KATIKA historia ya Tanzania, ni nadra kumpata kiongozi anayeunganisha usikivu wa kweli na hatua za maana kama Rais Samia Suluhu Hassan, tangu aingie madarakani Machi 19, 2021.
Kwa kipindi cha miaka minne ameonesha uongozi wa kipekee unaoweka wananchi mstari wa mbele.
Mojawapo ya mafanikio yake makubwa ni mageuzi ya sera za makato ya miamala ya simu na benki, ambayo yamebadilisha maisha ya wafanyabiashara wadogo, wakulima na vijana.
Pia, ujenzi wa minara 8,500 ya mawasiliano ndani ya miezi 48 na uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 uliofanyika Julai 17, 2025.
Kwa uongozi wake tunaona ameweka msingi wa uchumi wa kidijitali unaowafikia wote.
Uchambuzi huu unaangazi usikivu wake umechochea mageuzi haya, athari zake za kimfumo, na nafasi ya Tanzania katika muktadha wa kimataifa.
MAGEUZI YANAYOBADILISHA
Rais Samia amejenga sifa ya kusikiliza wadau, ikiwa ni pamoja na wananchi, wafanyabiashara, na asasi za kiraia.
Mnamo Septemba 2022, baada ya malalamiko kuhusu tozo za miamala ya kielektroniki, Julai 2022 serikali ilifuta na kupunguza baadhi ya tozo, ikilenga kushusha gharama na kuhamasisha huduma za kidijitali. Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba.
Alisema hatua hiyo ilizuia tozo za mara mbili na kuongeza ushirikishwaji wa kifedha.
Uamuzi huo uliungwa mkono na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafantakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya alitoa maoni yake kutona na mabadiliko hayo akisema:
“Wametugusa na imetusaidia.” Hadi Julai 2025, Serikali ilipunguza gharama za miamala hadi Sh. 5,000, ikiwa chini ya Sh. 4,000 hadi Sh.12,000 za awali, na ikazindua Mfumo wa Malipo ya Papo Hapo Tanzania (TIPS), jukwaa linalowezesha miamala salama ya muda halisi.
Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba alisema hatua hizi zinasaidia wafanyabiashara wadogo na wakulima wa vijijini.
Baadhi ya wananchi wanaojishughulisha na uwakala kama Hellen Mosha, wakala wa simu huko Moshi, alisema: “Sasa naweza kuhamisha pesa bila wasiwasi wa makato makubwa, jambo linalonipunguzia gharama za biashara.”
MIUNDOMBINU YA KIDIJITALI
Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), zinaonesha kuwa kwa kipindi cha miaka minne Tanzania imejenga minara 8,500 ya mawasiliano ndani ya miezi 48, ikifanya jumla ya minara kufikia 9,278 ifikapo 2025, ikilinganishwa na 754 tu mwaka 2020.
Minara hiyo imefungua maeneo ya vijijini kwa mawasiliano, ikichochea biashara za mtandaoni na miamala ya kidijitali.
Kwa mfano, wakulima sasa wanapata taarifa za soko na kulipa wazabuni kupitia simu, huku wafanyabiashara wadogo wakipanua shughuli zao.
Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk. Mwinuka Lutengano alisema: “Ujenzi wa minara umewezesha huduma za kidijitali kufika mbali, na kupunguza gharama za miamala kumeongeza uchukuzi wake.”
“Hatua hii inaonyesha jinsi Rais Samia anavyochanganya uwekezaji wa miundombinu na mageuzi ya sera.
DIRA 2050
Uzinduzi wa Dira 2050 Julai 17, 2025 jijini Dodoma ulikuwa hatua ya kihistoria, ikihusisha wadau milioni 1.17, wengi wao vijana waliotoa maoni kupitia ujumbe mfupi wa maandishi na tovuti.
Waziri wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema Dira 2050 hii inalenga uchumi wa kipato cha juu ifikapo 2050, na Pato la Taifa la Dola trilioni moja.
Inasisitiza teknolojia, demokrasia, na uhifadhi wa mazingira, ikilenga asilimia 80 ya huduma za serikali ziwe za kidijitali.
Mageuzi ya makato ya miamala na ujenzi wa minara yanasaidia malengo haya kwa kuimarisha ushirikishwaji wa kifedha na umahiri wa kidijitali.
Aidha, Dira 2050 inalingana na (Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hasa SDG 9 (viwanda, uvumbuzi, na miundombinu), na Umoja ya Afrika (AU) Agenda 2063, ikiongoza Tanzania kuelekea
uchumi jumuishi unaohusiana na AfCFTA (Eneo la Biashara Huria la Afrika), ambapo huduma za kidijitali zitaongeza ushindani wa Tanzania katika Soko la Afrika.
MAGEUZI YA 2025
Julai 2025, Serikali ilipunguza gharama za miamala hadi Sh. 5,000 na ikazindua TIPS, ikiongeza uaminifu wa umma kwa huduma za kidijitali.
Dk. Lutengano alisema hatua hizi zitaongeza hamasa ya miamala ya kidijitali, huku Profesa Kinyondo akiongeza kuwa zinachochea uchumi kwa kurudisha pesa kwa watu.
Kamati ya Bunge ya Bajeti, kupitia Twaha Mpembenwe, ilishauri kuboresha Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa, na Mbunge Josephat Kandege akasisitiza kupunguza gharama ili kuzuia ukwepaji wa kodi.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipongeza TRA kwa kukusanya Sh. trilioni 32.26 akizidi lengo la Sh. trilioni 31.05.
Rais Samia alielekeza kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kama semina, kufidia nakisi ya Sh.bilioni 500 ya 2022.
KABLA YA MAGEUZI
Kabla ya 2022, gharama za juu za miamala zilizuia ushirikishwaji wa kifedha, kulingana na ripoti ya BoT ya 2022. TCRA iliripoti kupungua kwa miamala ya simu kutoka 117 mwaka 2019 hadi 100 mwaka 2023 kutokana na tozo.
Profesa Mshiriki wa Uchumi wa Maendeleo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abel Kinyondo alisema changamoto hizo pamoja na athari za vita vya Ukraine na COVID-19, ziliathiri mzunguko wa fedha.
Wakizungumzia jambo hilo, baadhi ya wananchi akiwamo Mkazi wa Mwanza, Alicia Rugemalila alisema walirudi kwenye pesa taslimu.
Ripoti ya Taasisi ya Twaweza ya 2022 ilionyesha asilimia 70 ya wakazi wa Dar es Salaam walipunguza matumizi ya simu kutokana na gharama, ikisababisha serikali kukosa Sh. trilioni 1.25.
ATHARI ZA KIMFUMO
Mageuzi haya yamebadilisha tabia za kifedha nchini Tanzania, na kwamba idadi ya akaunti za miamala ya
simu na benki imeongezeka kwa asilimia 17 kati ya 2023 na 2024, ikionyesha kuongezeka kwa uwajibikaji wa kifedha.
Wafanyabiashara wadogo sasa wanatumia huduma za kidijitali kwa malipo ya wazabuni, huku wakulima wakilipia mbegu kupitia simu. TIPS imepunguza uhalifu wa mtandaoni, ikiongeza usalama wa miamala.
Hata hivyo, Mtaalamu wa Uchumi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk. Lawi Yohana alisema tozo za kutoa fedha taslimu bado ni changamoto.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alionyesha wasiwasi kuwa marekebisho yanawafaa zaidi wanaotumia benki kuliko simu.
Mbunge Juma Hamad Omary alishauri kurekebisha pensheni za wastaafu kulingana na mfumuko wa bei.
TANZANIA KIMATAIFA
Katika mataifa mengi ya Afrika Mashariki na Global South, gharama za miamala ya simu zimebaki changamoto, mathalani nchini Uganda, tozo ya miamala ya simu ya 2018 ilizua mjadala mkali
lakini haikupunguzwa kwa kiasi kikubwa hadi 2025.
Kenya ilishuhudia ongezeko la gharama za huduma za kidijitali baada ya kuongeza VAT kwenye miamala ya simu, ikipunguza uchukuzi wa huduma.
Tofauti na nchi hizi, Tanzania imepunguza makato bila kuathiri mapato ya serikali, ikiifanya iwe mfano wa kuigwa.
“Hatua hizi zinaonyesha uwezo wa kusikiliza wananchi huku zikidumisha uthabiti wa kifedha, na zinalingana na malengo ya AfCFTA ya kuimarisha biashara ya kidijitali barani Afrika,” anasema.
MAISHA YALIYOBADILIKA
Mageuzi haya yamegusa maisha ya Watanzania wa kawaida. Consolatha Costatine, mwanafunzi wa miaka 22 huko Morogoro, alisema: “Sasa ninalipa ada za chuo kwa simu bila makato makubwa, nikiokoa pesa za vitabu.”
Mfanyabiashara wa mjini Geita, Ikorongo Oto, alisema:
“Kupunguzwa kwa gharama kumenisaidia kulipa wazabuni kwa wakati, na mtandao bora umenifungulia masoko mapya.”
Hadithi hizi zinaonyesha jinsi mageuzi yanavyochochea maendeleo ya kibinafsi na kijamii.
Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya lugha na uchumi, na Mhadhiri msaidizi Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT). Anapatikana kwa namba ya simu 0717665540
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED