mkuu, Crispin Chalamila, kuwa wamepokea taarifa nyingi za vitendo vya rushwa na wamechukua hatua za kisheria.
Hata hivyo, mapambano haya hayawezi kufanikiwa bila uungwaji mkono wa wananchi. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema: "Serikali haiwezi kupigana na rushwa peke yake; wananchi wakikubali rushwa, basi serikali itashindwa."
Kwa hiyo, kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mwaka huu inapaswa kuwa zaidi ya tukio la kihistoria. Ni mwito wa kuzinduka. Ni wito wa kujitafakari kama taifa. Je, bado tunafuata maadili yake? Je, viongozi wetu na wapigakura wetu wanaishi falsafa yake ya uadilifu?
Rushwa ni kama saratani. Ikiachwa kidogo leo, kesho itameza mwili mzima wa taifa. Hivyo, kila Mtanzania anapaswa kuwa sehemu ya tiba, si sehemu ya ugonjwa.
Wosia wa Nyerere bado unakumbusha kwamba maendeleo ya kweli hayawezi kujengwa juu ya msingi wa rushwa, bali juu ya maadili, uwajibikaji na haki. Miaka 26 baada ya kifo chake, Mwalimu bado anaishi kupitia maneno yake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED