Kisa cha mjane Alice kiwe somo kwa wanaodhulumu wanyonge

Nipashe
Published at 01:11 PM Oct 22 2025
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akimpa siku tano (5) Mohamed Mstafa kujisalimisha kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa kabla ya hatua zaidi hazijachukuliwa
Picha: Mtandao
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akimpa siku tano (5) Mohamed Mstafa kujisalimisha kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa kabla ya hatua zaidi hazijachukuliwa

TUKIO la serikali kumrejeshea Alice Haule, mjane mkazi wa Kinondoni, nyumba yake iliyokuwa imenyang’anywa kwa njia isiyo halali, ni ushindi mkubwa wa haki na utu wa mwanadamu.

Ni tukio linalopaswa kupongezwa kwa nguvu zote, si tu kwa sababu mjane huyo amepata haki yake, bali kwa sababu linaleta matumaini mapya kwa maelfu ya wananchi wanaokandamizwa kimyakimya kila siku chini ya kivuli cha ukatili wa madaraka na ujanja wa kisheria.

Kwa miezi kadhaa, Alice alipitia mateso ambayo hayakupaswa kumpata raia yeyote katika nchi inayojinasibu kuwa na utawala wa sheria. Kufukuzwa kwake kwa nguvu kutoka nyumbani, mali yake kuuzwa kwa ujanja bila kibali cha mahakama, na kunyimwa haki ya kujitetea ni mambo yanayoibua maswali makubwa kuhusu mfumo wetu wa utoaji haki na nidhamu ya watendaji wa umma.

Hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kuingilia kati na kurejesha nyumba hiyo kwa mmiliki halali ni ya kupongezwa. 

Hii ni dalili kwamba pale ambapo dhamira njema inatangulia mbele ya maslahi binafsi, haki inaweza kushinda hata pale ambapo ujanja na fedha vilionekana kutawala. 

Kauli yake kwamba “serikali ipo upande wa haki” inapaswa kuwa mwongozo wa kweli wa utendaji katika kila ngazi ya utawala.

Hata hivyo, tukio hili linaacha maswali mazito ya msingi. Wako wangapi kama Alice ambao hawana fursa ya kusikilizwa? Wako wangapi waliopoteza ardhi, nyumba au mashamba kwa mikopo ya ujanja na makubaliano ya kifisadi, bila kupata msaada wa mamlaka yoyote? Wako wangapi ambao sauti zao hazijawahi kufika ofisini kwa viongozi wenye dhamira kama aliyoonesha Chalamila?

Ni dhahiri kwamba tatizo hili si la mtu mmoja. Ni dalili ya mfumo dhaifu wa ulinzi wa wanyonge na usimamizi hafifu wa haki za ardhi na mirathi.

Matapeli wengi wamekuwa wakitumia mianya ya kisheria, uelewa mdogo wa wananchi na urasimu katika mahakama kujinufaisha kupitia mali za wajane, yatima na wazee. 

Mara nyingi, wanufaika wa uovu huo wamekuwa na kinga ya ushawishi au uhusiano na watendaji serikalini, jambo linalozidisha ukosefu wa imani kwa mfumo wa haki.

Kwa mantiki hiyo, hatua ya kurejesha nyumba kwa Alice inapaswa kuwa mwanzo wa mabadiliko ya kimfumo. Serikali isiishie kutoa tamko la uadilifu bali ichukue hatua thabiti za kujenga mifumo madhubuti ya kulinda mali za mirathi, kuwajengea wananchi uelewa wa kisheria na kuweka ufuatiliaji wa karibu kwa maofisa wanaohusika na kesi za ardhi na mirathi.

Aidha, hatua ya kumlipa mjane huyo fidia ya Sh. milioni 10 ni muhimu kama ishara ya kuomba radhi, lakini haitoshi kulipa maumivu ya kisaikolojia na kiuchumi aliyopitia. 

Fidia hiyo itakuwa na maana zaidi iwapo itafuatwa na uwajibikaji halisi. Wale wote waliohusika katika kumfukuza, kuidhinisha mauziano haramu au kutumia nguvu bila mamlaka lazima wawajibishwe kisheria. Ni kupitia hatua kama hizo tu ndipo ujumbe wa uadilifu wa serikali utakuwa na meno.

Zaidi ya hayo, ni wakati wa kuimarisha mfumo wa usimamizi wa mirathi. Mirathi si suala la kifamilia pekee; ni kipimo cha utu na usawa katika jamii. Pale mjane anaponyang’anywa mali za mumewe, ni heshima ya taifa lote inayodhalilishwa. 

Ni wajibu wa serikali na jamii kwa pamoja kuhakikisha kuwa mjane, yatima au mwenye ulemavu hana tena sababu ya kuishi kwa hofu ya kuporwa anachostahili.

Tukio la mjane Alice limetufunza jambo muhimu: haki inaweza kuchelewa, lakini inapofika, huangaza giza lote la dhuluma. Serikali imeonesha upande wake mzuri, lakini imani ya wananchi haitajengwa kwa matukio machache. Itajengwa pale kila ofisa wa umma atakapowajibika kwa haki, bila hofu wala upendeleo.

Kwa sasa, Nipashe tunampongeza Alice kwa ujasiri wake na Mkuu wa Mkoa kwa uamuzi wa kishujaa. Zaidi ya hapo, tuitake serikali kusimamia haki kwa wote, bila kusubiri kamera, bila kelele za mitandao na bila kuchagua nani ni muhimu zaidi.