Iithaminiwe analonena Mkuu Maktaba wenye sifa ndio watumikie fani hiyo

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 10:53 AM Apr 03 2025
Maktaba Tanzania.
Picha: Mtandao
Maktaba Tanzania.

TAARIFA ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) Dk. Mboni Ruzegea, kuhusu uwapo wa baadhi ya shule na vyuo vinavyotumia walimu kutoa huduma kwenye maktaba za taasisi hizo husika, inapaswa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Dk. Ruzegea ametamka hayo hivi karibuni  jijini Dar es Salaam, wakati alipokuwa akitoa taarifa ya mafanikio ya miaka minne ya bodi hiyo, chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania ni taasisi ya umma chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge ya mwaka 1963 na kufanyiwa marekebisho mwaka 1975, huku mtendaji wake mkuu wa sasa ni mtaaluma mwandamizi wa fano hiyo . 

Majukumu ya msingi ya bodi ni pamoja na kuanzisha, kuendeleza na kuratibu huduma za maktaba nchini, ikihifadhi machapisho ya kitaifa na kusambaza maarifa kwa jamii bila ubaguzi.  

Nadhani  hii ni taarifa muhimu inayolenga kuona kwamba kila taaluma inatumika mahali pake sahihi, kwa kufanya hivyo, wanataaluma husika nao wanajipatia ajira, hivyo kuwa na kipato lakini pia inakuza taaluma.  

Katika taarifa hiyo ya Bodi TLSB imeitaka serikali kuajiri wakutubi waliobobea katika taaluma hiyo ili kuwapunguzia walimu mzigo wa kazi, pia kuongeza ubora wa huduma katika maktaba za shule na jamii.  

Pia, bodi hiyo ikashauri shule ama vyuo vinavyotumia walimu kama wakutubi  kuhakikisha  wanapelekwa kupata mafunzo ya muda mfupi, ili kuwajengea uwezo wa kitaaluma, kwa kuwa wengi wao hawajasomea taaluma ya ukutubi.  

Dk.Ruzegea akasema bodi inatambua juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuinua sekta ya elimu na maarifa. Chini ya kauli mbiu ya “Kazi Iendelee”, hivyo itaendelea kuimarisha huduma za maktaba kwa maendeleo mapana ya taifa.   

Naona matarajio ya bodi hiyo ya kupunguza pengo la maarifa kwa kupitia maktaba za shule na za jamii na matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma, ni mbegu njema ambayo inapaswa kupandwa kwenye shamba bora ili kuvuna 'mazao' bora.  

Kwa kutambua kwamba kuna mabadiliko ya kiteknolojia bodi hiyo pia inatarajia kuboresha TEHAMA kwa maktaba zilizobaki, kupanua huduma za usomaji hadi vijijini, kuwezesha upatikanaji vifaa vya elimu na mafunzo ndani ya maktaba zote nchini na kuimarisha huduma jumuishi na endelevu kwa jamii nzima.  

Ni wazi TLSB kwa kutambua wajibu wao inatamani kuhakikisha maktaba zinakuwa za kisasa kulingana na uwapo wa teknolokijia, malengo hayo yanaweza kufanikiwa kwa kiwango kilochokusidiwa iwapo mahali ambapo alipaswa kuwepo mkutubi yupo mwalimu.  

Kama ambavyo mkutubi hapaswi kuajiriwa kama Mwalimu, kwa kuwa hajasomea, ndivyo inavyopaswa kuwa kwenye taaluma zote zinapaswa kuheshimiwa maana zina umuhimu katika sektq husika.  

Kuna mafanikio ambayo taasisi hiyo ya maktaba imebainisha kuyapata, ikiwamo kuwahudumia watumiaji 2,157,622 katika maktaba za umma nchini, kwa wastani, hii ni sawa na watumiaji 539,406 kwa mwaka, pia inatarajia kuongeza watumiaji hadi kufikia milioni 10 ifikapo mwaka 2030.  

Mapato ya ndani yameongezeka kutoka Sh.1.5 bilioni mwaka 2021/22 hadi 1.92 bilioni mwaka 2024/25 – ongezeko la asilimia 28 kwa ujumla, au CAGR ya asilimia 6.37 kwa mwaka.  

Ni vyema serikali hasa Ofisi ya Menejmenti ya Utumishi wa Umma, kuwasha tochi kuchunguza taasisi zake zote kama zina waajiriwa wenye sifa kwenye ofisini husika. Ili kila mwanataaluma aliyepata nafasi sahihi aone umuhimu wakuiheshimisha taaluma yake  kwa kuwajibika ipasavyo, kulingana na alichojifunza.