Tusijisahau, tuzingatie ya wataalam, mswaki upigwe kwa njia tulizopewa

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 12:09 PM Apr 08 2025
Tusijisahau, tuzingatie ya wataalam, mswaki upigwe kwa njia tulizopewa
Picha:Mtandao
Tusijisahau, tuzingatie ya wataalam, mswaki upigwe kwa njia tulizopewa

HUENDA ikawa taarifa ngeni kwa baadhi yetu, lakini ndivyo wataalam wa afya ya kinywa na meno wanavyoshauri, kwamba mswaki itumike kwa miezi mitatu tu kisha utupwe, kwa kuwa haifai tena kwa matumizi.

 Pamoja na kuutumia kwa miezi mitatu, wanashauri pia kwamba kila mswaki unapotumika, hubaki na wadudu, hivyo ni muhimu kuuosha kwa maji ya moto kila unapotaka kuutumia tena.
 
 Aidha, wanasema kiusafi haishauriwi kuchemsha mswaki ili kuua wadudu, bali ni kuuosha kwa maji ya moto unapotaka kuutimia na kuuhifadhi mahali salama ambapo ni mbali na choo. 

Kwa nini? Kwa sababu ukihifadhiwa chooni unachukua wadudu wengi ambapo mtu anapoflash choo wadudu husambaa hewani na kukijaza choo kwa hali ambayo wataalam hao wanaiita 'Toilet Plume Effect'.
 
 Vilevile kwa upande wa muda wa matumizi ya mswaki, wataalam hao wanasisitiza kwamba, ili mswaki uwe na viwango vinavyotakiwa, unatakiwa kubadilisha agalau kila baada ya miezi mitatu.
 
 Bila kufanya hivyo, inaelezwa kuwa mtumiaji anaweza kuwa katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya kinywa na meno, na kwamba kwa mwaka mtu anatakiwa kutumia miswaki minne.
 
 Kwa maelezo hayo ya wataalam, nadhani ni wakati sasa wa kubadilika na kufuata njia sahihi ya matumizi ya mswaki, kwa sababu ninaamini kwamba taarifa hii inaweza kuwa ngeni kwa wengi wetu. 
 
 Ikumbukwe kuwa taarifa inapokuwa ngeni, mara nyingi watu huwa ni wazito kuiamini. Lakini kwa sababu ya wataalam wa afya, hatuna budi kukubaliana nayo kwa ajili ya usalama wa afya ya kinywa na meno yetu.
 
 Kimsingi, watu tunatakiwa kubadilika, kwani inaelezwa kuwa kama mtu ataendelea kutumia mswaki ambao tayari umeshakuwa mgumu na nyuzi zake zimeanza kutoka unakuwa anaumiza fizi na meno.
 
 Utumiaji wa mswaki wa aina hiyo, inaelezwa kuwa linasugulika tabaka la juu linalolinda hizi, hivyo linabaki wazi na litatoboka na kusabaabisha mtumiaji kupata maumivu na magonjwa ya kinywa na meno.
 
 Pia, tunakumbusha kuwa kuna madhara kwa afya ya kinywa na meno pale tunapotumia majivu, mkaa, karafuu, sabuni, chumvi na njia zingine zisizo za kitaalamu wakati wa kupiga mswaki.
 
 Katika hilo, tunasisitizwa kwamba njia sahihi ya kutunza meno na kinywa ni kutumia dawa ya meno ambayo ina madini ya floraidi, si vinginevyo waliovyozoea baadhi ya watu.
 
 Taarifa zaidi ni kwamba, mtu anatakiwa kutumia mswaki wenye brashi laini na dawa yenye floride. Wakati wa kupiga mswaki anatakiwa atumie dakika mbili baada ya hapo anatema povu na asiweke maji mdomoni.
 
 Kwa nini? Kwa sababu inaelezwa kitaalam kuwa mtu anapopiga mswaki na kuweka maji mdomoni, kusukutua na kutema, unakuwa umetoa dawa ambayo ilikuwa ni muhimu kuzuia meno kuoza.
 
 Mbali na hayo yote, wataalam wa afya wanabainisha kuwa kwa sasa  dawa ya jino sio kung’oa bali ni kufanya matibabu sahihi kulingana na tatizo na kwamba mtu anaweza kuziba jino au kukata mzizi wa jino na hatua mwisho kabisa ni kung’oa iwapo itashindikana.
 
 Hivyo ni wazi kwamba, kuna haja ya kutunza afya ya kinywa na meno kwa kuzingatia maelekezo ya wataalam ili kuendelea kuwa salama zaidi badala ya kufanya kienyeji na kujikuta katika changamoto.
 
 Pamoja na hayo, watu wazima tunashauriwa kupiga mswaki hata mara mbili kwa siku, kuepuka matumizi ya pombe na tumbaku ili kukwepa kukumbwa na saratani ya kinywa. Ninaamini hayo yanawezekana iwapo kila mmoja wetu atazingatia ushauri huo wa wataalam wa afya.