Kwa hili, TFF hongereni

Nipashe
Published at 05:20 PM Oct 27 2025
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia
Picha: Mtandao
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia

LIGI ya Vijana chini ya Umri wa miaka 20, msimu huu umefanyiwa maboresho makubwa zaidi na moja wapo ni kuhakikisha wachezaji wenye umri husika tu ndio wanashiriki.

Hii maana yake ni kwamba, vijana chini ya umri wa miaka 20 watakuwa wamehakikiwa haswa kuwa wana umri huo, tofauti na miaka ya nyuma.

Ni kwa sababu tutashuhudia vijana halisi wenye miaka husika. Ligi hii inachezwa na vijana chini ya miaka 20.

Lakini kwa miaka kadhaa tumekuwa tukishuhudia wachezaji wengi wenye umri mkubwa tofauti na inavyotakiwa.

Ukiwaangalia tu usoni, utagundua kuwa wengi wao walikuwa wamezidi miaka 20, hivyo sasa ilikuwa si ligi ya vijana chini ya miaka hiyo kwa kuwa waliokuwa wakicheza wengi walikuwa wamezidi umri huo.

Wako wachezaji ambao ukiziona sura zao na maumbo yao ukiambiwa na umri wao, unaweza kubisha mpaka kupigana. Haviendani, hata mtoto mdogo anaweza kubaini.

Kwa maana hiyo ilikuwa inaondoa kabisa dhana ya michuano hiyo ambavyo lengo lake ni kusaka wachezaji chipukizi wenye vipaji ambao watakuja kuzisaida klabu za hapa nchini na taifa kwa ujumla.

Mara nyingi michuano ya vijana si ya kusaka ubingwa, bali kuibua, kulea na kuendeleza vipaji hatimaye vikisha komaa ndiyo vianze kutumika na kutoa matunda.

Lakini mara nyingi viongozi wa timu hizo, husaka wachezaji wa mitaani wanaocheza ndondo na kuwachukua kuziwakilisha timu zao kwa malengo ya kuchukua ubingwa tu.

Kutokana na hali hiyo vijana ambao hilo ndilo jukwaa lao wengi wanakosa nafasi ya kuonekana, hatimaye vipaji vyao vinaishia mitaani.

Na sasa Shirikisho la Soka Tanzania limetoa ratiba ya Ligi ya vijana chini ya miaka 20 ambayo itaanza Novemba 11, mwaka huu.

Timu ya vijana ya Simba chini ya miaka 20, itaanza mechi yake ya kwanza na ya ufunguzi wa Ligi ya hiyo, itakapocheza na JKT Tanzania, Uwanja wa TFF Centre Kigamboni, ukiwa mchezo wa Kundi A, huku Yanga ikianza dhidi ya Prisons Novemba 12, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Jumla ya timu 16 zinashiriki, zikiwa zimegawanywa kwenye makundi mawili, huko zote zikiwa ni vikosi vya pili kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu.

Simba inaliongoza Kundi A, likiwa na timu za JKT Tanzania, Dodoma Jiji, Mashujaa FC, Singida Black Stars, TRA United, KMC na Pamba Jiji, huku Kundi B, linaloongozwa na Yanga, zipo timu za Prisons, Azam FC, Namungo, Mbeya City, Coastal Union, Mtibwa Sugar na Fountain Gate.

Jambo la msimu zaidi ni kumsikia Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Oscar Mirambo, akisema kabla ya ligi hiyo msimu huu walikuwa na kazi ya kuwapima wachezaji wote umri kwa kutumia kifaa maalum ambacho kitaalam kunaitwa, 'Magnetic Resonance Imaging', (MRI).

Mirambo alibainisha kuwa wamewaondoa wachezaji wengi kutoka timu zote, kiasi kwamba zilibakia na wachezaji wachache. Kwa maana hiyo klabu zitalazimika kuendelea kusaka wachezaji wengine vijana wenye umri sahihi.

Kaimu Katiba Mkuu huyo alisema ni Prisons pekee ndiyo iliyoongoza kwa kuwa na wachezaji wenye umri sahihi.

Kwa hili lililofanywa na TFF, wanastahili pongezi na sasa inaonekana wamedhamiria kabisa kuibua vipaji vya wachezaji wapya nchini badala ya wale wale kila kukicha tunaowaona kwenye Ligi Kuu wakibadilisha timu kila msimu.

TFF wametumia gharama kubwa kukipata chombo kifaa cha MRI, na kuwalipa wataalam kukitumia kwa ajili ya kuwapima wachezaji.

Kwa maana hiyo msimu huu sasa tunaona ushindani halisi na wenye uwiano halisi baina ya timu na timu kutokana na umri wa vijana hao.

Kitakachoonekana sasa ni vipaji vya wachezaji wenyewe uwanjani, ambavyo vitawasaidia walimu kuvichukua, kuviongezea ujuzi na kuvilea.

Hivyo tunasema kuwa Ligi ya vijana chini ya umri wa miaka msimu wa 2025/26 itachezwa bila vijeba.