WAKAZI wa Kata ya Kwedizinga, wilayani Handeni, wamejawa na furaha mwishoni mwa wiki, mara baada ya Shirika la World Vision, kuwakabidhi mradi wa maji wa Mkumburu AP.
Mradi huo utawawezesha wakazi zaidi ya 4,500 kutoka katika vijiji mbalimbali vya kata hiyo kunufaika.
Akikabidhi mradi huo wa maji ya kisima mwishoni mwa wiki, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, amewashukuru wadau hao wa maendeleo kwa kuwaondolea adha ya maji wakilazimika kutembea umbari wa km 5 kufuata huduma ya maji kwenye mto,
"Awali wakazi wetu walilazimika kutembea umbari wa kilomita tano, kufuata huduma ya maji, tunashukuru sana kufanikisha mradi huu, na sasa akinamama watakuwa na furaha kubwa sana, hawatotembea umbali mrefu kufuata huduma hii, muhimu ya maji," amesisitiza Nyamwese
Amewataka wananchi kuhakikisha wanautunza mradi huo pamoja na mazingira, ili kulinda vyanzo vya maji.
Mkurugenzi wa shirika hilo, James Anditi, amesema mradi huo umegharimu Sh. mil. 297.6 hadi kukamilika kwake, umetekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza uligharimu Sh. mil 245.8 na awamu ya pili uligharimu Sh. mil. 51.8.
"Upanuzi huu wa mradi wa awamu ya pili, umewezesha kufikia vitongoji viwili vya Mlangali kituo kimoja cha Mnyundo chenye vituo vinne, benki ilichangia Sh. mil 50 na wakazi wa Kwedizinga walichangia mil.1.8,” amesisitiza James Anditi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED