TANZANIA na TANESCO imepata pigo kwa kumpoteza kiongozi aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Mhandisi Boniface Nyamohanga aliyefariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea Bunda mkoani Mara juzi.
Historia inaonyesha kuwa Nyamohanga mwenye umri wa miaka 63, alizaliwa Juni 18, 1962 mkoani Mwanza. Alikuwa kiongozi mashuhuri aliyekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya nishati ambaye kitaaluma ni mtaalamu au mhandisi umeme
Nyamohanga atakumbukwa kwa utumishi uliotukuka amefanya kazi kwenye ofisi ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Dodoma, akiwa na jukumu la kusimamia shughuli za ukumbi mpya wa mikutano ya bunge.
Akiwa mhandisi stadi na kiongozi mwenye maono, alijitolea kwa kazi mbalimbali kuchagiza maendeleo ya nchi kwa mchango wake alioutoa kwa kila taasisi alizofanya kazi.
Baadaye alihamia Wakala wa Nishati Vijijini REA kuanzia mwaka 2008 hadi 2019 akiwa meneja msaidizi wa ufundi na kufanikisha kufikisha na kuboresha utoaji wa huduma ya nishati hasa umeme vijijini na vitongojini.
Uwezo mkubwa wa mhandisi huyo wa kuunganisha maarifa ya kiufundi na utekelezaji kwa vitendo, ulisaidia kuboresha huduma za nishati katika maeneo mbalimbali vijijini.
Aliwahi kuwa mwanachama wa Jukwaa la Kitaifa la Ushauri wa Nishati kuanzia mwaka 2017 hadi 2020. Katika jukumu hilo, alitoa ushauri muhimu kwa serikali kuhusu masuala yanayohusiana na nishati na jukumu lake katika kuleta maendeleo ya nchi.
Juni 2021, uongozi wake ulitambulika zaidi pale Rais Samia Suluhu Hassan alipomteua kuwa mjumbe wa Baraza la Ushindani wa Haki kwa kipindi cha miaka mitatu.
Uteuzi huo ulizingatia sifa zake, utaalamu na kujitolea huku jukumu lake katika baraza hilo likiwa ni kuhakikisha kuwa ushindani sokoni unabakia kuwa wa haki na uwazi.
Akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, alikuwa na jukumu kubwa katika kusimamia mifumo ya usambazaji umeme nchini, huku uongozi wake ukiwa na sifa mchanganyiko.
Miongoni mwa sifa hizo ni ustadi wa kiufundi, mtazamo wa kimkakati na kujali kwa dhati masilahi ya wafanyakazi na wateja, lakini akiwa na jukumu la kudhibiti matatizo ya shirika hilo.
Chini ya uongozi wake, ilianza miradi kadha ya kisasa yenye lengo la kuongeza ufanisi wa usambazaji wa nishati katika maeneo mbalimbali ya nchi ambayo hayana huduma ya uhakika ya nishati hiyo.
Katika muda wote wa kazi yake, alidumisha ushirikiano wa kitaaluma ambao uliboresha zaidi akiwa Mhandisi Mtaalamu aliyesajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB).
Mbali na kuwa mtendaji mkuu wa TANESCO, alikuwa ni mwanachama wa mashirika mbalimbali makubwa ya kitaaluma kama Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania (IoDT), Taasisi ya Wasuluhishi Tanzania (TiArb), Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA).
Mbali na hayo, imo pia Jumuiya ya Kimataifa ya Nishati ya Jua (ISES), na Taasisi ya Usimamizi wa Miradi (PMI) yenye makao yake makuu nchini Marekani.
Hata hivyo, maisha na kazi yake vimefikia mwisho usiotarajiwa na wa kusikitishwa juzi baada ya kupata ajali wilayani Bunda mkoani Mara wakati dereva wake akimkwepa mwendesha baiskeli.
Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya mhandisi Nyamo-hanga, kazi na utumishi wake uliotukuka na mchango wako mkubwa katika kufikia maendeleo ya Tanzania kwenye maeneo mbalimbali vyote vitabaki kuwa kumbukumbu kwa Watanzania na wazalendo.
Kifo chake cha ghafla kimeleta mshtuko katika sekta ya nishati na kwingineko, kwani si kwa wale tu wanaomfahamu, bali pia kwa Watanzania kutokana na mchango kwenye nishati.
Maisha aliyoishi ambayo historia inaonyesha kuwa yalijaa utumishi kwa ajili ya maendeleo ya nchi, yamekatishwa ghafla na ajali ya gari, hivyo, mwendo umeumaliza na matendo yako mema yanafuatana nawe.
Tunaiombea faraja, nguvu na ustahimilivu familia yako, ndugu zako . Aidha, tunazidi kuwapa tumaini wale wote waliokuwa wanakutegemea na kukuona kuwa una umuhimu wa kipekee kwenye maisha yao kuwa Mungu amekuchukua lakini hatawaacha.
Poleni pia wana TANESCO na sekta ya nishati na umeme ambayo ilitegemea ushauri, uchapakazi na muongozo wa Nyamohanga.
Bwana ametoa Bwana ametwaa jina la Mungu lihimidiwe.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED