Chonde Iddi tuivuke salama na watoto, vilevile Pasaka!

By Tuntule Swebe , Nipashe
Published at 12:53 PM Apr 01 2025
Sikukuu Iddi.
Picha: Mtandao
Sikukuu Iddi.

JANA kitaifa na leo tunaendelea kuadhimisha sikukuu ya Idd El Fitri, pia ikikaribia sikukuu ya Pasaka, iko wazi kuwa wazazi na walezi ni vema kuwalinda watoto wetu kwa namna mbalimbali.

Tukiwa sahihi, tunapaswa tusikumbwe na mabaya, kwani wakati huu wahalifu wanaweza kutumia fursa ya kuwatenda vibaya watoto, kwani kuna mengi huwa tunasikia. 

Licha ya kuwa katika nyakati hizi watoto wanakuwa na utundu kupita kiasi, hiyo ni kwa sababu ya kufurahi, hivyo wanalazimika kucheza michezo ya hatari.
 
 Hata hivyo, tufahamu kuwapo watoto wanaopendelea kwenda maeneo ya ufukweni mwa bahari, kwa ajili ya kuweza kufurahia sikukuu hiyo.

 Pamoja na wenzao, ingekuwa vyema kama wazazi wangeambatana nao. Bila shaka ndugu zangu Waislamu mnajua wazi siku hii ni siku ya kuwa pamoja na familia zenu, mkipata riziki na kufanya ibada.

 itambulike kuwa siku hii ni ya kufikiri namna ya kuendeleza matendo uliyokuwa ukiyatenda ndani ya kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na hata Wakristo, ifikapo Pasaka mkumbuke matendo ya nyakati za mfungo.

 Napenda maoni ya Imamu mmoja wa Dar es Salaam, akatamka kwamba mtu atakayetenda uovu katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Idd, ana adhabu mbele ya Muumba. 

Kila mtenda mema, amali yake (ziada) ipo kwa Mola wake. Bila shaka, kila anayefikiri kufanya uovu kwenye nyakati hizi na nyinginezo.

Ni vyema tumewekewa maoni ya wazi, kwamba Imani zetu wanatuelekeza kwamba, kila tunatenda uovu kuwa kinyume na maoni mbele za Mungu. 

Hivyo watu wote, kwa pamoja ni wakati wa kufurahia siku hii na sio kuwa na simanzi, licha ya kuwa Kamanda wa Polisi, ametoa tamko juu ya tahadhari na kujikinga, wakati wa kufurahia siku hii.
 
 Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, tulisikia siku chache zimepita, limetoa rai kwa wazazi na walezi kuhakikisha usalama wa watoto wao katika kipindi hiki cha sikukuu kwa kuwaepusha na mazingira hatarishi. 

Ikatajwa mkuu wa polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi mkoa huo, SACP Issa Juma Suleiman, akasisitiza umuhimu wa wazazi kuwa makini, hasa katika maeneo yenye hatari kama baharini na mabwawa.

Mtazamo ni kujiepusha na madhara mengine yanayoweza kutokea, amewataka kuhakikisha watoto wanakuwa chini ya uangalizi wa watu wazima wanaoaminika, badala ya kuwaachia watoto wenzao kuwaongoza katika makundi.
 
 Aidha, amewakumbusha wananchi kuzingatia falsafa ya “Ulinzi Jirani” kwa kuwajulisha majirani zao wanapokuwa safarini, kusaidia kudumisha usalama wa mali na makazi yao. 

Kama hilo, umakini huo pia ni wa hali ya juu, kwani rai hizo ni sambamba na Kanda Maalumu Dar-es Salaam, akawataka wazazi kuwa makini kwa watoto zao. 

Ili kuweza kuwalinda wasipatwe na mabaya hivyo ana wataka endapo watoto wao wanaenda kutembea, waongozane nao ili kuweza kuwalinda watoto.

Licha ya kuwa wataweka ulinzi kwenye fukwe za bahari, lakini wazazi wanatakiwa kushirikiana nao, ili kuweza kuimarisha ulinzi.

Hata hivyo, wale waliojipanga kwa ajili ya uhalifu, wanatakiwa kutambua kuwa polisi ipo kuwakabili usiku na mchana, hivyo watambue kuwa wana jiweka hatiani.

Wazazi wanatakiwa kutoa elimu kwa watoto wao juu ya madhara ya kutembea peke yao katika wakati huu, pia namna ya kujikinga na michezo hatarishi kama vile kuogelea baharini pasipo kuwa na uangalizi. 

Hii inaweza kusababisha vifo na hata kuitwa na kuongozana na watu wasiowajua, kwani kuna uwezekano wa kupotea kwa watoto na kupata shida ya kuwatafuta.