KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imetoa meno yake kwa kutoa adhabu mbalimbali kwa wachezaji, waamuzi na klabu.
Kila aliyefanya kosa ameadhibiwa adhabu inayomstahili kwa mujibu wa kanuni.
Adbabu zilizotolewa ni nyingi, lakini zipo ambazo zimeonekana kugusa, au kuteka hisia za mashabiki wengi wa soka nchini.
Nazo ni za baadhi ya waamuzi kuondolewa kwenye orodha ya waliopangwa kuchezesha mechi zijazo za Ligi Kuu.
Waamuzi hao ni Omari Mdoe wa Tanga, aliyecheza mechi ya Mbeya City dhidi ya Yanga na Jackson Samuel, aliyechezesha mchi ya maafande wa JKT Tanzania dhidi ya Azam.
Imetajwa pia, Mdoe alishindwa kutafsiri tukio la dakika ya 46, ambapo mchezaji wa Mbeya City, Mateo Antony alishika mpira ndani ya eneo la hatari lakini hakuchukua hatua na lile la beki wa kati ya Yanga kumkanyaga kwa makusudi, Ibrahim Ame wa Mbeya City katika mechi iliyopigwa, Jumanne iliyopita, Uwanja wa Sokoine Mbeya. Kutokana na kutokuwa makini, ameondolewa kwenye orodha ya wataochezesha mechi za ligi kwa michezo mitano
Jackson naye amefungiwa michezo mitano na Kamati hiyo kwa kosa la kumkanyaga kwa makusudi mchezaji wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda, katika mchezo wa Ligi Kuu, uliopigwa, Jumatano iliyopita, Uwanja wa Meja Isamuhyo, mechi iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.
Mbali na hayo, Bacca, amefungiwa kucheza za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kosa la kumkanyaga makusudi, Ame wa Mbeya City na mchezaji mwingine wa JKT Tanzania, Mohamed Bakari naye amefungiwa michezo mitano wa Kamati hiyo kwa kosa la kumkanyaga kwa makusudi mchezaji wa Azam FC, Lusajo.
Kwanza kabisa tunaipongeza kamati hiyo kwa jambo moja la kuwahi kutoa adhabu hiyo mapema.
Ni tofauti na msimu mingine ambapo adhabu kama hizi hutolewa wakati waaamuzi au wachezaji wameshacheza zaidi ya michezo mitatu ndipo adhabu inatoka.
Siku zote adhabu ni fundisho, hivyo inatakiwa itoke mapema kwa ajili ya kumuumiza mhusika ili asirudie tena alichokifanya. Adhabu ikichelewa haiwi tena adhabu.
Ushauri wetu kwa kamati iendelee na uzi huu huu ili kuweka nidhamu kwenye mpira wetu, hasa soka la Tanzania ambalo kwa sasa linasonga mbele.
Hili ni onyo kwa waamuzi wengine ambao walikuwa wanatarajia au kufikiria kufanya hivyo kwa makusudi na kama si makusudi basi watakaochezesha watakuwa makini zaidi
Tunatoa ushauri pia kwa wachezaji kuwa mpira wa miguu ni kazi kama kazi zingine zozote, hivyo uchezaji wa kuhatarisha maisha ya mwenzako si mzuri.
Mchezaji anapaswa afikirie, kumkanyaga mwenzake kwa makusudi kama angekanyagwa yeye ingekuwaje? Angefurahia? Aina ile ya rafu tulizoziaona si za kimichezo, bali zinaweza kumfanya mchezaji kutofanya tena kazi hiyo maisha yake yule, kwani anaweza kupata ulemavu.
Kuna rafu za kumpira ambazo ni za kuhakikisha mpinzani haendi kukudhuru langoni kwako, lakini zingine kama zile tulizoziona ni za kuumizana na hazina maana, wala sababu yoyote zaidi ya kuharibiana maisha.
Nje ya timu, wachezaji wote ni kitu kimoja, wote ni wafanya kazi, na maisha ya uchezaji huwezi kujua leo ni wapinzani, kesho wanacheza timu moja, hivyo sioni haja ya kuumizana.
Nadhani kwa adhabu hizi zilizotoka, zitakuwa fundisho kwa wachezaji wengine. Ifike wakati iwe jambo la kulinda afya uwanjani ni la wachezaji wenyewe wa timu zote uwanjani. Ukimlinda mwenzako leo kesho atakulinda yeye. Kila mmoja anatafuta maisha na ana familia inayomtegemea.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED