Wanafunzi 7,000 kufikiwa mradi elimu usalama barabarani

By Christina Mwakangale , Nipashe Jumapili
Published at 04:02 PM Jul 27 2025
Wanafunzi kupewa elimu usalama barabarani
Picha: Mpigapicha Wetu
Wanafunzi kupewa elimu usalama barabarani

WANAFUNZI 7,000 kutoka shule saba nchini, watafikiwa na mradi wa uelewa wa kina wa elimu ya usalama barabarani, kupitia sanaa ya uchoraji, ili kupunguza ajali kwa kundi hilo wanapokwenda na kurudi kutoka masomoni.

Watakaonufaika ni wanafunzi kutoka shule Makuburi, Buza, Ubungo National na Shule ya Msingi Buguruni ya Viziwi zote za Dar es Salaam); Mnadani (Dodoma) na Ndalala sekondari (Temeke).

Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Temeke, Sadath Mtware, amesema hayo Dar es Salaam, katika shule ya sekondari Ndalala iliyopo Temeke ikiwa ni mara ya kwanza kwa mradi huo kufanyika katika ngazi ya sekondari.

“Mradi huo utachangia juhudi za serikali za kukabiliana na ajali za barabarani, kwa sasa Temeke ajali za barabarani zimepungua kwa kiasi kikubwa, kutokana na mikakakati imara iliyowekwa kudhibiti ajali za barabarani,” amesema Mtware.

Pia amezitaka taasisi za umma na kampuni nyingine binafsi, kujitokeza kushiriki juhudi hizo, kutoa elimu kwa kundi hilo ili kupunguza ajali.

“Kaika harakati za kuimarisha elimu ya usalama barabarani na kukuza ubunifu miongoni mwa vijana, kampuni ya Total energies, imezindua rasmi toleo la mwaka 2025 la ‘Via creative’ katika shule ya sekondari Ndalala.

“Kupitia mradi huu uliolenga kutoa elimu ya usalama barabarani, kwa wanafunzi kupitia vipaji ama sanaa ya uchoraji, kukabiliana na ajali za barabarani,” amesema.

Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano kutoka kampuni hiyo, Getrude Mpangale, alifafanua kupitia mradi huo ulioanzishwa mwaka 2022, ambao tayari umewafikia zaidi ya wanafunzi 22,000 wa shule za msingi katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Wanafunzi kupewa elimu usalama barabarani
“Lengo ni kuwajengea vijana uelewa wa kina kuhusu usalama barabarani, kukuza ubunifu wao na kuwawezesha kuongoza mabadiliko katika jamii zao,” amesema Mpangale.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Ndalala, Silvia Majaliwa, ameeleza kwamba mradi huo si tu utawawezesha wanafunzi kuwa mabalozi wazuri wa masuala ya usalama barabarani kwenye jamii, pia watakuza vipaji vyao kupitia sanaa ya uchoraji.

Wanafunzi kupewa elimu usalama barabarani
Mwanafunzi James Kamote, ameeleza kufurahishwa na uwapo wa mradi huo, kwa kuwa wataweza kujikinga nakuepukana na ajali za barabarani.