Waliofanya udhalilishaji mwanafunzi wasifumbiwe macho

Nipashe
Published at 09:37 AM Apr 23 2025
Waliofanya udhalilishaji mwanafunzi wasifumbiwe macho
Picha:Mtandao
Waliofanya udhalilishaji mwanafunzi wasifumbiwe macho

KATIKA tukio lililotokea hivi karibuni na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii linaloonesha mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu akidhalilishwa na wenzake, limeonesha picha mbaya na halipaswi kufumbiwa macho.

Tukio hilo la udhalilishaji limefanywa na wanafunzi wa kike, wakimfanyia mwanafunzi mwenzao.

Hakika tukio hilo limeibua mijadala katika majukwaa mbalimbali ya kijamii na kuhoji iweje wanafunzi hao wasomi wa chuo kikuu wenye uelewa wamfanyie mwenzao udhalilishaji huo.

Kitendo hicho kingefanywa na watu wa mtaani isingekuwa gumzo, kwa kuwa inaeleweka kuwa baadhi yao hawana uelewa wa masuala mbalimbali ikiwamo ya kisheria na haki za binadamu.

Kwa wanafunzi waliosoma mpaka kufikia elimu ya juu wanachukuliwa kuwa wana uelewa mkubwa wa masuala mbalimbali yakiwamo ya kupinga ukatili wa kijinsia.

Suala la ukatili wa kijinsi limekuwa likiimbwa na kukemewa si na serikali pekee bali hata taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali na wanaharakati wanaopinga vitendo hivyo.

Kwa wasomi kama walioonekana kwenye mitandao ya kijamii wakifanya kitendo hicho, kunaibua maswali kama kweli wamefikia elimu ya juu ya chuo kikuu na badala ya kuwaza masomo, wanafanya mambo ya ovyo na kugombania wanaume.

Wazazi wao nyumbani wanajua watoto wao wako vyuoni kuongeza ujuzi na maarifa ili watakapohitimu waweze kuwajibika vyema wanapopata ajira ili nao waweze kusaidia wazazi wao na kufaidi matunda, lakini kwa picha waliyoionesha kuna walakini.

Mtu anaweza kujiuliza, hawa watu wakimaliza chuo na kupata ajira wanaweza kweli kuwajibika kazini na kutenda haki?

Hivi hiyo elimu waliyokwenda kuitafuta ni hiyo ya kugombania mambo ya ovyo? Kimsingi wameshajipotezea sifa za kupata ajira kutokana na kuonekana kwenye mitandao ya kijamii.

Tunashukuru kuwa baada ya tukio hilo kusambaa kwenye mitandao, uongozi wa chuo kilichotajwa umeanza kufuatilia kujua kama kweli wanafunzi hao wanasoma kwenye chuo hicho ili taratibu za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Pia, kuna jukwaa la Women Inspire Women (WIW), ambalo limetoa tamko kulaani matukio ya udhalilishaji watoto wa kike nchini.

Jukwaa hilo limelaani udhalilishaji uliofanywa na kundi la wanafunzi wa kike dhidi ya mwanafunzi mwenzao na kusema ni kinyume na maadili ya utu, heshima ya binadamu na halilingani kabisa na matarajio ya jamii kutoka kwa wasomi wa ngazi ya elimu ya juu.

Aidha, limesema ni ishara ya wazi ya ukosefu wa maadili, nidhamu na uelewa wa haki za binadamu miongoni mwa baadhi ya vijana walioko vyuoni.

Ukatili na udhalilishaji wa aina yoyote ni kosa la jinai na haupaswi kuvumiliwa kwa namna yoyote na kwamba kuwa na elimu ya juu haipaswi kuwa uwanja wa kudhalilisha , bali ni jukwaa la kukuza fikra, utu na mshikamano wa kijamii.

Jamii kwa nafasi yao wana wajibu wa kuwafundisha vijana kuheshimu tofauti za kutatua migogoro kwa njia ya kistaarabu na kisheria.

Wanawake wanapaswa kuepuka tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kufuata taratibu za kisheria katika kutatua changamoto mbalimbali.

Jukwaa la WIW limeahidi kuendelea kufuatilia kwa karibu matukio hayo ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia na kusimama mstari wa mbele kulinda haki, kuhimiza uwajibikaji na kujenga jamii yenye usawa, utu na heshima kwa wote.