Tunautaka ushindani JKT Queens vs Simba, Yanga Ligi Kuu wanaume

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:25 PM Oct 20 2025
 JKT Queens
Picha: Mtandao
JKT Queens

WAKATI kwenye Ligi Kuu ya wanaume, timu za Simba na Yanga zimekuwa ndiyo wababe wa kutwaa ubingwa, kwenye soka la wanawake hali imekuwa tofauti, baada ya JKT Queens kuwa ndiyo timu iliyojiwekea ufalme wake katika soka hili.

Wakiwa ndiyo mabingwa wa Tanzania Bara msimu uliopita tena kwa kuzinyanyasa Simba Queens na Yanga Princess, hali hiyo imeendelea kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu.

JKT Queens imeendelea kuzitambia timu hiyo katika mechi za Ngao ya Jamii zilizomalizika wiki iliyopita, zikichezwa, Uwanja wa KMC Complex.

Oktoba 9, maafande hao waliwaadhibu Yanga Princess jumla ya mikwaju 6-5 ya penalti, baada ya sare ya 1-1, katika mchezo wa nusu fainali wa Ngao ya Jamii na kutinga hatua ya fainali.

Katika mchezo wa fainali uliopigwa Oktoba 12 kwenye uwanja huo huo, iliichakaza Simba Queens mabao 2-1 na kutwaa Ngao ya Jamii.

Hii ni ishara kuwa bado JKT Queens ni imara na ndiyo timu inayoogopwa zaidi ya timu hizo mbili ambazo kaka zao wanaogopwa kwenye Ligi Kuu za wanaume.

Kwenye ligi ya wanaume, kwa misimu 12 mfululizo, Simba na Yanga zimekuwa zikigawana mataji.

Mara ya mwisho ni Azam FC, ikiyotwaa ubingwa msimu wa 2013/14 na tangu hapo hakuna timu iliyotwaa ubingwa zaidi ya timu hizo mbili ambapo zimekuwa zikipokezana.

Kwanza kabisa niipongeze JKT Queens kwa hicho inachokifanya licha ya kwamba haina wachezaji wa kigeni hata mmoja.

Inatumia wachezaji wa Kitanzania ambao wamekuwa wakiwatetemesha wa kigeni, wakiwaonesha kuwa hata hapa nchini kuna vipaji vingi tu, lakini tatizo linalotukabili ni kuwatafuta tu.

Imeelezwa kuwa viongozi wa JKT Queens wamekuwa wakizungumza kwenye shule mbalimbali za msingi na sekondari kusaka vipaji na kuvipeleka kwenye timu hiyo.

Kwa hali ninavyoiona, ligi ya soka ya wanawake itakuwa moja kati ya ligi ngumu mno na yenye msisimko na ushindani mkubwa kuliko ya wanaume ambako Simba na Yanga zinatawala.

Nasema hivi kwa sababu wakati Simba Queens na Yanga Princess zinataabika na JKT Queens, taratibu naiona timu ya Mashujaa Queens nayo ikianza kuwa moja ya timu ngumu na bora kwenye Ligi Kuu.

Inaonekana inafuata nyayo za JKT Queens, hivyo baada ya muda Ligi ya wanawake itakuwa na timu nne ngumu. Nadhani baada ya hapo zitapatikana zingine ambapo zitaifanya ligi ya wanawake iwe na mvuto, huku mshindi akiwa hatabiriki.

Ifike wakati timu za wanaume za Ligi Kuu ziige mfano wa JKT Queens kwa kujitengeneza heshima licha ya kwamba tunaelewa kuna matatizo mbalimbali ikiwamo timu kubwa za Simba na Yanga kuonekana kubebwa na baadhi ya matukio na maamuzi ya waamuzi.

Ingawa kuna timu kama Azam FC, ambayo inajitahidi, lakini bado haijafika kile kiwango ambacho Simba na Yanga inaihofia na kuleta ushindani kama JKT Queens kwa Simba Queens na Yanga Princess.

Kinachoonekana sasa kwenye soka la wanawake na inachokifanya JKT Queens iwe somo kwa timu za wanaume za Ligi Kuu.