Pongezi NHIF kujiendesha kwa faida baada ya miaka mitano ya hasara

Nipashe
Published at 12:09 PM Apr 08 2025
Pongezi NHIF kujiendesha kwa faida baada ya miaka mitano ya hasara
Picha:Mtandao
Pongezi NHIF kujiendesha kwa faida baada ya miaka mitano ya hasara

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ambao mwaka jana uliripotiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kuwa uko hatarini kufisilika, umeimarika.

Wakati Ripoti ya CAG kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2023 ilionesha ulikuwa umepata hasara kwa miaka mitano mfululizo kutokana na kutoa fedha zaidi ya unachoingiza, ripoti mpya ya ukaguzi inaonesha umeanza kujiendesha kwa faida.

Ripoti ya CAG kwa mwaka 2023/24 iliyokabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Machi 27, 2025, inaonesha NHIF imeimarika baada ya kupata faida ya Sh. bilioni 75.51 tofauti na ilivyokuwa miaka miwili iliyotangulia ambayo mfuko ulipata hasara ya Sh. bilioni 200.

Mafanikio hayo ya NHIF, kama inavyofafanuliwa na CAG Charles Kichere, yametokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali katika kuimarisha mfuko huo.

Jitihada za serikali kuimarisha NHIF ni hatua zinazostahili pongezi na kupigiwa mfano, kutokana na mabadiliko chanya baada ya miaka mitano ya hasara. Faida ya Sh. bilioni 75.51 inadhihirisha juhudi za kuboresha utendaji na kusimamia vizuri rasilimali za umma, jambo ambalo litasaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi. 

Ni hatua muhimu kwa taifa katika kuhakikisha upatikanaji huduma bora za afya, kwa kuhakikisha kuwa mfuko unajiendesha kwa ufanisi na kuleta tija kwa wanufaika wote.

Hatua hizi pia zinatoa somo la umuhimu wa kufuatilia na kuboresha mifumo ya kifedha, hasa ile inayohusiana na huduma za kijamii kama vile afya. Matokeo haya yanatoa matumaini kuwa masuala ya kifedha yanaweza kushughulikiwa kwa njia ya kimkakati, kwa kuzingatia ufanisi na uwazi, na hivyo kuboresha huduma kwa wananchi.

Pamoja na pongezi hizo, tusisahau kuwa waajiri kutowasilisha kwa wakati michango ya wanachama, serikali kutolipa mabilioni ya shilingi iliyokopa kwenye mfuko, wastaafu kulipiwa matibabu na mfuko bila kuchangia, pamoja na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanaongezeka na kugharimu mfuko mabilioni ya shilingi kila mwaka ndicho kilikuwa kiini cha hasara NHIF. 

Ikumbukwe kuwa Kifungu cha 9 cha Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kinawataka waajiri waliosajiliwa, kuwasilisha michango inayodaiwa kwa mwezi husika ndani ya siku 30 baada ya mwisho wa mwezi. 

Hata hivyo, inaporejewa Ripoti ya CAG kwa mwaka 2022/23, jumla ya michango iliyokuwa inadaiwa hadi kufika tarehe 30 Juni 2023, ilikuwa Sh. bilioni 42.57.

Kati yake, michango ambayo zilikuwa zinadaiwa taasisi za serikali ni Sh. bilioni 19.04 sawa na asilimia 45 na Sh. bilioni 23.53 sawa na asilimia 55 zinajumuisha madeni kutoka kwa mashirika yasiyo ya kiserikali.

Uchambuzi zaidi wa CAG kuhusu hesabu za NHIF ulibaini kuwa, kati ya michango yote ya wanachama inayodaiwa na mfuko huo, michango ya Sh. bilioni 19.6 sawa na asilimia 40 inadaiwa zaidi ya siku 30. Mfuko ulikusanya Sh. bilioni 5.34 ya madeni hadi kufikia mwishoni mwa Novemba 2023 na kuacha deni lililokuwa linadaiwa la Sh. bilioni 11.56. 

Katika hili, Nipashe tunaungana na CAG kupendekeza serikali ihakiki malimbikizo ya michango iliyobaki na kuidhinisha kwa ajili ya malipo, na mfuko uendelee kufuatilia madeni ambayo hayajalipwa na kuhakikisha kiasi chote kinakusanywa.

Nipashe tunatambua pia NHIF inadai fedha kutokana na mikopo ambayo haijalipwa Sh. bilioni 208 (kwa hesabu zilizokaguliwa za mwaka 2022/23). Ni mikopo inayosababisha mzigo mkubwa wa kifedha, na hivyo kupunguza uwezo wa mfuko kuwekeza katika huduma muhimu na miundombinu.

Tunapongeza NHIF kwa kuanza kutengeneza faida, lakini ni muhimu serikali ikarejesha fedha zote ilizochukua katika mfuko ili kutoathiri utoaji huduma kwa wanachama na uendelevu wa mfuko na kuendelea kufuatilia kwa ukaribu utendaji wa mfuo huu kwa maslahi ya umma.