Tuanze elimu kwanza kwa waendao shamba na watoto bila hata ya uji

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 03:54 PM Apr 04 2025
Shamba.
Picha: Mtandao
Shamba.

KUNA simulizi hii, tabia iliyojengeka mkoani Njombe, baadhi ya kinamama wanaodamka alfajiri mapema kwenda shambani, wakiwa wamebeba watoto mgongoni bila kuwachukulia chakula.

 Wanawake hao wanashindwa kuwachukulia watoto uji, huku wakitegemea viazi ambavyo watachimba shambani ndivyo hivyo hivyo watoto wao wale.

Umma tumedokezwa hilo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Erasto Mpete, katika siku ya Afya na Lishe yaliyofanyika Utalingolo, Halmashauri ya Mji wa Njombe.

 Mwenyekiti huyo ameenda mbali zaidi akisema, wanawake wenye tabia hiyo wanapaswa kuchukuliwa hatua, kwani itasaidia kupunguza matatizo ya kiafya kwa watoto wao.

 "Unakwenda shambani kuchimba viazi kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi jioni unampikia mtoto wako saa ngapi? Watoto ni wenu, hakuna mwingine wa kuwalea zaidi ya wazazi wenyewe,

 “ Tukiwajali watoto tutakuwa na kizazi chenya afya. Niombe viongozi wa jiji shughulikieni wale ambao hawazingatii mahitaji ya lishe kwa watoto wao," akasema mwenyekiti huyo.

 Akawaagiza viongozi wa vijiji kuanzisha sheria ndogo za kudhibiti tabia ya baadhi ya kinamama wanaokwenda kuchimba viazi alfajiri bila kubeba chakula chenye virutubisho kwa watoto, ikiwamo uji.

 Binafsi nimpongeze sana mwenyekiti huyo kwa kuonyesha kujali kama mzazi, huku wazazi wenyewe wakishindwa kufanya hivyo kwa watoto wao.

 Inashangaza kuona kwa nini kinamama hao wanashindwa kuwapikia uji watoto zao, ili wanapodamka alfajiri kwenda nao shambani au huko anakokwenda kuchimba viazi?

 Inawezekana kinamama wengi wa Njombe, bado hawajapata elimu ya lishe hasa kwa watoto wao, na hili ndilo linalosumbua wengi, siyo mkoani humo tu, bali maeneo mengi ya nchi, hasa vijijini.

 Ndiyo maana utaona baadhi ya wanawake wa huko, wanawalisha vyakula vigumu watoto wenye umri mdogo asuhuhi tu wanapoamka. 

Mtoto analishwa kiporo ambacho wakati mwingine hata hakijapashwa moto, siyo kama hawawapendi watoto zao, bali ni ukosefu wa elimu.

 Nimeona hapo, mwenyekiti anataka hatua kali zichukuliwa juu yao, lakini kwangu mimi naona kabla ya kuchukua hatua zozote, inapaswa wakusanywe kinamama wa hamlashauri hiyo na wapigwe msasa wa elimu, kuwepo na utekelezaji wa kuchukuliwa hatua moja kwa moja. 

Iwapo watakutwa bado tatizo tatizo litakuwa halijatatulika, badala yake wanawake wataona ni kama wanaonewa na kunyanyaswa. 

Hata waume zao nao hawatokubali hilo, kuona eti wake zao wanakamatwa na kwenda kulazwa selo, au kulipishwa faini kwa sababu ambazo hazijulikani vyema.

 Kinachotakiwa ni elimu itolewe kwa muda wa miezi kadhaa kuhusu kuwajali watoto, kuwapikia uji na kwenda nao shambani, wakitaja na faida zake, pamoja na hasara za kutofanya hivyo. 

Unampomtajia mama faida ya afya atakayopata mtoto wake kama akienda shambani uji, halafu madhara atakayopata na kwa mifano, sidhani kama wanaweza kuendelea kufanya hivyo.

 Nadhani hilo kwanza lingetangulia kabla ya lingine ambalo linaweza kutumiwa na watu ambao si waaminifu wanaotumiwa na viongozi wa vijiji, kunyanyasa wanawake. 

Na hili ninalosema la elimu kwa kinamama kwenda shamba na chakula kwa watoto lisiwe kwa Mjombe tu, bali Tanzania nzima, ili kupata kizazi chenye afya njema, na nchi yenye watu wenye afya na siha nzuri.