Uamuzi mgumu ni Oktoba 29

By Augusta Njoji , Nipashe Jumapili
Published at 12:39 PM Jul 27 2025
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji (Rufani), Jacobs Mwambegele
Picha: Ibrahim Joseph
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji (Rufani), Jacobs Mwambegele

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imepuliza kipyenga cha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu, huku wadau wakihimiza kudumisha amani kwa kufanya kampeni za kistaarabu.

Kadhalika, INEC imesema imekabidhi kwa Jeshi la Polisi orodha ya wapiga kura 8,703 ambao wamebainika kujiandikisha zaidi ya mara moja, ili liendelee na hatua za kisheria.

Akizungumza jana katika uzinduzi wa ratiba ya uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji (Rufani), Jacobs Mwambegele, alisema Agosti 9 hadi 27, mwaka huu, itakuwa ni utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais.

“Agosti 14 hadi 27, mwaka huu, itakuwa utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea ubunge na udiwani, Agosti 27, mwaka huu, itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais, uteuzi wa wagombea ubunge na uteuzi wa wagombea udiwani,” alisema.

Alisema Agosti 28 hadi Oktoba, 28, mwaka huu, zitafanyika kampeni za uchaguzi kwa Tanzania Bara, huku upande wa Zanzibar zitakoma Oktoba 27, mwaka huu, ili kupisha kura ya mapema.

“Oktoba 28, mwaka huu, siku ya Jumatano itakuwa kwa ajili ya upigaji kura. Tume inatoa wito kwa wadau wote ikiwa ni pamoja na wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na maelekezo yatakayotolewa na Tume,” alisema.

Pamoja na hayo, alisema Tume imekamilisha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa awamu mbili na uchakataji wa taarifa za uboreshaji wa daftari hilo.

Alisema wapiga kura wapya 7,641,592 wameandikishwa katika daftari, sawa na asilimia 136.79 ya makadirio ya awali ya 5,586,433 ambayo ni sawa na asilimia 18.77 ya wapiga kura wote walioandikishwa katika uboreshaji wa 2019/20.

“Jumla ya wapiga kura 4,291,699 wameboresha taarifa zao, sawa na asilimia 98.23 ya makadirio ya awali ya 4,369,531 ambayo ni sawa na asilimia 15 ya wapiga kura walioandikishwa 2019/20,” alisema.

Pia alisema wapiga kura 99,744 wameondolewa katika Daftari kwa kupoteza sifa, sawa na asilimia 16.78 ya makadirio ya awali ya 594,494 ambayo ni sawa na asilimia 1.9 ya walioandikishwa 2019/20.

Kadhalika, alisema kwa mujibu wa kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, uandikishaji wa wapiga kura kwa upande wa Tanzania Zanzibar kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na Wabunge, unazingatia sheria inayohusu uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

“Hivyo, kwa mujibu kifungu cha sheria tajwa, idadi ya wapiga kura 725,876 waliko kwenye Daftari la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), ni sehemu ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litakalotumiwa na INEC kwa ajili ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Wabunge kutoka Zanzibar,” alisema.

Alisema kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Na. 4 ya Mwaka 2024, kimeweka utaratibu kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kulifunga Daftari la Wapiga Kura siku saba baada ya uteuzi wa wagombea wa uchaguzi na kwamba, kwasasa Tume ya Zanzibar bado inaendelea na uchakataji wa Daftari kwa mujibu wa sheria na iwapo takwimu zitabadilika wadau watajulishwa.

MILIONI 37 KUPIGA KURA 

Alisema wapiga kura 37,655,559 wamejiandikisha kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka huu.

“Idadi hii ni sawa na ongezeko la asilimia 26.55 kutoka idadi ya wapiga kura 29,754,699 waliokuwa kwenye Daftari, mwaka 2020. Kwa upande wa Zanzibar, wapiga kura 725,876 wapo katika Daftari la ZEC na wapiga kura 278,751 wameandikishwa na INEC kwa kuwa hawakuwa na sifa za kuandikishwa na ZEC,” alisema.

Alifafanua kuwa kati ya idadi hiyo ya wapiga kura 37,655,559, wapiga kura 1,004,627 wapo Tanzania Zanzibar.

“Kati ya wapiga kura hao, 18,943,455 ni wanawake sawa na asilimia 50.31 na wapiga kura 18,712,104 ni wanaume sawa na asilimia 49.69 na wapiga kura 49,174 ni watu wenye ulemavu,”alisema.

VITUO 99,911 VYA KUPIGIA KURA

Mwenyekiti huyo alisema vituo 99,911 vitatumika kupigia kura kwa Tanzania Bara ambapo, 97,349 vitatumika kwa ajili ya kupigia kura kwa Tanzania Bara na vituo 2,562 vitatumika kwa ajili ya kupigia kura kwa visiwani Zanzibar.

“Idadi hii ya vituo 99,911 ni sawa na ongezeko la asilimia 22.49 ya vituo vya kupigia kura 81,567 vilivyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020,” alisema.

Alisema kwa mujibu kifungu cha sheria idadi ya vituo 1,766 vilivyoko sasa kwa mujibu wa Daftari la Wapiga Kura la Tume ya ZEC, ni sehemu ya vituo vitakavyotumiwa na INEC kwa ajili ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na wabunge kutoka Zanzibar.

Kuhusu orodha ya wapigakura 8,703 waliokabidhiwa polisi, Kailima Ramadhan, wamewakabidhi Jeshi la Polisi kwa mujibu wa kifungu cha 114 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024.

Alisema ni kosa kujiandikisha zaidi ya mara moja na kwamba, orodha hiyo ina taarifa za namba ya mpigakura, majina ya wapigakura aliyotumia, jina la mkoa, halmashauri, kata, kituo, ina namba za simu na alama za vidole na picha alizopigwa kwenye vituo hicho. 

MAONI YA WADAU

Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, alisema uzinduzi wa kalenda ya uchaguzi ni hatua muhimu inayotoa nafasi kwa vyama kupanga mikakati, kuchora ramani ya ushindi na kujiandaa vyema na kampeni.

“Tunaiomba Tume iendelee kushirikisha vyama vya siasa katika hatua zote zinazofuata, ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki na huru,” alisema Ado. 

Katibu Mkuu wa Chama cha National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi), Dk. Eveline Munusi aliwatoa hofu Watanzania kwamba uchaguzi uko na tarehe imeshatajwa. 

“Tujitokeze kwa wingi kupiga kura na tuhimize utunzaji wa amani wakati wa kampeni na siku ya kupiga kura. Ulinzi wa amani unaanza kwa mtu mmoja mmoja,” alisisitiza.

Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, ambaye pia ni mgombea urais wa chama hicho, alisema maandalizi ya uchaguzi yameridhisha, jambo lililowasukuma kuingia rasmi kwenye kinyang’anyiro hicho.

 “Vyama vya siasa tunaingia kwenye kampeni kwa ustaarabu na kuwasilisha sera zetu kwa wananchi. Chama changu kinatarajia kuzindua Ilani ya Uchaguzi Agosti 5, ambayo imebeba matumaini makubwa kwa Watanzania. Tuna imani kuwa Tume itatenda haki,” alisema Doyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, ametaka mawakala kuapishwa kwa wakati ili kuondoa changamoto ambazo zimewahi kujitokeza huko nyuma.

Prof. Lipumba alisema utaratibu wa kuchukua na kurejesha kusiwe wa kuzuia watu kugombea kwa makosa madogo.

“Kuna watu wazuri wamejitokeza tunakwenda kuwaangalia watakaopeperusha bendera ya CUF, tutakutana Agosti 4-7, mwaka huu, mchakato wa ndani,” alisema.

Alisema katika mkutano mkuu ndio atajulikana mgombea urais na kwamba, kuna vijana wamejitokeza kutiania ya kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ikiwamo wa urais.