DC Msando aonya mikusanyiko isiyo rasmi waumini wa Gwajima

By Imani Nathaniel , Nipashe Jumapili
Published at 12:47 PM Jul 27 2025
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando
Picha: Imani Nathaniel
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando

MKUU wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, ametoa kauli kuhusu uvumi wa kufungwa kwa ukumbi wa Tanzanite ulioko Kimara Korogwe,Dar es Salaam, akibainisha kuwa ukumbi huo umesajiliwa kwa ajili ya shughuli za biashara na si ibada.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Msando alisema ukumbi wa Tanzanite ulitumiwa na Kanisa la ABC kutoka Shinyanga kwa ajili ya semina ya kidini ambayo ilimalizika siku ya Ijumaa. 

Alisema binafsi alifika ukumbini huko na kuzungumza na viongozi wa dini waliokuwapo, bila kuchukua hatua yoyote kwa kuwa shughuli iliyoombewa ilikuwa ni matumizi ya semina.

Msando ameonya dhidi ya waumini wa Kanisa la Gwajima, ambao alisema wamekuwa wakitumia makanisa na maeneo mengine kwa mikusanyiko isiyo rasmi baada ya kanisa lao kufungiwa kutokana na ukiukwaji wa taratibu.

 “Ukumbi wa Tanzanite haukusajiliwa kwa ajili ya ibada. Walioomba semina ni Kanisa la ABC, siyo waumini wa Gwajima. Kwa hiyo, mikusanyiko ya aina hiyo ni marufuku,” alisema Msando.

Alisema waumini waliotakiwa kufika ofisini kwake hawakufanya hivyo, badala yake walikwenda mahakamani na kisha kuhamia katika kanisa lingine bila ruhusa, jambo ambalo ameliita ni kinyume cha sheria.

“Haki ya kuabudu iko, lakini lazima ifuate utaratibu. Viongozi wa Gwajima wasithubutu kufanya mikusanyiko isiyo rasmi ndani ya Wilaya ya Ubungo,” alisema.

Msando ametoa wito kwa bodi ya wadhamini wa Kanisa hilo kufuata maagizo, huku akimtaka kiongozi mkuu wa kanisa hilo kujitokeza kwa mazungumzo ya amani ili kutafuta suluhisho la kudumu.