WANAHABARI kutoka vyombo mbalimbali nchini, juzi walitunukiwa Tuzo za Uandishi wa Habari za Samia, maarufu kama Samia Kalamu Award ikiwa ni kutambua mchango wao kwa uandishi wa habari za maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Katika tuzo hizo, wanahabari walijizolea zawadi mbalimbali ambazo zimewafanya wajisikie fahari katika kuitumikia taaluma yao ambayo kwa miaka mingi ilionekana kama haina maana kwa baadhi ya Watanzania. Licha ya kuitwa mhimili wa nne wa dola usio rasmi kutokana na dhima yake kwa jamii, tasnia ya habari ilionekana kama vile ni fani ambayo ipo kwa ajili ya kuchokonoa viongozi na wanasiasa kuhusu yale yanayofanyika katika serikali na taasisi zake.
Kuwapo kwa dhana hiyo, baadhi ya wanasiasa na watu wengine walikuwa wakiwaona wanahabari kama maadui na walikuwa wakiwachukia kutokana na kutekekeza majukumu yao ya kila siku. Wakati mwingine, wanahabari pia walikuwa wakitumiwa tu na baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara kufikisha ujumbe wao na baada ya hapo walikuwa hawana habari nao.
Mwanzoni mwa miaka ya 2000 jijini Dodoma, kulikuwa na tukio la utiaji saini uwekezaji katika mradi wa makaa ya mawe na chuma Mchuchuma na Liganga mkoni Njombe lililohusisha wataalamu wa serikali, viongozi na wawekezaji kutoka Afrika Kusini. Baada ya hafla hiyo, ilifuatia chakula lakini waandishi wa habari walizuiwa na ofisa mmoja wa serikiali kwa madai kwamba wasije wakamwandika Waziri akimwagikiwa na mchuzi wakati anakula.
Hilo ni tukio mojawapo linaloonesha kuwa waandishi wa habari ni watu wanaowekwa katika daraja la chini katika jamii. Kwa maneno mengine, wanahabari wamekuwa wanaonekana kama watu wa daraja la tatu licha ya umuhimu wao katika matukio au shughuli za kisiasa, kijamii na kiuchumi. Hata baadhi ya taasisi ambazo huandaa tuzo, zimekuwa zikitoa zawadi za viwando duni.
Baada ya kuwapo kwa hali hiyo miaka nenda rudi, hatimaye Tuzo za Samia Kalamu zimeitoa kimasomaso taaluma ya habari na kuonekana ni ya viwango vya juu kwa wanahabari walioshinda kuonekana ni watu wa maana na wenye thamani katika jamii.
Katika tuzo hizo, waandishi wa habari walizawadiwa viwanja kwa ajili ya kujenga nyumba, mashamba kuendeleza shughuli za kilimo, boti na mashine za umeme kuendesha uvuvi na fursa za mafunzo Ufaransa, Marekani na Japan ili kuinua taaluma. Kubwa zaidi baadhi ya wanahabari wamepatiwa mamilioni ya fedha hadi Sh. milioni 50 kuendeleza shughuli zao za kimaisha. Pia wengine wamezawadiwa vyombo vya usafiri kuwawezesha kufika maeneo ya kazi kwa wakati, hivyo kuwachochea kufanya kazi kwa ufanisi na kwa viwango.
Hakika Tuzo za Samia Kalamu zimeleta mapinduzi ya kweli katika tasnia ya habari Tanzania ambayo kwa miaka mingi ilionekana kuwa si lolote si chochote na baadhi ya Watanzania. Kutolewa kwa tuzo hizo, zawadi na fedha kwa washindi, kumewafanya Watanzania kuamini kuwa uandishi wa habari ni fani muhimu katika kukuza na kuendeleza uzalendo, hivyo kuacha dhana iliyojengeka kuwa ni fani ya waliofeli masomo au kukosa kazi.
Rais Samia Suluhu Hassan katika kuonesha kwamba fani ya habari ni ya muhimu, ameudhihirishia umma kwamba uandishi ni taaluma kama zilivyo taaluma zingine ndiyo maana wanataaluma hao wameanzishiwa bodi ya ithibati ili watambulike kama ilivyo kwa wanataaluma wengine kama wahandisi, wahasibu, wataalamu wa afya na wanasheria.
Kutokana na kuvunjwa kwa ukimya huo kuhusu umuhimu wa tasnia ya habari, ni wakati sasa kwa wanataaluma kutembea kifua mbele na kuuzika unyonge uliokuwa umetamalaki sasa umewafanya wawe wenye nguvu na heshima katika jamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED