TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imesema itahakikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unakuwa huru, wa uwazi, wa haki na wa kuaminika kwa kuweka mazingira sawa ya ushindani kwa wagombea na vyama vyote vya siasa vitakavyoshiriki.
Akifungua leo mkutano huo jijini Dodoma katika mkutano wa kitaifa wa Tume hiyo na Vyama hivyo kuhusu uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji (Rufaa),Jacobs Mwambegele, amesema Tume itahakikisha inasimamia Katiba, Sheria na Kanuni ili kila mwenye sifa ya kugombea anapata haki ya kupewa na kuteuliwa pale atakapotimiza masharti ya uteuzi.
Aidha, amesema katika kipindi cha Kampeni, Tume hiyo inawahakikishia kuwapo kwa uwanja sawa kwa vyama vyote wakati wa kampeni.
Amesema watahakikisha kila chama kitafanya mikutano yake kwa mujibu wa ratiba itakayokuwa imepitishwa na kamati ya ratiba ngazi ya Taifa inayoratibu ratiba ya kampeni ya wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais, kamati ya jimbo inayoratibu ratiba ya wagombea wa ubunge na kamati ya kata inayoratibu ratiba ya wagombea wa udiwani.
“Kipindi cha kampeni kunakuwa na joto kali la kisiasa linalotokana na baadhi ya watu
kukosa uvumilivu wa kisiasa hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.”
“Napenda kutoa rai kwenu na wafuasi wenu kwa kuwasihi kufanya kampeni za kistaarabu na hivyo kuepuka kufanya vitendo vitakavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi yetu,”amesema.
Amewasihi wasome sheria, kanuni na maelekezo ya Tume ili ushiriki wao katika mchakato wa uchaguzi ufanyike kwa kuzingatia masharti na matakwa ya sheria, kanuni na maelekezo husika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED