Uchaguzi wa CHADEMA ulishamalizika, makundi na chokochoko ya nini jamani?

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 11:32 AM Apr 02 2025
Uchaguzi wa CHADEMA ulishamalizika, makundi na chokochoko ya nini jamani?
Picha: Mtandao
Uchaguzi wa CHADEMA ulishamalizika, makundi na chokochoko ya nini jamani?

JANUARI 22 mwaka huu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilifanya uchaguzi wa viongozi wake wa juu, huku Tundu Lissu akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa taifa wa chama hicho.

 Wapo viongozi wengine waliochaguliwa katika uchaguzi huo akiwamo John Heche ambaye kwa sasa ndiye Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA taifa akimsaidia Lissu majukumu.
 
 Hata hivyo, tangu uchaguzi huo umalizike, kumekuwapo na sintofahamu ya kurushiana vijembe kati ya waliochaguliwa na waliowekwa pembeni kwenye kinyang'anyiro hicho kilichokuwa cha vuta nikuvute.
 
 Binafsi ninaamini kuwa suala la mabadiliko ya uongozi katika chama ni jambo la kawaida ambalo halikwepeki. Kwa mtu unaweza kuongoza leo, lakini kesho ukang'atuka na kuwaachia wengine kijiti.
 
 Nilitarajia kwamba hata CHADEMA wamefanya hivyo, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha demokrasia, lakini ajabu ni kuona wale walioshindwa katika uchaguzi kuwarushia vijembe viongozi wapya.
 
 Lakini pia kwa upande mwingine inashangaza kuona hata waliochaguliwa nao kuwarushia vijembe viongozi wa zamani, jambo ambalo ninaamini linaweza kusababisha mgawanyiko kama ilivyokuwa wakati wa kampeni za uchaguzi huo.
 
 Nini kimesababisha wanachama kuendelea kukosoana hadharani wakati uchaguzi ulishamalizika siku nyingi? Ndivyo utaratibu wa chama chenu ulivyo kwamba mgombea akishindwa akosoe hadharani walioshinda?
 
 Je, ndivyo utaratibu wa chama chenu ulivyo kwamba aliyeshinda asiwape uzito wale walioshindwa. Ninadhani ipo haja kwa pande mbili kukaa pamoja na kusaidiana jinsi kuimarisha umoja wenu.
 
 Mnajenga nyumba moja ambayo ni chama chenu, kwanini kama kuna jambo halipo sawa muitane na kurekebishana badala ya kukosoana hadharani kana kwamba nyie ni wa vyama viwili tofauti?
 
 Ninajua kwamba katika harakati za kutafuta nafasi ya uongozi ndani ya chama, ni dhahiri kulikuwa na makundi yaliyokuwa ‘yakipambana’ hapa na pale kila upande ukitaka wagombea wao washinde.
 
 Lakini, baada ya uchaguzi kumalizika, makundi hayo huwa yanakufa kifo cha asili huku wanachama wakiunganisha nguvu ili kukabili maadui wa chama chao katika uchaguzi unaoshorikisha vyama vyote.
 
 Kwa maana hiyo, walioshinda na walioshindwa wanakuwa ni wamoja na sio kusemana vibaya na kuwapa faida maadui wenu kisiasa kitendo ambacho ni sawa na kudhoofishana wenyewe.
 
 Makundi wakati wa kampeni, kimantiki hayaepukiki. Uchaguzi umeisha,  viongozi wamepatikana, sasa ni muda wa kuyavunja ndani ya chama na kuwa kitu kimoja kwa maslahi ya chama badala ya kuyaendeleza.
 
 CHADEMA ni chama kikuu cha upinzani, ndicho kinachotegemewa kuleta chachu kwa vyama vingine vya upinzani kwa kujifunza jinsi ya kuwa imara katika siasa, lakini chokochoko zikiendelea, ni wazi kwamba makundi yaliyokuwa yanapingana wakati wa kampeni hayajavunjwa.
 
 Kimsingi, kutokuwapo makundi yanayotokana na uchaguzi, ni sawa na kuendeleza umoja ndani ya chama, lakini yakipewa nafasi, yanaweza kuleta mpasuko ambao ungedhibitiwa mapema.
 
 Ikumbukwe kuwa baadhi ya migogoro ni midogo na huweza kusuluhishwa kwa haraka. Migogoro mingine ni mikubwa ambayo huweza kuacha madhara makubwa yasiyoweza kurekebishwa.
 
 Kukosona kunakoendelea ndani ya chama baada ya uchaguzi, ni matokeo ya makundi wakati wa kampeni na mgogoro mdogo ambao unaweza kumalizwa haraka, lakini ukiachwa unaweza kuwa mkubwa.
 
 Ingawa migogoro mingi vyanzo vyake huwa si rahisi kuvigundua haraka, lakini kukosoana hadharani katika chama ni rahisi kugundua kuwa ni makundi ya kampeni za uchaguzi uliopita ambayo hayajavunjwa.
 
 Hivyo nimalizie tu kwamba, uchaguzi CHADEMA ulishamalizika, makundi yasipewe nafasi, kwani yanaweza kusababisha chama kisipige hatua kwenda mbele.