CHAMA Cha ACT-Wazalendo, kimesema iwapo kitaingia madarakani kitahakikisha huduma za afya, elimu, ardhi, zinapatikana kwa ukamilifu na kuhakikisha changamoto zilizopo sasa hazijirudii.
Hayo yamesemwa jana, mkoani Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara, Isihaka Mchinjita, alipoeleza mambo waliyo yabaini katika ziara yao ya siku 15 iliyopewa jina la 'Operesheni mMajimaji' ilivyokuwa inawahamasisha wananchi kulinda kura zao kipindi cha uchaguzi.
Akianza kwa kuzungumzia eneo la afya, Mchinjita amesema chama hicho lazima kitarejesha thamani ya hospitali, vituo vya afya na zahanati kama sehemu za matibabu na matumaini.
Amesema pia kitahakikisha wauguzi na watumishi wa sekta ya afya wanahudumiwa vizuri na wanasimamiwa ipasavyo, ili kutoa huduma zinazozingatia misingi ya usawa, haki na weledi wa kazi.
Katika sekta ya elimu amesema chama hicho, kitahakikisha kinamaliza tatizo la upungufu wa walimu na miundombinu katika shule zote nchini.
"ACT-Wazalendo tunasisitiza kwamba sekta ya elimu lazima ifumuliwe na kusukwa upya, kuendana na hali ya ulimwengu na maendeleo ya jamii na kiteknolojia.
"Ila kabla ya hayo, tutahakikisha kwamba tunasitisha na kuondosha michango yote ya fedha, chakula na mengineyo," amesema Mchinjita huku akisisitiza hata ilani yao watakayoiandaa itakwenda kujibu changamoto hizo.
Kuhusu kilimo, amesema chama hicho kitahakikisha serikali inashiriki kikamilifu kuinua na kuiendeleza sekta hiyo, kwa kutenga zaidi ya asilimia 10 ya bajeti na kuweka mfumo wa kudhibiti anguko la bei ya mazao.
Ameendelea kueleza kwamba pamoja na hayo, watahakikisha unakuwapo mfumo wa ushirika unaosimamiwa na wakulima wenyewe na sio kwa urasimu.
Kadharika amesema watashughulika na mzizi wa migogoro ya ardhi, kwa kufanya uhakiki wa mipaka nchi nzima, kupunguza eneo la hifadhi na kisha kuweka mpango wa matumizi bora kote nchini.
"Pamoja na haya, tunasisitiza kwamba njia pekee ya kushughulika na uvamizi wa tembo na wanyamapori waharibifu ni kuwavuna na chama chetu kitalisimamia zoezi hili kama linavyoruhusiwa na sheria za nchi," amesema Mchinjita
Amesema katika ziara hiyo walishuhudia nyuso za watanzania, zimejaa huzuni kwa kile alichodai zina viashiria vyote vya kuchoshwa na uongozi butu unao ongozwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
"Tumechoshwa na uongozi usiokuwa na maarifa ya kutumia rasilimali gesi iliyoko Lindi na Mtwara, kwa ajili ya kuzalisha umeme na ajira na kugeuza mikoa hiyo kama kitovu cha uchumi kusini mwa Tanzania.
"Tumechoshwa na uongozi usiokuwa na maono na dira na kuacha chuma na makaa ya mawe kulala katika mikoa ya Ruvuma na Njombe, huku mamilioni ya watanzania wakiwa hawana ajira," amesema Mchinjita
Ziara hiyo ilianza Julai Mosi, mwaka huu na kitamatika Julai 15, mwaka huu, huku viongozi wakuu wa chama hicho wakijigawa katika makundi mawili moja likiongozwa na Kiongozi mstaafu Zitto Kabwe na jingine likiongozwa na kiongozi wa chama, Dorothy Semu.
Katika ziara mikoa ambayo ilifikiwa na chama hicho ni pamoja na Tanga, Dar es Salaam, Tabora, Katavi, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Mtwara, Lindi na Pwani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED