MATUMIZI holela ya dawa ya uzazi wa mpango ya dharura aina ya P2 yamekuwa yakiongezeka kwa kasi miongoni mwa wanawake na wasichana, hasa vijana. Hal hii imezua taharuki katika jamii na kuibua tahadhari kutoka kwa wataalam wa afya.
Kauli ya hivi karibuni kutoka kwa Dk. Wanu Bakari Khamis, Mratibu wa Masuala ya Uhamasishaji na Mabadiliko ya Tabia kutoka Kitengo Shirikishi cha Afya ya Uzazi na Mtoto Zanzibar, inatoa ujumbe mzito na wa muhimu kuhusu tatizo hili.
Kwa mujibu wa Dk. Wanu, dawa ya P2 imekusudiwa kwa matumizi ya dharura pekee, kama vile kwa wanawake waliobakwa au waliojikuta katika mazingira ambayo ulinzi dhidi ya mimba haukuwapo isivyo bahati.
Dawa hii haikupangwa kuwa kinga ya kawaida ya uzazi wa mpango, bali tiba ya dharura inayotakiwa kutumika mara moja ndani ya saa 72 baada ya tendo la ndoa.
Hata hivyo, baadhi ya wasichana na wanawake wamegeuza dawa hiyo kuwa ngao ya kila siku dhidi ya mimba, wakidhani ni njia rahisi na salama, bila kujua madhara yake makubwa kiafya.
Takwimu zisizo rasmi kutoka vituo vya afya zinabainisha kuwa idadi ya vijana wanaotumia dawa za P2 mara kwa mara imeongezeka. Wengine huzitumia hata zaidi ya mara moja kwa mwezi.
Hii ni hatari kubwa kwa sababu dawa hiyo ina kiwango kikubwa cha vichocheo (hormones) vinavyoweza kuvuruga mfumo wa homoni za uzazi na kusababisha madhara makubwa kama vile kutopata hedhi kwa muda mrefu, kuharibika kwa mayai ya uzazi na hata kukosa uwezo wa kuzaa baadaye (utasa).
Nipashe tunaona kuwa tatizo la matumizi mabaya ya P2 si tu la kiafya bali pia ni kielelezo cha pengo kubwa la elimu ya afya ya uzazi katika jamii yetu.
Wengi wa wanaotumia dawa hizi mara kwa mara hawana uelewa wa kutosha kuhusu mwili wao, mzunguko wa hedhi, na njia sahihi za uzazi wa mpango.
Ni ukweli mchungu kwamba mijini, baadhi ya maduka ya dawa hutoa vidonge hivi kwa urahisi bila ushauri wa daktari, huku vijijini wasichana wengi wakibaki gizani kuhusu afya ya uzazi na hatari za uamuzi wao.
Ni wajibu wa kila mdau katika sekta ya afya na elimu kuchukua hatua. Serikali, kupitia Wizara ya Afya, inapaswa kuimarisha kampeni za kitaifa za elimu ya afya ya uzazi, hasa kwa vijana wa shule za sekondari na vyuo.
Programu za Huduma Rafiki kwa Vijana ziongezwe na kupewa nguvu zaidi, zikitumika kama vyanzo vya elimu, ushauri na msaada wa kisaikolojia kwa vijana wanaokabiliwa na changamoto za ngono za mapema.
Vilevile, wazazi na walezi hawana budi kubadili mitazamo yao. Jamii yetu bado inashindwa kuzungumza wazi kuhusu masuala ya uzazi, ikihofia aibu na tamaduni.
Matokeo yake, vijana wanabaki kujifunza kutoka mitandao ya kijamii, marafiki au maduka ya dawa, vyanzo ambavyo mara nyingi havina taarifa sahihi.
Ukimya wa wazazi ni chachu ya ujinga wa vijana kuhusu afya ya uzazi, hali inayosababisha matumizi mabaya ya dawa kama P2.
Vilevile, Baraza la Famasia na wizara husika zinapaswa kuimarisha udhibiti wa uuzaji dawa za P2 na dawa nyingine za uzazi wa mpango.
Wauzaji wanapaswa kutoa dawa hizo tu kwa ridhaa na ushauri wa daktari au mtaalam wa afya, kama ilivyo kwa dawa za hospitalini. Ni muhimu pia kuanzisha utaratibu wa kufuatilia na kutoa onyo kwa maduka yanayokiuka taratibu hizo.
Kwa upande mwingine, vijana wenyewe wanapaswa kuelewa kuwa afya ya uzazi ni sehemu muhimu ya maisha yao na ndoto zao za baadaye. Kutumia dawa za P2 mara kwa mara si ushahidi wa uhuru, bali ni kujiumiza taratibu.
Njia sahihi za uzazi wa mpango zipo, salama, za gharama nafuu na zenye ushauri wa kitaalamu. Wanawake na wasichana wanapaswa kuzitumia badala ya kutegemea dawa za dharura kila mara.
Nipashe tunaona elimu ya afya ya uzazi ndiyo silaha bora ya kukabiliana na tatizo hili. Serikali, taasisi za dini, mashirika ya kijamii na vyombo vya habari vinapaswa kushirikiana kutoa elimu endelevu, inayoeleweka na inayoheshimu maadili ya Kitanzania. Hatuwezi kuruhusu kizazi kipoteze afya yake kwa kutojua.
Tunawakumbusha wananchi kwamba dawa za P2 si kinga ya kudumu, bali ni msaada wa muda kwa hali maalumu. Kila mwanamke na msichana anapaswa kushauriana na daktari kabla ya kutumia dawa yoyote ya uzazi wa mpango. Ni bora kuchukua tahadhari mapema kuliko kujutia uamuzi mbaya baadaye.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED