CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimepitisha mabadiliko ya Katiba yake ya mwaka 1977 Toleo la Mei, 2025, kwa kura 1,912 zilizopigwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum ulifanyika jana kwa njia ya matandao, sawa na asilimia 99.8.
Aidha, mkutano huo umebadili Katiba kwa kuongezea idadi ya majina yatakayopitishwa kutoka matatu na kuwa kwa kadri Kamati Kuu ya CCM itakavyoona inafaa.
Mabadiliko yaliyofanywa na mkutano huo ni Ibara ya 105 Ibara Ndogo ya 7 (f) inayoelekeza Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kufikiria na kuteua majina ya wagombea wa CCM matatu kwa kila jimbo la uchaguzi walioomba nafasi za ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi ili wakapigiwe kura za maoni.
Kwa upande wa madiwani mabadiliko yaliyofanyika ni Ibara ya 91 Ibara Ndogo ya 6 (c) ya Katiba ya Chama hicho.
Ambapo, Kamati ya Siasa ya Halmashauri ya CCM Taifa ya Mkoa imepewa mamlaka ya uteuzi wa majina yasiyozidi matatu ya wanachama wanaogombea nafasi ya udiwani kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni kwenye Kata.
Akisoma matokeo ya kura zilizopigwa na wajumbe Spika wa Baraza wa Wawakilishi Zanibar, Zubeir Ali Maulid, alisema idadi ya wajumbe wa mkutano huo walikuwa 1,931 na waliopiga kura ni 1,915.
“Kama nilivyoelezwa hapo awali, jumla ya wajumbe wote wa mkutano huu ni 1,931, waliopiga kura ni 1,915 wasiopiga kura ni 16, na kura zilizoharibika ni tatu na hapana hakuna, hivyo kura za ndiyo ni 1,912 sawa na asilimia 99.8,” alisema Maulid.
Awali, akiwasilisha mapendekezo ya mabadiliko madogo ya Katiba ya Chama hicho kwa wajumbe wa Mkutano Maalum Katibu wa NEC, Idara ya Oganaizesheni CCM, Taifa, Issa Gavu, alisema mkutano huo ndio mwenye mamlaka kufanya mabadiliko hayo.
“Mheshimiwa Mwenyekiti kwa niaba ya Halmashauri Kuu ya Taifa ninapenda kuwasilisha mbele ya Mkutano Mkuu wa Taifa mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ya CCM ya Mwaka 1977, Toleo la Mei, 2025,”alisema.
Alisema mapendekezo hayo ya mabadiliko ya Katiba ya chama yanafanywa kwa mujibu wa Ibara ya Katiba ya CCM Ibara ya 101 inayozungumzia kazi za mkutano mkuu wa taifa.
Gavu alisema katika majukumu yake chini ya Ibara ya 101 Ibara Ndogo ya 4, Mkutano Mkuu wa CCM, Taifa una mamlaka ya kubadili sehemu yoyote ya Katiba kwa uamuzi wa theluthi mbili ya wajumbe walio na haki ya kupiga kura Tanzania Bara na theluthi mbili ya kutoka Zanzibar.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo kwa mujibu wa Ibara ya 105 Ibara Ndogo ya Saba 7(f) ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi, Toleo la Mei, Kamati Kuu ya CCM, Taifa, imepewa mamlaka ya kufanya uteuzi wa awali wa majina yasiyozidi matatu ya wanachama wanaogombea nafasi ya ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi ili waende wakapigiwe kura za maoni.
“Kwa upande wa madiwani mheshimiwa Mwenyekiti kwa mujibu wa Ibara ya 91 Ibara Ndogo ya 6 (c) ya Katiba ya CCM, Toleo la Mei, Kamati ya Siasa ya Halmashauri ya CCM Taifa ya Mkoa imepewa mamlaka ya uteuzi wa majina yasiyozidi matatu ya wanachama wanaogombea nafasi ya udiwani kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni kwenye kata,” alisema.
Alisema Kamati Kuu ya CCM Taifa kwa mazingira maalum yanayopelekea kusudio la kuleta majina zaidi ya matatu kwa wagombea ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, chama kinalazima kufanya mabadiliko madogo ya katiba kwenye ibara zinazaohusika.
Gavu alisema mkutano mkuu ndiyo utakuwa mahususi kwa ajili ya kufanya marekebisho ya katiba kwenye Ibara 105 Ibara Ndogo ya 7 (F) pamoja na Ibara ya 91 6 (c) ya Katiba ya CCM, Toleo la Mei, 2025.
“Kwa sasa Mheshimiwa Mwenyekiti ibara hizo zinasomeka kama ifuatavyo, Ibara ya 105 Ibara Ndogo ya 7 (f) inasema kufikilia na kuteua majina ya wagombea wa CCM matatu kwa kila jimbo la uchaguzi walioomba nafasi za ubunge na ujumbe wa baraza la wawakilishi ili wakapigiwe kura za maoni.
“Kwa Ibara 91 6 (c) kwa upande wa madiwani inasomeka kuwa Kamati ya Halamshauri Kuu ya CCM, itafikiria majina ya wana CCM wasiozidi watatu kwa kila kata waliomba kugombea udiwani, ili wakapigiwe kura za maoni baada ya kura za maoni, itatoa mapendezo na ushauri wake kwa mujibu wa sheria za uchaguzi,”alisema.
Kutokana na hali hiyo, Gavu alisema inapendekezwa kufanyiwa mabadiliko ya Ibara ya 105 Ibara Ndogo ya saba (f) kwa kuongeza maneno isipokuwa kama Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya CCM, Taifa itaamua vinginevyo.
“Hivyo Ibara 105 Ibara Ndogo ya saba (f) ya CCM inapendekezwa isomeke kama ifuatavyo, kufikiria na kuteua majina ya wana CCM wasiozidi watatu kwa kila jimbo la uchaguzi walioomba nafasi ya ubunge.
“Na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi ili wakapigiwe kura za maoni isipokuwa kama Kamati Kuu na Halmshauri Kuu ya CCM taifa, itaamua vinginevyo,”alisema.
Vilevile, alisema kwa upande wa udiwani inapendekezwa kufanya marekebisho kwenye Ibara ya 91 6 (c) kwa kuongeza maneno isipokuwa Kamati Kuu na Halmasaku Kuu ya CCM, Taifa itaamua vinginevyo.
“Hivyo mheshimiwa Mwenyekiti mapendekezo yatakavyosomeka ni kwamba, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, itafikiria na kuteua majina ya wana CCM, wasiozidi watatu kwa kila kata waliomba kugombea udiwani, ili wakapigiwe kura za maoni isipokuwa kama Kamati Kuu na Halmashauli Kuu ya CCM, Taifa itaamua vinginevyo,” alisema.
KAULI YA MWENYEKITI
Mara baada ya kutangwa kwa matokeo, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan, alisema kufanyika kwa madiliko hayo madogo kunawapa fursa ya kuanza mchujo wa majina ya watiania kwa nafasi za ubunge na udiwani kuanzia leo.
“Ndugu wajumbe kazi iliyotukutanisha leo (jana) imeisha ninawashukuru sana kupitishwa mabadiliko haya ya Katiba, Mmetusaidia kuanza kazi ya mchujo wa majina ya watiania kuanzia kesho (leo).
“Lengo letu ni kuongeza majina kutoka matatu kuendelea ili kutoa nafasi kwa vijana wengi wenye nia ya kutaka kugombea na kuliongoza taifa hili,” alisema.
Mwenyekiti Samia alisema majimbo mengi idadi ya watiania imekuwa kubwa, hivyo mabadiliko hayo ya katiba yanakwenda kusaidia idadi ya watiania watakaoteuliwa kwenda kupigiwa kura za maoni kuongezeka tofauti na ilivyokuwa awali.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama hicho (CC) itakaa kikao chake cha mwisho cha kutoa majina ya wagombea kesho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED