ZAIDI ya washiriki 300 wamejitokeza na kuchangia mapendekezo ya namna bora ya kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya 2050, kutimia huku wakikazia msimamo wa Pato la Taifa kufikia dola trillioni moja .
Wasomi na wananchi wametoa mapendekezo hayo katika kongamano lililoandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), kwa kushirikiana na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet), ili kuhakikisha Tanzania inafikia pato hilo, ili kukuza uchumi na kuboresha maisha ya kila mmoja
Prof. Adelardus Kilangi ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, akizungumza katika kongamano hilo ameweka wazi kuwa, ili kufikia adhima hiyo kunapaswa kuwapo na uchambuzi wa siasa uchumi kwenye faida na changamoto za dhana ya ubia.
Anasema ili kuimarisha ushirikiano madhubuti kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), kunahitajika kuwepo kwa uelewa na mawasiliano kati ya sekta binafsi na ya umma katika utekelezaji wa miradi ya ubia.
Anaeleza kuwa chakuangazia ni namna ambavyo usuluhishi wa migogoro ya kitaifa, umuhimu wa kushughulikia masuala hayo hasa katika mikataba ya kitaifa, kuleta tija, kwa sababu nchi nyingi zinapoteza fedha, kwa sababu hakuna maandalizi madhubuti ya kutatua migogoro kisheria.
"Tunachopaswa kukiangazia ni ujamaa ,uzalishaji wa utajiri na ugawaji wa mapato hayo tatizo lugha inayozungumzwa na sekta hizi mbili, bado haijaungana tunahitaji tafiti za kina kuhusu historia ya PPP.
“Ili kubaini kwa nini kumekuwa na tatizo pamoja na uhusiano wa siasa na sheria na namna sera zetu zinavyounga mkono au kudhoofisha ushirikiano huu,” amesema Prof. Kilangi.
Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila, ameonesha dhamira yake ya kufikia uchumi wa dola trillion moja, akieleza kuwa hayo ni malengo ambayo yanatekelezeka na ni wajibu wa kila mtu kushiriki, ili kufikia azma hiyo.
Anaeleza kuwa sera na sheria ya ubia ina ushindani katika utekelezaji wa miradi, hivyo wanazuoni wanapaswa kushirikiana kufanya tafiti, ili kubaini changamoto hizo.
“Japokuwa Tanzania imeweka mazingira bora ya sheria na sera, ili kuimarisha nafasi ya ubia kwenye uchumi wa Tanzania na tayari matokeo ya awali yameanza kuonekana na yatakuwa wazi zaidi kwenye utekelezaji wa Dira.”
Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo cha Mtakatifu Agoustino(SAUT), Mwanza, Dk.Delphine Kessy, anaweka wazi kuwa, ili kufanikisha hayo kuwapo na chombo maalumu ambacho kitasimamia ubia pia kifanye utafiti na kusaidia PPPC, kuondoa makosa yaliyojitokeza nyuma na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Anasema endapo watanzania wana uwezo wa kuwekeza vizuri na hakuna sehemu ya kuwekeza na kuuza vizuri, hakutakuwa na maana hivyo, kinachojhitajika ni mitaji ya nje, kwa sababu watu hao wanawahitaji.
Dk. Ponsian Ntui kutoka SAUT, amesema kinachopaswa kufanyika ni kukuza sekta binafsi ya wazawa yenye nguvu, ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Anaeleza kuwa wakati umefika wa wataalamu kuwa na uwezo wa kubadilisha mpango kuwa matokeo kipaumbele kikiwa ni kuwekeza kwa watu kuboresha mazingira ya biashara, ili yaweze kuwavutia wawekezaji.
Anasema kuwa serikali ya mitaa, inatakiwa kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha wanakuwa na teknolojia ya kisasa ya ukusanyaji wa taka, kisha kuchakatwa na kutengeneza bidhaa nyingine ambayo itasaidia kulinda mazingira pamoja na kukuza uchumi.
Khadija Khamis, mwanafunzi wa kidato cha sita aliyehudhuria kongamano hilo, ameitoa wito kwa serikali kuboresha ufundishaji wa masomo ya uchumi na biashara katika shule za sekondari, ili kuwajengea wanafunzi msingi imara wa kushiriki kwenye uchumi wa nchi.
Easter Chuwa, ameeleza kuwa suala la teknolojia lipewe kipaumbele, ili iweze kutumika katika kukuza sekta mbalimbali na kufikia uchumi imara pia kuwe na chombo maalumu cha kusimamia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mohamedi Juma, ni mwananchi aliyepata fursa ya kuhudhuria kongamano hilo, anaeleza kuwa amepata uelewa kuhusu maendeleo endelevu imani yake dira hiyo itakwenda kutatua migogoro na kuboresha maisha ya wananchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED