ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma, Beatus Kinyaiya, amesema ni jambo jema mwanadamu anayefanya shughuli ya uzalishaji na kupata kipato, kujenga tabia ya kuweka akiba ya fedha sehemu salama, ikiwamo benki, ili zimsaidie wakati wa uzeeni.
Askofu Kinyaiya, amesema hayo mwishoni mwa wiki, kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa Benki ya Mkombozi, uliofanyika jijini Dar es Salaam.
“Kuna watu ambao wamefanya kazi kwa miaka mingi lakini wanapostaafu wanajikuta hana, hohehahe, chochote, mwombaji. Nawahimiza watu wote tupende kuweka fedha benki.
“Pia kiasi fulani tuwekeze akiba ya muda mrefu ikusaidie mbele ya safari kwa ajili ya maendeleo yako na familia,” alisema Askofu Kinyaiya.
Amesema kwamba ilipoanzishwa mifumo rasmi ya kuhifadhi fedha, malengo ni kumkomboa aliye mdogo kabisa, kwa kumpatia mkopo.
“Tumejikita kweli kuwasaidia wale ambao kweli wanahitaji msaada, ili kuwasaidia hawa wadogo lazima tupate fedha za kuwakopesha. Fedha tunazipata kwa ambao wanawekeza, nahimiza kwanza tuache tabia ya kuweka fedha chini ya godoro, tuweke benki.
“Tupo karne hii bado kuna watu wanaficha fedha sehemu zisizofaa, benki zikiwa na fedha zitasaidia maendeleo na kumsaidia mdogo aamke,” amesema Askofu Kinyaiya.
Awali, Mwenyekiti wa bodi hiyo, Gasper Njuu, amesema kwamba mfumo wa kidijitaliu umeleta mabadiliko ya kiuchumi ikiwamo wa usimamizi wa fdeha shuleni, hospitalini, vyuoni, huku wakianzisha huduma ya Sadaka Dijitali.
“Tutajikita katika kutoa mikopo zaidi ambayo ni salama, viashiria vyote vya hatari vinasimamiwa kikamilifu ili kukuza huduma katika sekta ya kifedha,” amesema Njuu.
Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Respige Kimati, amesema miongoni mwa changamoto kwenye utoaji huduma ni kuwakopesha waliopo sekta binafsi kwa kuwa walio wengi huzalisha mikopo chechechfu na wengine kukimbia.
“Hivyo mara kadhaa wakopeshwaji wa mikopo hiyo wamekuwa wakipewa kipaumbelea zaidi watumishi wa umma, kwa kuwa huwa rahisi kuwafuatilia kutokana na mifumo iliyopo. Lakini sekta binafsi akiachishwa kazi ni vigumu kumfuatilia, utampata wapi?” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED