MIAKA 26 imetimia tangu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere afariki dunia Oktoba 14 mwaka 1999 nchini Uingereza ikiwa ni miaka 14 tangu ang'atuke.
Kumbukumbu ya kifo chake ilifanyika jana ikiambata na shughuli za kuzima Mwenge wa Uhuru ambao uliitimisha mbio zake kwa mwaka huu wa 2025 jijini Mbeya.
Wakati huu wa kumbukizi ya kifo chake, ni kukumbuka mambo kadhaa ambayo busara yake ilitumika kuyaweka sawa ili kusaidia taifa kuendana na mazingira ya sasa hasa uwapo wa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Ilikuwa ni mwanzoni mwaka 1991, aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi alipounda tume iliyoongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania wakati huo, Francis Nyalali (marehemu)
Tume hiyo ilikuwa maarufu kwa jina la 'Tume ya Nyalali', iliyotumwa kukusanya maoni ya wananchi ili kutaka kujua kama wanataka nchi iendelee na mfumo wa chama kimoja au vingi.
Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na vuguvugu la mageuzi ya kisiasa katika mataifa mbalimbali, lililosababisha baadhi ya wadau wa mabadiliko ya kisiasa kutaka Tanzania iwe na mfumo wa vyama vingi.
Baada ya tume hiyo kuzunguka nchi nzima, ilikuja na maoni ya wananchi yakionyesha kuwa asilimi 80 ya Watanzania walitaka nchi iendelee kuwa ya mfumo wa chama kimoja huku asilimia 20 wakitaka vyama vingi.
Hapo ndipo karata ya Baba wa Taifa ilifanya kazi na kusababisha wale wenye asilimia 20 kuwa washindi, hivyo nchi ikarejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa ambao unaendelea nao hadi sasa.
Ilikuwa ni Februari mwaka 1992 kwenye Mkutano Mkuu wa CCM jijini Dar es Salaam, baada ya Tume ya Nyalali kuwasilisha ripoti ya maoni ya wananchi ikionyesha wengi wakitaka nchi iendelee kuwa ya chama kimoja, ndipo Baba wa Taifa anapotoa maoni yake.
Katika maoni hayo, alisema CCM si chombo kinachozama, ambacho baadhi ya waliomo wanataka kukiacha wasizame nacho, bali ni chama chenye nguvu na ndivyo Tume ya Nyalali ilivyoonyesha kutokana na asilimia 80 ya wananchi kutaka mfumo wa chama kimoja.
Katika kujenga hoja, akabainisha kuwa anapenda mageuzi yafanyike wakati huo, kwa maelezo kwamba mageuzi makubwa yanahitaji kiongozi mwenye uwezo na anayeaminiwa Watanzania.
Akamtaja kiongozi huyo mwenye uwezo na anayeaminiwa na Watanzania kuwa ni CCM, na kwamba chama hicho kina uwezo wa kusimamia mageuzi kwa kuwa kinaaminiwa na wananchi.
Hivyo, akashauri mfumo wa vyama vingi urejeshwe, kwa kuwa mwenye kuusimamia yupo ambaye ni chama tawala. Ushauri huo ulikubaliwa na wajumbe wa mkutano huo wa CCM ndipo vyama vingi vikarejeshwa.
Hotuba yake kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, ni miongoni mwa hotuba zilizopata umaarufu, kutokana na ukweli kwamba iliowageuza wana CCM na kuruhusu kurejeshwa mfumo wa vyama vingi ingawa kwa mujibu wa Tume ya Nyalali, Watanzania wengi walikuwa hawautaki.
Turufu yake hiyo ndio ulikuwa mwanzo wa kuwapo kwa utitiri wa vyama vya siasa ambavyo vilianzishwa na baadhi ya watu waliokuwa na kiu ya mageuzi, huku NCCR-Mageuzi kikiwa chama kikuu cha upinzani.
Chama hicho ambacho kwa sasa hakina nguvu kama ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu wa kwanza ndani ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, kilifanikiwa kupata wabunge na madiwani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED