Kulinda, kudumisha amani jukumu la kila mtanzania

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 10:47 AM Apr 03 2025
 Kulinda, kudumisha amani jukumu la kila mtanzania.
Picha: Mtandao
Kulinda, kudumisha amani jukumu la kila mtanzania.

TANZANIA imekuwa ikitajwa kuwa kisiwa cha amani. Msemo huo umedumu katika awamu zote za uongozi wa nchi tangu ilipoundwa baada ya kuunganishwa na yaliyokuwa mataifa ya Tanganyika na Zanzibar.

Viongozi wengi hususan wa serikali na chama tawala- Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanapokuwa majukwaani, wamekuwa wakisisitiza suala la kulinda amani. Licha ya kusema hivyo, baadhi wamekuwa wakivuka hata mipaka nyakati za uchaguzi kuwa waichague CCM ndiyo inayodumisha amani na wapinzani wakichaguliwa, amani inaweza kutoweka.

Kauli hizo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya wanasiasa wengine wakionya kuwa watanzania wajifunze kutoka Rwanda na Budundi kwa madai kuwa nchi inaweza kuingia kwenye machafuko kama wapinzani watapewa dola! Kwa ujumla, kauli hizo na zile zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wa vyama vingine kama nchi haiwezi kutawalika kwa sababu Fulani, ni viashiria tosha vya uvunjifu wa amani. 

Jumatatu ilikuwa sikukuu ya Idd el Fitri ambayo iliadhimishwa mkoani Dar es Salaam na Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi. Katika maadhimisho hayo, jambo kubwa lililotawala ni kudumishwa kwa amani huku Rais Samia akitoa rai kwa Watanznia kudumisha amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu huku akiwatwika jukumu hilo viongozi wa dini.

Wakati Rais Samia akitoa wito huo, Shekhe Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir, alitaka kutokuvumiliwa kwa mtu au kikundi cha watu watakaothubutu au kutoa kauli zinazohatarisha uvunjifu wa amani.

Kauli hizo zimewaibua wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini na siasa, wakitoa maoni tofauti kuhusu nini kinachotakiwa kufanyika ili kudumisha amani huku. Wadau hao wamesisitiza kuwa amani ya nchi ikayosisitizwa inaweza kuwapo kama kasoro zilizojitokeza wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 na 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 zitafanyiwa kazi kwa kuwa mifumo ya uchaguzi isiyotoa haki kwa wananchi inaweza kuwa chanzo cha machafuko.

Katibu Mkuu wa Baraza la maaskofu wa kanisa la katoliki, Dk. Charles Kitima, alisisitiza kuwa haki ndio msingi wa amani na kama haitatendeka katika jamii, hata suala la amani litakuwa changamoto. Alisema amani itakuwapo kama watu watatendewa haki, watapewa haki zao na haki hizo kama zitalindwa wakati wote na waliopewa dhamana. 

Kiongozi wa Chama cha ACT – Wazalendo, Dorothy Semu, kwa mfano, alisema jamii haina budi kufahamu kuwa amani ni tunda la haki na kwamba kama haki haitatendekea kama ilivyojitokeza katika uchaguzi wa 2019, 2020 na 2024 ni vigumu amani kudumishwa. 

Askofu Dk. Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), alisema haki ndiyo inayowaunganisha watu wote (wakiwamo watanzania) bila kujali itikadi, imani, jinsia, kabila, hali ya kiuchumi, urefu wala kimo cha mtu. Pamoja na kufafanua hayo, alisema hivi sasa mtu anaposimama na kuzungumzia haki, anahojiwa ni wa chama gani badala ya kusikilizwa anazungumza nini. 

Mdau mwingine, Wakili Dk.  Onesmo Kyauke, alisisitiza kuwa ni muhimu kila mtu kutimiza wajibu wake katika kufuata sheria huku akibainisha kuwa uchaguzi hauna maana ya kuvunja sheria bali kuhubiri amani, umoja na mtangamano wa kitaifa. Pia alisisitiza kuwa amani inaweza kuvunjwa kwa mambo mbalimbali yakiwamo wanasiasa kuchochea kutaka wachaguliwe kwa misingi ya udini ukabila, ukanda au jinsia. 

Wadau hao wameeleza kwa kinagaubaga kuwa kuna umuhimu wa kulinda amani lakini jambo hilo linawezekana iwapo mamlaka zilizopewa dhamana zitasimamia utoaji haki. Kuna maneno katika maandiko matakatifu kuwa haki huinua taifa bali dhambi ni aibu kwa watu wote. 

Kwa mantiki hiyo, kama haki itatendeka katika jamii, kuna nafasi kuwa ya kushamiri kwa amani lakini kama haki haitatendekea, ni vigumu kwa amani kushamiri. Kwa mfano kama mahakama zitapindisha haki, polisi kukandamiza haki kwa maslahi ya wachache na huduma kutolewa kwa misingi ya upendeleo, ni ndoto kupatikana kwa haki, hivyo suala la amani ni la kila mtanzania.