Kuna mtu nyuma ya waandamaji Yanga

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 01:03 PM Mar 31 2025
 Ligi Kuu Tanzania Bara
Picha:Mtandao
Ligi Kuu Tanzania Bara

SERIKALI ina juhudi za makusudi kusuluhisha tatizo lililojitokeza baada ya kutochezwa kwa mechi ya dabi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kati ya Simba dhidi na Yanga, Machi 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Baada ya malumbano ya hapa na pale kati ya Yanga, Shirikisho la Mpira wa Miguu na Bodi ya Ligi, serikali, kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, inayoongozwa na Profesa Palamagamba Kabudi, iliita pande zote, ikiwemo klabu ya Simba ambayo baada ya taarifa ya kwanza ambayo waliipeleka Bodi ya Ligi kuhusu kukataliwa kuutumia Uwanja wa Benjamin Mpaka siku moja kabla ya mchezo, ikisema kutokana na kukiukwa kwa kanuni isingekanyanga uwanjani, haikutoa taarifa wala kuzungumza chochote kuhusu jambo hilo.

Baada ya Bodi ya Ligi kuahirisha mchezo, ndipo Yanga ilipotoa taarifa mbalimbali, ikiwemo kutaka viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), na Bodi ya Ligi wajiuzulu.

Matamko ya kila kukicha ya wazee na watu wengine yakalazimisha serikali iingilie kati.

Nimpongeze Waziri Kabudi na wenzake kwa kufanya kazi kubwa ambayo ilizikutanisha pande zote, ingawa bado yaliyozungumzwa yamekuwa siri, lakini bado yanasubiriwa kwa hamu.

Lakini kwa sababu jambo hilo ni la serikali, basi tunajua hakuna chochote kitakachoharibika.

Chochote kitakachoamriwa ni kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa Tanzania, usalama na amani ya nchi kwa ujumla.

Nje ya Uwanja wa Benjamin Mkapa ambako kuna ofisi za Wizara hiyo, kulikuwa na kundi la mashabiki waliovalia jezi za Yanga ambao walionekana kuimba na kucheza wakidai hawataki mechi ya dabi irudiwe.

Bila woga wowote, mashabiki hao walionyesha kujiamini na kama walivyotarajia wenyewe, hawakuguswa na mtu yoyote hadi viongozi wa timu zote walipotoka nje.

Cha ajabu ni kwamba baadhi yao walikuwa na fulana zilizochapishwa neno, 'Hatuchezi' wakisisitiza msimamo wao wa kutoingiza timu kwa tarehe nyingine itakayotajwa na bodi ya ligi.

Kilichonishangaza mimi na kujiuliza maswali ni je, mashabiki au wanachama hao hawawamini viongozi wao?.

Ninavyojua, wananchi, taasisi au jumuiya yoyote ile ikishampata kiongozi au viongozi wao wanawapa mwongozo wa nini cha kufanya.

Kila kinachoamriwa na viongozi kinatokana na mawazo ya watu hao. Lakini pia viongozi huweza kubadilika kutokana na mazingira yaliyopo, na kwa sababu wamepewa dhamana na wanaowaongoza inakuwa sawa tu kwa mazingira husika.

Ndiyo maana si kila mmoja anaweza kuwa kiongozi. Wakati mwingine unatakiwa utumie busara, ushawishi, karama, hekima kulingana na wakati husika katika kuongoza.

Sikuona umuhimu wa mashabiki wale kukaa pale, kuimba kupiga kelele kwenye ofisi za watu.

Inaonekana kwamba hawawamini viongozi wao, kwa hiyo wanakwenda kuwakumbusha kuwa wasikubali kucheza tena mchezo huo.

Nadhani wangefanya kama wa Simba ambao wao wamewaachia kila kitu viongozi wao, wataamua kwa manufaa yao na klabu, hata haikuwa na haja na kutaka kujazana, kuimba na kucheza kwenye ofisi za wizara. Ni ukosefu wa heshima na adabu.

Kingine ninachojiuliza ni nani aligharamia kuchapishwa kwa fulana zenye maandishi yale?.

Kwa akili yangu tu ya kawaida, sioni kama wao wenyewe wamefanya hivyo. Kuna watu wamegharamia. Hao watu watakuwa ndani ya klabu hiyo ya Yanga. 

Wakati viongozi wengine wanakwenda kutafuta muafaka, wengine wanashikilia msimamo wa 'hatuchezi' kwa kukusanya watu kwenye ofisi za watu.

Kitendo kile kilikuwa kinamaanisha kuwa waliowaita, na hao wanaokwenda kusuluhishwa wote hawana maana, hakuna ulazima wa serikali kusuluhisha jambo hilo, badala yake lifanyike lile tu ambalo wanalihitaji.

Niseme tu kuna mtu nyuma ya pazia kwenye sakata la wale waandamaji. Huyu anawazunguka wenzake wenye nia nzuri ya majadiliano. Niisihi Wizara chini ya Kabudi, isikatishwe tamaa, iendelee kusaka muafaka thabiti wa sakata hili.