Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia iwe chachu ya kumaliza migogoro

Nipashe
Published at 11:51 AM Apr 15 2025
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama  Samia iwe chachu ya kumaliza migogoro
Picha:Mtandao
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia iwe chachu ya kumaliza migogoro

TANGU Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ilivyoanza maeneo mbalimbali nchini, imesaidia wananchi wengi ambao walikosa msaada wa kisheria kutatua kero zao na kupata haki zao.

Kampeni hiyo imeanzishwa kwa lengo maalumu la kusaidia wananchi hasa wasiokuwa na uwezo wa kuweka wanasheria wa kuwasimamia katika kesi zao, waweze kupata msaada wa wanasheria na kuelekezwa njia sahihi za kufuatwa.

Kampeni hiyo imeibua wananchi wengi hasa kinamama ambao wengi wamedhulumiwa haki zao za kumiliki mali baada ya waume zao kufariki dunia na ndugu wa mume kuwanyang’anya mali zao.

Hivi sasa kampeni hiyo iko katika Mkoa wa Kagera, wilayani Bukoba ambako inaelezwa kuwa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya dhuluma wilayani humo ipo haja ya serikali kufika na kutatua kesi mbalimbali na kwa kutumia wataalamu wa msaada wa kisheria.

Wananchi wa mkoa huo wanasema msaada wa sheria katika jamii ni njia pekee ambayo itasaidia kuelewa haki na usawa wa migogoro inayoendelea katika ardhi.

Kwa mujibu wa wananchi hao migogoro ya ardhi imekuwa ni tatizo katika familia hali ambayo imefanya unyanyasaji wa kudhulumiwa haki ambayo mwanajamii alitakiwa apate urithi kama mwana familia.

Matatizo yanayoibuka ni baadhi ya wanafamilia kuibuka na kugombania kwamba walipewa kama mrithi wa eneo, au mipaka inatenganisha kiwanja cha mwingine na pengine ni hatua ndogo tu ndio zinafanya kutokuelewana.

Aidha, matatizo hayo ya kumiliki mali kutoka kwa wazazi waliofariki yamesababisha kesi za urithi za muda mrefu, wengine zaidi ya miaka 10 na kushindwa kupata haki zao kisheria.

Tatizo kubwa linalosababisha wengi kukosa haki hizo ni kukosa utetezi kutoka kwa wanasheria kwa sababu ya kukosa uwezo wa kuwalipa.

Kutokana na hilo, mali nyingi zinapotea kwa kuharibika kwa kukosa kuendelezwa na hiyo yote inatokana na ubinafsi wa baadhi ya watu na uvivu wa kutafuta mali zao badala yake wakisubiri mali za kurithi.

Katika kuhakikisha kuwa mkoa wa Kagera unakabiliana na tatizo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa alisema msaada huo tayari umefika mkoani humo Aprili 14, 2024 na kuwa watakuwapo kwaajili ya kutoa msaada kwa ngazi mbalimbali.

Wataalam wa sheria kitaifa na wilaya watatoa msaada wa sheria mkoani Kagera ikiwa ni kampeni iliyotolewa na Rais  Samia Suluhu Hassan yenye lengo la kusaidia wananchi.

Pia, ipo fursa kwa wananchi mkoani Kagera kutumia msaada wa sheria kutatua kero zao zinazohusu sheria kwa kuwa sio wakazi wote wanaoweza kutafuta wanasheria au mawakili.

Msaada wa kisheria kupitia kampeni ya Mama Samia ni msaada kwa wananchi katika kutatua matatizo yao na Kagera ni miongoni mwa mikoa ambayo ina matatizo ya migogoro ya ardhi, mirathi na dhuluma katika maeneo mbalimbali kwenye vitongoji, vijiji na mitaa.

Kampeni ambayo imetolewa na Rais bado ni sehemu ya watumishi kuendelea kutoa msaada wa sheria kwa kuanzisha kliniki ambazo zitakuwa msaada kwa wananchi.

Malalamiko yanayohitaji utatuzi wa kisheria juu ya ardhi na dhuluma mbalimbali ni mengi hali inayoashiria kuwa yapo matatizo katika jamii yanayohitaji usawa.