MAZOEZI ya mwili ni kinga muhimu dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, husaidia kuimarisha mzunguko wa damu, kupunguza mafuta mwilini, kudhibiti uzito na kuongeza nguvu ya moyo pamoja na mapafu kufanyakazi.
Vilevile, mazoezi husaidia kupunguza msongo wa mawazo, kuboresha usingizi na kuongeza nguvu ya mwili na akili kufanya kazi kwa ufanisi.
Lakini pamoja na umuhimu wake, wataalam wa mazoezi wanasema sehemu kubwa ya Watanzania, hasa walioko mijini, hawafanyi mazoezi na wanaofanya si ya kutosha.
Katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii, Mkazi wa Mwananyamala, Dar es Salaam, Pendaeli Damas anakiri katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, Tanzania imeshuhudia ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza.
“Wakati familia ya jirani yako kuna mtu anaugua figo, nyumbani kwako au ndugu kuna mtu ana kisukari, mwingine shinikizo la damu, magonjwa ya moyo au saratani, na sasa tunashuhudia tatizo la msongo wa mawazo unaouwa watu kimya kimya,” anasema.
Damas anasema kati ya sababu kuu zinazochangia kuenea kwa kasi kwa magonjwa hayo, wataalam wanasema ni pamoja na mtindo wa maisha usiofaa, ulaji usio na mpangilio, matumizi ya vileo na tumbaku, pamoja na kutofanya mazoezi ya mwili.
“Mabadiliko ya maisha, hususan katika miji, yamesababisha watu wengi kupunguza shughuli za mwili na kubadili aina ya lishe, hali inayochochea kuongezeka kwa magonjwa haya.
“Mfano, mimi ninafanyakazi Posta ninatoka nyumbani kwangu na gari, nikifika ninaegesha gari nje ya jengo la ofisi ninapanda lifti.
“Nikiingia ofisini shughuli zangu ni za kukaa zaidi, nikisimama labda naenda kumuuliza mtu kitu au naelekea msalani, au kula, nikitoka naingia kwenye gari narudi nyumbani, nikishakula chakula mara nyingi saa mbili au saa tatu ninalala kwa ajili ya kuwahi kesho yake ofisini,” anafafanua.
Mkazi wa Kigogo Sambusa, Dar es Salaam, Salma Iddi anasema watu wengi hawafanyi mazoezi na sababu kubwa ni ukosefu wa muda kutokana na majukumu ya kazi, kutokujua umuhimu wa mazoezi, na ukosefu wa maeneo salama ya kufanyia mazoezi.
“Wengi tuna mtazamo potofu kuwa kufanya kazi za kila siku kama kufagia au kuosha vyombo kunatosha kuwa mbadala wa mazoezi, sidhani kama inatosha.
“Mtu anaweza kuruka kamba, kutembea, kukimbia lakini pia yako mazoezi ya viungo ambayo unaweza kuyafanya nyumbani kwako ukawa umetoka jasho na mwili kufanya kazi vizuri,” anasema.
Anataja changamoto nyingine ni kwa vijana ambapo wengi wanashawishika zaidi kutumia muda wao katika mitandao ya kijamii au kutazama runinga kwa muda mrefu badala ya kushiriki shughuli za kimwili.
“Inaongeza uwezekano wa kupata uzito mkubwa kupita kiasi (obesity), hali ambayo ni kichocheo kikubwa cha magonjwa yasiyoambukiza,” anasema.
Salma anasema kuna haja ya kuweka mkazo mkubwa katika elimu ya afya kwa umma kuhusu umuhimu wa mazoezi na namna ya kuyafanya kwa njia rahisi na salama kwa kushirikisha watu wengi.
“Tunajua baadhi ya taasisi na baadhi ya maeneo kuna mwamko wa mazoezi ingawa si mkubwa na hufanyika kwa matukio maalum. Tunapaswa jambo hili libebwe na taasisi zote kwa wiki kila angalau ikiwezesha wafanyakazi wake kushiriki kwa pamoja mazoezi baada ya muda mwamko utakuwapo wa mtu mmoja mmoja,” anasema.
Shujaa wa ugonjwa wa kisukari, Aziz Mgai, anasimulia namna alivyogundulika kuwa na tatizo hilo kuwa ni baada ya kuugua ugonjwa wa malaria, homa ya matumbo na alipokwenda kupima ndipo akaambiwa pia kisukari.
Anasema katika jamii wengi huamini mtu anapopata changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza amerogwa.
“Hii inatokana magonjwa yasiyoambukiza hayaji kama magonjwa mengine, mfano mtu anajiuliza huyu hanywi pombe inakuwaje anapata matatizo ya moyo, kisukari, kifafa, saratani au shinikizo la damu, marathi ambayo huwa tunaamini hupata wazee.
“Nilipoambiwa nina tatizo kama hili sikuamini, hata shangazi yangu aliamini nimerogwa, na mimi nilijua nimerogwa kwa sababu niliamini magonjwa haya ni kwa wazee tu. Lakini kumbe kwa sasa mtu anazaliwa ana tatizo la sukari,” anasema.
Shujaa huyo anaonya wale wanaojisikia vibaya katika mwili na kukimbilia duka la dawa badala ya hospitalini, akisema hayo ni matumizi yasiyo sahihi ya dawa na mwisho wa siku hutengeneza usugu na kuchangia maradhi.
MTALAAM MAZOEZI
Mtaalam wa Afya na Mazoezi kutoka Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), Dk. Waziri Ndonde, anaitaka serikali kutia mkazo utekelezaji wa sheria.
Akizungumza na Nipashe, Dk. Ndonde amesema nchi ina sheria ya usalama barabarani, mipango miji, ujenzi wa barabara na namna ya kuzitumia.
Kadhalika, anasema kuna sheria ya mtu anapoanzisha shule anapaswa kuzingatia pamoja na mambo mengine kuwe na kiwanja cha michezo, lakini baadhi hawalifuati hilo.
Anasema ameona sheria inaruhusu ujenzi wa barabara za waenda kwa miguu, lakini hakuna mkazo wa kisheria kuzuia watu ambao hawapaswi kuzitumia mfano vyombo vya moto kupita au kuweka biashara maeneo hayo.
“Eneo la Tanzanite ni moja ya juhudi ambazo tulifanya kuonesha mfano, na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitoa wito kuhakikisha kunakuwa na eneo lililotengwa kwa siku moja watu kukusanyika na kufanya mazoezi na limeonesha mabadiliko makubwa.
“Tunaona vyombo vyote vya kutekeleza sheria vinatekeleza, baada ya Waziri Mkuu kuongea siku ile barabara ile ifikapo saa 12 asubuhi inafungwa na saa tatu asubuhi inafunguliwa.
Dk. Ndonde anasema bado kuna baadhi ya maeneo ambayo barabara hazifungwi, watu hawafuati sheria, na kuna ambayo ni njia ya waenda kwa miguu, kumepangwa biashara, watu wanapishana na magari barabarani.
“Mfano, Watanzania tunawadharau watu wanaotembea kwa miguu na wanaoendesha baiskeli, tunafikiri tunaoendesha vyombo vya moto tumepatia maisha, kitu cha msingi, dunia imeumbwa watu watembee zaidi wajenge afya zao,” anasema.
Anatolea mfano, nchi ya Finland, kila raia mmoja nchini humo kwa kuweka uwiano wa baiskeli, mtu mmoja ana baiskeli nne, hivyo kama kuna watu milioni 10 kuna baskeli milioni 40.
Anasema nchi hiyo ni iliyoendelea kiuchumi na wana magari mengi kuliko Tanzania, lakini wanazingatia sheria walizojiwekea na kuipunguzia serikali mzigo wa kutibu magonjwa yasiyoambukiza.
“Ninatoa wito kwa serikali za mitaa, na kata kila kiongozi wake kuhakikisha katika maeneo yao kuna maeneo huru ya watu kufanya mazoezi.
“Katika kila barabara ambayo imetengwa sehemu ya kutembea kwa miguu au kuendesha baiskeli ziachwe wazi ili watu watembee na kufanya mazoezi.
Anasema lengo kubwa ni watu wengi kushiriki kufanya mazoezi, ili kupunguza mzigo mkubwa wa magonjwa yasiyoambukiza na kuiondolea serikali mzigo mkubwa wa matibabu kama wanavyofanya nchi nyingine.
Kadhalika, Dk. Ndonde ametaka wananchi kuheshimu sheria za usalama barabarani, kwa kujenga tabia kwamba wanapomwona mtu anatembea barabarani si maskini, anajenga afya yake.
Anasema jukumu kubwa la watu wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza kubwa ni kujikubali, kujitambua na kujihudumia wenyewe ili kupunguza mzigo wa ugonjwa.
Anasema mtu anapokuwa na magonjwa na kutofuata masharti ya mtoa huduma wa afya au daktari kama dawa, kufanya mazoezi na lishe, ugonjwa huwa mkubwa zaidi.
“Kuna watu wanakatwa miguu, kuna watu wanakosa nguvu za kiume, wengine wana matatizo ya figo au matatizo ya macho, hivyo watoa huduma ngazi ya jamii hupewa elimu ya kusaidia wananchi, na wanapoona tatizo linaongezeka wanatoa rufani za wagonjwa,” anasema.
Mei 17, mwaka huu, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, katika maadhimisho ya Siku ya Shinikizo la Juu la Damu Duniani, miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza alisema:
“Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), vifo vingi vinavyotokana na shinikizo la juu la damu hutokea kati ya umri wa miaka 39 hadi 79.
“Takribani asilimia 33 ya vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza husababishwa na hali hiyo. Nchini Tanzania, takwimu kutoka Mfumo wa Ukusanyaji wa Taarifa za Afya Nchini (DHIS2) zinaonesha ongezeko la wagonjwa kutoka 1,315,000 mwaka 2019/2020 hadi 1,665,019 mwaka 2023/2024,” anasema.
Dk. Mollel anasema miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza, shinikizo la damu ndilo linaongoza kwa idadi ya wagonjwa wanaopata matibabu katika vituo vya afya.
Kwa mujibu wa WHO, mtu mzima anatakiwa kufanya mazoezi ya angalau dakika 150 kwa wiki. Hii ni sawa na dakika 30 kila siku kwa siku tano.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED