MWAKA huu, Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi wa sita utakaohusisha vyama vingi ambao utahusisha watu kujitokeza na kugombea nafasi mbalimbali kuanzia uraisi, udiwani na ubunge kwa Tanzania Bara. Kwa upande wa Zanzibar, uchaguzi huo utahusisha pia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Masheha.
Uchaguzi huo ambao hufanyika kwa misingi ya kidemokrasia, hutoa nafasi kwa vyama kushindana kwa hoja kuonyesha vitafanya nini pindi vitakapopewa ridhaa na wananchi kuongoza dola. Kwa mantiki hiyo, hoja zitawashawishi wananchi kuchagua chama kipi ili kuwaondolewa kero zinazowakabili.
Kabla ya kufikia hatua hiyo ya kila chama kuteua wagombea kwa nafasi husika kusimama katika uchaguzi, vyama huteua wanachama kwa ajili ya kugombea nafasi hizo baada ya kuwapo kwa mchuano baina ya wanachama. Kwa mantiki hiyo, wanachama hushindanishwa ili kupata watu watakaopeperusha bendera ya chama katika nafasi husika.
Kutonaka na kuwapo kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu mwaka huu, vyama vimeanza kujipanga kuona ni wanachama wapi wanaofaa kugombea nafasi hizo katika ngazi mbalimbali ili kuletea chama husika ushindi na hatimaye kutekeleza yale yaliyoahidiwa kupitia ilani zao.
Kama ilivyo ada unapokaribia uchaguzi, wanachama na makada wa vyama huanza kuonesha nia ya kuwania nafasi mbalimbali kwa kutangaza nia au kupita katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kujaribu kufanya ushawishi kutoka kwa wanachama ili kukubalika. Wengi kati ya makada hao, ni wale wanaowania ubunge na udiwani ambao hupita na kutengeneza mazingira ya kukubaliwa.
Katika nafasi ya urais, kuna mifumo ambayo umeweka katika vyama kuhusu ni nani anayeweza kupitishwa kuwa mgombea. Ndani ya CCM, kwa mfano mchakato wa kuwapitisha wagombea urais na wagombea wenza katika uchaguzi ujao umekamilika, Rais Samia Suluhu Hassan ameteuliwa kuwa mgombea wa urais kwa Tanzania na Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza. Kwa Zanzibar, Dk. Hussin Ali mwinyi ameteuliwa kugombea tena nafasi hiyo kwa mara ya pili.
Wakati CCM ikiwa imefanya hivyo, vyama vingine havijaanza mchakato wa kuweka wagombea wa nafasi ya urais huku vingine vikibainisha kuwa havitashiriki kama mabadiliko ya sheria za uchaguzi hayatafanyika. Pamoja na msimamo huo, baadhi ya wanachama wameonesha nia ya kugombea huku wakionesha kupingana na msimamo wa chama kuhusu kugombea uchaguzi.
Kwa ujumla, Tanzania inaongozwa kwa misingi ya uhuru na demokrasia katika kupata wagombea wa nafasi mbalimbali kama urais, ubunge, udiwani, uwakilishi na masheha. Kwa mantiki hiyo, kila mwanachama anayeona ana sifa, anaruhusiwa kugombea kwa kuchukua fomu na kufuata taratibu zote hadi vikao vya mchujo vitakapofanyika. Pamoja na hayo, katika baadhi ya vyama kumekuwa na vitisho dhidi ya wale wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali, ikiwamo ya urais.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mathalan, kimekuwa kikijinadi kuwa hakitashiriki uchaguzi mkuu kwa madai kuwa kama hakutakuwa na mabadiliko hakiwezi kushiriki mchakato huo kupitia kaulimbiu yake kuwa ‘no reform no election (hakuna mabadiilko hakuna uchaguzi).
Pamoja na msimamo huo, kuna mwanachama wa chama hicho, Romanus Mapunda, ametangaza kugombea urais na kuweka wazi kwamba hakubaliani na msimamo wa chama chake kutokushiriki uchaguzi. Kutokana na msimamo huo, Mapunda ameandikiwa barua na chama chake kufika mbele ya Kamati Tendaji ya Tawi la Mtongani kujieleza kwa kile kilichodaiwa kuwa mwenendo wake usioridhisha ndani ya chama.
Katika misingi ya kidemokrasia, kila mwanachama wa chama cha siasa, ana uhuru wa kutumia nafasi yake kugombea nafasi yoyote ya uongozi ili mradi ana sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi na ya chama chake.
Kutokana na ukweli huo, hakuna wenye haki wana hati miliki ndani ya chama kuliko wengine, hivyo misingi ya haki na demokrasia iinapaswa kuzingatiwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED