Tumeiona dabi ya majirani, sasa tunasubiri ya Kariakoo

Nipashe
Published at 01:00 PM Mar 31 2025
Tumeiona dabi ya majirani,  sasa tunasubiri ya Kariakoo
Picha:Mtandao
Tumeiona dabi ya majirani, sasa tunasubiri ya Kariakoo

JANA ilichezwa mechi kubwa zaidi kwa majirani zetu Kenya kwa kuzikutanisha timu za Gol Mahia na AFC Leopards katika mchezo wa dabi, maarufu kama 'mashemeji dabi'.

Mchezo huo uliojaza maelfu ya mashabiki kwenye uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, awali uliahirishwa zaidi ya mara moja lakini jana ukafanyika na mashabiki wakaitika hasa uwanjani.

Wakati wakenya  wakipata burudani ya soka kupitia mchezo huo wenye upinzani mkubwa kama wa Simba na Yanga hapa nyumbani, Bodi ya Ligi bado haijatangaza hatma ya mchezo wa dabi ulioahirishwa.

Ni zaidi ya wiki mbili sasa tangu mchezo wa dabi ya kariakoo baina ya Yanga na Simba uliopohairishwa na Bodi ya Ligi baada ya kutokea sintofahamu siku moja kabla ya mchezo Machi 7.

Baada ya kuharishwa kwa mchezo huo kulianza kutokea mvutano kati ya Bodi ya Ligi na klabu ya Yanga huku wenyeji wa mchezo huo, Yanga wakitoa kauli ya kutokuwa tayari kucheza tena mchezo huo kwa tarehe itakayotajwa tena na bodi ya ligi.

Baada ya mvutano huo ambao ulichagizwa zaidi ya baada ya bodi ya ligi kusisitiza kuwa mchezo huo uliokuwa uchezwe Machi 8, utapangiwa tarehe mpya.

Hivi majuzi, Serikali kupitia kwa Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paramagamba Kabudi ilikutana na pande tatu tofauti kwa maana ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF), uongozi wa klabu za Simba na Yanga kujadili masuala mbalimbali huku mchezo huo nao ukiwa sehemu ya ajenda.

Kikao hicho kilichochukua siku nzima kilimalizika bila ya kuwapo kwa taarifa kamili ya kule kilichojadiliwa na maamuzi yake.

Hata hivyo, Rais wa klabu ya Yanga akizungumza mara baada ya kutoka kwenye kikao hicho, aliwataka wanayanga kuwa watulivu na viongozi wao watasimamia haki zote za klabu hiyo.

Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Murtaza Mangungu yeye alinukuliwa akisema kwenye kikao chao hawakuzungumzia kabisa suala la mchezo huo lakini walijadili maendeleo ya michezo hapa nchini hususani mpira wa miguu.

Kifupi kuhusu mchezo wa dabi kurudiwa ama kutorudiwa imebaki kuwa jambo linalosubiriwa na wadau wengi wa mpira kutaka kuona nini kitaamuliwa hasa baada ya Yanga kusisitiza mara kwa mara kupitia viongozi wao kuwa hawatacheza mchezo huo.

Pande zinazohusika zinatakiwa kukaa pamoja na kutoa majibu ya suala hilo ili mashabiki na wadau wa soka wafahamu nini hatma ya mchezo huo mkubwa hapa nchini.

Nipashe tunafahamu klabu za Simba na Yanga ni klabu kubwa na zenye ushawishi mkubwa kwenye ligi yetu inayotajwa kushika nafasi ya nne Afrika.

Sio mbaya kuiga kile kilichotokea Kenya jana, baada ya mvutano wa mchezo wa dabi ya mashemeji, hatimaye mchezo huo umechezwa jana huku kukiwa na mashabiki walioujaza uwanja.

Viongozi wote wanapaswa kutambua maamuzi sahihi yenye tija kwa soka letu yanatakiwa kuliko mapenzi binafsi au ukibuli wa aina yoyote.

Ligi yetu ilipofika sasa ilipofikia sasa inatazamwa na kufuatiliwa na nchi nyingi kutokana na umaarufu na ukubwa wa klabu hizi za Simba na Yanga.

Dabi ya Kariakoo inatajwa kuwa miongoni mwa dabi kubwa Afrika kama zilivyo zile za Misri ( Al Ahly na Zamareki) au Afrika Kusini ( Kaizer Chief na Orlando Pirates) hatupaswi kuichafua.

Kwa kuwa vikao vitaendelea kufanyika, tunaomba kwenye ajenda ya mchezo huu wa dabi kurudiwa, busara zadi itumike na kuacha kutunishiana vifua kujua nani mwenye nguvu.

Kitu pekee ambacho wadau wa soka wanakitaka ni maendeleo ya mpira wetu yazidi kuonekana na kushamiri na kuacha kudidimiza maendeleo hayo ambayo yamejengwa kwa nguvu kubwa.

Tunaamini kwenye wengi hakuna kitakachoharibika, vikao hivi vilivyoanza juzi na kutolewa kauli kwamba vitaendelea kufanyika, vitoke na majibu sahihi na kurudisha ushirikiano wa wadau wote, maamuzi yawe ya busara na yenye kuleta tija kwenye soka letu. Watu wanasubiri kuiona dabi ya Kariakoo.